JUKWAA LA WAHARIRI WAMSHUKIA PROFESA LIPUMBA,NI KUHUSU ''MUNGIKI WAKE''SOMA HAPO KUJUA

Jukwaa la Wahariri nchini (TEF) limelaani kitendo cha waandishi wa habari kujeruhiwa katika tukio la uvamizi lililotokea katika mkutano wa CUF katika hotel ya Vina kata ya Mabibo ambapo waandishi wa habari walipigwa na kujeruhiwa

Katika taarifa hiyo ya (TEF) imemtaka Profesa Lipumba kujitokeza na kukiri na kuomba radhi kwa waandishi wa habari pamoja na Watanzania kufuatia tukio hilo kama alivyofanya Maalim Seif

"Tunamtaka Profesa Lipumba binafsi atoe kauli kuhusu tukio hili kama alivyofanya Maalim Seif ambaye binafsi aliandika barua rasmi kwa uongozi wa TEF akilaani kupigwa kwa waandishi wa habari na kutoa pole kwa wale waliomizwa na kupata mshtuko" Walisema viongozi wa TEF

Taarifa hiyo ya TEF ilikwenda mbali zaidi na kuwatahadharisha waandishi wa habari, wahariri kuwa wanapaswa kuwa makini pindi wanapokuwa wanaitwa na kundi hili la Lipumba kwa ajili ya kutoa habari zao 


A

MWANDISHI WA GAZETI LA GAURDIAN ASIMULIA JINSI ALIVYOTAKA KUULIWA NA 'MUNGIKI' WA LIPUMBA,SOMA HAPO KUJUA

Mwandishi wa Gazeti la The Gaurdian Henrry Mwang'onde asimulia jinsi alivyonusurika kupoteza maisha alipokuwa akijinusuru kutoka kwenye kipigo cha wavamizi wa Mkutano wa CUF na waandishi wa Habari.

Uvamizi huo ulifanywa na wafausi wa Chama cha wananchi CUF wanaomuunga Mkono Mwenyekiti anayetambulika na Msajili wa Vyama vya siasa nchi Professa Ibrahimu Lipumba

Henrry ameeleza jinsi alivyokimbia kutoka kwenye chuma hicho cha mkutano na kwenda nje ya chumba hicho kilichopo Ghorofa ya Nne na kutaka kujiokoa kwa kushuka chini kupitia kolido la Ghorofa hilo ili adondokee floo inayofuata.

Hennry amesema kuwa aliishiwa nguvu na kwamba manisura yake ni waandishi wenzake walikuwepo karibu ambao  nao walikuwa wanata kuokoa uhai wao.

Amesema kuwa hakuwa sawa kisaikolojia .

SAKATA LA MITUNGI YA GESI YA TANZANIA KUPIGWA 'STOP' NCHINI KENYA,MBUNGE ZITTO KABWE ASHUKIA SERIKALI,SOMA HAPO KUJUA

Wizara ya Nishati ya Kenya imepiga marufuku gesi ya kupikia kutoka Tanzania kuingia nchini humo. Tamko la Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati ya Kenya linasema ‘ ndani ya siku 7 kuanzia juzi tarehe 24 Aprili 2017, itakuwa ni marufuku Kwa Kenya kuagiza Gesi ya kupikia kutoka Tanzania ‘.

Uamuzi huu wa Kenya ni kinyume na misingi ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ambapo Tanzania na Kenya ni wanachama. Kwa mujibu wa Itifaki ya Soko la Pamoja, bidhaa za nchi zetu zinaruhusiwa kusambaa ndani ya jumuiya bila vikwazo.

Gesi ya kupikia kuingia Kenya hutokea Tanzania Kwa sababu Tanzania ni nchi pekee katika ukanda huu ambayo imewekeza mitambo ya kupokea Gesi na kuiweka kwenye mitungi. Bandari ya Dar Es salaam na mfumo mzuri zaidi wa kupokea gesi kuliko Bandari ya Mombasa na hivyo kuifanya gesi inayotoka Tanzania kuwa na gharama nafuu nchini Kenya kuliko gesi inayoagizwa kupitia bandari ya mombasa.

