Zinazobamba

CUF YALAANI MASHAMBULIZI DHIDI YA PADRI KITIMA

 ```THE CIVIC UNITED FRONT (CUF- Chama Cha Wananchi)

TUNALAANI MASHAMBULIZI DHIDI YA PADRI CHARLES KITIMA:

Chama Cha Wananchi CUF kinasikitishwa na matukio yanayojirudia mara kwa mara ya Watanzania wenye hadhi tofauti kwenye jamii kutekwa,kuteswa na hata kuuawa na watu wanaodaiwa 'KUTOJULIKANA'. 

Ikiwa ni miezi tisa (9) tangu aliposhushwa kutoka  garini na baadae kuripotiwa kuuawa, Kiongozi wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo Mhe. Ali Kibao wakati wa 'mshike mshike' wa kuelekea kwenye Mkutano Mkuu wa Uchaguzi wa Chama hicho, tunapokea kwa huzuni na mshtuko mkubwa taarifa ya kushambuliwa kwa Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu wa Kanisa Katoliki (TEC), Padri Charles Kitima na kuumizwa vibaya.

Vyovyote iwavyo, na bila kujali nani anatekeleza uharamia huu, TUNALAANI vikali mfululizo wa matukio haya ambayo Jeshi la Polisi linakosa upenyo wa kujivua uhusika. 

Watanzania huwa tunafarijika pale majeshi yetu, hususan Jeshi la Polisi, yanapojitokeza mbele ya Umma wa Watanzania kudhihirisha Kuimarika kwake Kiweledi na kwa vifaa madhubuti katika kupambana na Uhalifu na mbinu bora za kisasa za Uchunguzi na Upelelezi. 

Kuendelea kutokea kwa matukio haya bila ya watuhumiwa kukamatwa na hatimaye kufikishwa mahakamani kunazalisha maswali mengi kuliko majibu juu ya nafasi ya Jeshi hilo kwenye Kadhia hizi.

Aidha, kuwepo kwa Taarifa zilizotolewa na Dkt Wilbroad Silaa, alipoteuliwa kuwa BALOZI,  zinazokituhumu CHADEMA kuwa na Kikosi Maalum cha Utekaji na Utesaji na bado Jeshi hilo halijatoka hadharani na kusema ni kwa namna gani limefaidika na taarifa alizotoa Dkt Slaa, kwa kumhoji ipasavyo, ni ishara kwamba Jeshi hilo haliko tayari kutumia taarifa muhimu kufanikisha Upelelezi unaoweza kupunguza vilio kwa Watanzania.

Tukio hili kutokea siku chache baada ya kutolewa kwa Kauli Kinzani na TEC na baadaye Mwadhama Kardinali Protase Rugambwa ambazo kiini chake ni Kesi ya Uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa CHADEMA Mhe. Tundu Lissu ni jambo linaloongeza mkanganyiko, hofu na taharuki.

CUF- Chama Cha Wananchi kinatoa wito kwa Serikali chini ya Dkt Samia Suluhu Hassan kuwajibika kukomesha haraka matukio haya yanayoashiria kiwango cha chini cha Usalama wa Watanzania, kinyume na matumaini wanayopewa wakati wa Kushuhudia Majeshi yetu wakati wa Dhifa mbalimbali za Kiserikali. 

Watanzania wanatarajia kusikia angalau Ripoti za Awali zinazohusu Uchunguzi kuhusu Kadhia za Utekaji, Utesaji na Mauaji yanayoongeza taharuki kila uchao. Tunatoa wito kwa Serikali kwa kujua kwa uhakika kwamba Serikali ndiyo inayopaswa kuwa na Majibu na si Viongozi wa Kitaifa wa CCM.

Kujitokeza Mbele ya Waandishi wa Habari, kwa Katibu Mkuu wa CCM Septemba 13, 2024 na kutoa maelezo ambayo hayakuleta nafuu yoyote ya kutokomeza matendo haya ni Kielelezo cha Matumizi mabaya ya 'Kofia' miongoni mwa viongozi wa CCM, hali inayotokana na Serikali na Vyombo vyake kutowajibika ipasavyo. 

Ndiyo maana haikuwa ajabu kwa Dkt Nchimbi kutumia Jukwaa lisilo muafaka kuzungumzia 'MARIDHIDHIANO YA KISALITI'  YALIYOKUWA YANAENDELEA KWA SIRI KUBWA BAINA YA CCM, CHADEMA NA ACT-Wazalendo kabla hawajageukana.

CUF- Chama Cha Wananchi kinatoa Pole kwa Padri Kitime na wale wote wanaokutwa na matukio haya na kuwaombea wapone haraka na kurudi kwenye majukumu yao.

HAKI SAWA KWA WOTE!

Eng. Mohamed Ngulangwa 

Mkurugenzi wa Habari, Uenezi na Mahusiano na Umma 

CUF- Chama Cha Wananchi 

Mei 2, 2025```

No comments