Uamuzi wa kuzuia Gesi kutoka Tanzania ni uamuzi wenye kulenga kuilinda bandari ya Mombasa Kwa kuvunja mkataba wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na Kwa kutaka kuifanya Tanzania iendelee kuwa muuzaji wa malighafi kwenda Kenya badala ya bidhaa zilizokamili Kama gesi ya kupikia.

Uamuzi huu wa Serikali ya Kenya una lengo la kuathiri urari wa biashara kati ya Tanzania na Kenya ambapo Kwa miaka ya hivi karibuni Tanzania imekuwa ikiuza bidhaa nyingi zaidi huko Kenya kuliko inazoagiza kutoka nchi hiyo.

Ninamsihi Waziri wa Biashara na Viwanda wa Tanzania afuatilie suala hili na kuzungumza na mwenzake wa Kenya ili waondoe vikwazo Hivi vya biashara ambavyo havina maana yeyote na vinazuia raia wa kenya kupata bidhaa nafuu kutoka Tanzania. 

Viwanda vingi vya Kenya hutegemea malighafi kutoka Tanzania, kuzuia gesi ya kupikia na kuendelea kuagiza malighafi za kuendesha viwanda vyao ni sera ya Kenya kuifanya Tanzania kuwa chanzo cha malighafi tu na sio chanzo cha bidhaa zilizoongezwa thamani.

Serikali ya Tanzania isikubali hili na ianze mazungumzo mara moja na Serikali ya Kenya ili Watanzania wanaouza gesi ya kupikia huko Kenya waendelee kuuza na kutumia Bandari ya Dar Es Salaam. 

Kama Serikali ya Kenya ikiendelea na msimamo wake basi Tanzania ichukue msimamo kama huo Kwa bidhaa za Kenya Kama maziwa ambayo yamejaa kwenye soko letu.

Zitto Kabwe, Mb
Kigoma mjini
26/4/2017

RAIS MAGUFULI ATOA MIKWARA MIZITO ,NI KWA WALE WASIOPENDA MUUNGANO,SOMA HAPO KUJUA

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, leo tarehe 26 April 2017, ameongoza maelfu ya Watanzania katika sherehe za miaka 53 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar zilizofanyika katika Uwanja wa Jamhuri Mjini Dodoma.

Akizungumza mara baada ya kukagua gwaride la vikosi vya ulinzi na Usalama lililoandaliwa kwa heshma yake, Rais Magufuli amewahakikishia watanzania kuwa yeye na Rais wa Zanzibara Dkt. Ali Mohamed Shein wataendelea kuulinda Muungano kwa nguvu zao zote na kwamba atakayejaribu kuuvunja atavunjika yeye.

''Muungano ndio silaha yetu. Ni nguvu yetu. Mimi na mwenzangu Dkt. Shein tutaulinda Muungano  kwa nguvu zote. Yeyote atakayejaribu kuuvunja atavunjika yeye'' amesema Rais Magufuli.

Aidha Dkt. Magufuli amewataka watanzania kuendelea kudumisha amani iliyopo nchini kwani amani ndio chachu ya maendeleo yanayopatikana nchini.

Rais Magufuli amesema Tanzania imeweza kufikisha miaka 53 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar kwa sababu ya amani iliyopo nchini iliyowezesha kupatikana mafanikio makubwa ikiwa ni pamoja na kuunganisha mataifa yetu mawili na kuuunda taifa moja lenye nguvu.

Aidha amesema Muungano wa Tanganyika na Zanzibar umewezesha kupatikana mafanikio makubwa katika nyanja za kiuchumi, kisiasa na kijamii.

Mhe. Rais ametaja mafanikio mengine yaliyopatikana kutokana na Muungano ni kukua kwa uchumi na kukabiliana na matatizo ya umasikini na ukosefu wa ajira,kuimarisha miundombinu ya usafiri wa anga, majini,reli  na nchi kavu.

Aidha Muungano umeimarisha na kuboresha upatikanaji wa huduma za jamii ikiwa ni pamoja na kuongezeka kwa idadi ya shule na hospitali pamoja na kukua kwa demokrasia nchini.

Kwa mara ya kwanaza katika historia ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar Maadhimisho ya Sherehe za Muungano zinafanyika mkoani Dodoma makao makuu ya Serikali ikiwa ni ishara tosha kuwa Serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na chama cha Mapinduzi imedhamiria kwa dhati kuhakikisha makao makuuu ya Serikali yanakuwa Dodoma.

''Niwahahakikishie wana Dodoma na Watanzania kwa ujumla  kwamba Serikali sasa tumefika Dodoma na hatutarudi tena, na  kama tulivyoahidi mwaka 2020 Serikali yote itakuwa imehamia hapa'' amesema Rais magufuli.

Sherehe za miaka 53 ya Muungano zimehudhuriwa na viongozi mbalimbali ikiwa ni pamoja na wajane wa viongozi waasisi wa Muungano mke wa hayati Mwalimu Julius Nyere Mama Maria Nyerere na hayati Abeid Aman Karume, Mama Shadya Karume,Makamu wa Rais Mama Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, na viongozi wa chama na serikali.

Kauli mbiu ya Sherehe za Muungano mwaka huu ni ''Miaka 53 ya muungano,Tuuulinde na kuuimarisha, Tupige vita Dawa za Kulevya na Kufanya Kazi kwa Bidii''

Jaffar Haniu
Naibu Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dodoma
26 Aprili, 2017

MBUNGE MDEE ATUMIA HEKIMA YAKE KUMALIZA TOFAUTI YAKE NA SPIKA NDUGAI,SOMA HAPO KUJUA


Mbunge wa jimbo la Kawe kwa tiketi ya CHADEMA Mhe. Halima Mdee jana amefunguka na kuomba radhi bungeni kufuatia kutoa lugha isiyokuwa na staha bungeni wakati wa uchaguzi wa Wabunge wa Bunge la Afrika Mashariki uliofanyika April 4, 2017.

Halima Mdee wakati akiomba radhi hiyo anasema kuwa siku hiyo ya uchaguzi kulikuwa na matukio ambayo yalikuwa yakiendelea bungeni ambayo yalimpelekea kutoa lugha isiyokuwa sawa kitamaduni za bunge, ambayo ilimgusa Spika wa Bunge na Naibu waziri wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. Khamis Kigwangala

"Mhe. Mwenyekiti tarehe 4 mwezi wa 4 wakati wa uchaguzi wa EALA kuna matukio ambayo yalikuwa yanaendelea yakanipelekea kuzungumza lugha ambayo kitamaduni za Bunge si sawa na lugha husika ilimgusa Spika wa bunge na Mhe, Kigwangala kwa namna moja au nyingine

"Kama mbunge mzoefu nilitumia jitihada binafsi kuzungumza na kuomba radhi wahusika katika 'individual capacity'lakini vilevile nikaona ni busara kwa sababu haya maneno niliyasema bungeni hivyo kuzungumza pia hapa na kumuomba radhi Mhe. Spika kwa hiyo niliomba huu muda kwa lengo la kumuomba radhi, kumwambia namuheshimu na kumwambia sitarudia" alisema Halima Mdee

Mbali na hilo Halima Mdee aliendelea kuomba radhi kwa wabunge, watanzania pamoja na wananchi wa jimbo la Kawe lakini pia Halima Mdee alisisitiza kuwa michango yake ya bunge itaendelea kama kawaida yake lakini kwa kutumia lugha za staa

RAIS MAGUFULI AWAACHIA HURU WAFUNGWA HAWA,SOMA HAPO KUJUA

Katika kuadhimisha Miaka 53 ya Muungano wa Tanzania tarehe 26 Aprili, 2017 Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kutumia madaraka aliyopewa chini ya Ibara ya 45(1)(d) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ametoa msamaha kwa wafungwa wafuatao:-

Wafungwa wote ambao baada ya punguzo la kawaida la moja ya tatu (1/3) linalotolewa chini ya Kifungu 49(1) cha Sheria ya Magereza Sura ya 58, wawe wametumikia nusu (½) ya vifungo vyao vilivyobaki, isipokuwa wafungwa walioorodheshwa katika Ibara ya 2(i – xxi).

Wafungwa wagonjwa wenye magonjwa kama UKIMWI, Kifua kikuu (TB) na Saratani (Cancer) ambao wako kwenye “terminal stage”. Wafungwa hawa wathibitishwe na Jopo la Waganga chini ya Uenyekiti wa Mganga Mkuu wa Mkoa/Mganga Mkuu wa Wilaya.

Wafungwa wazee wenye umri wa miaka sabini (70) au zaidi. Umri huo uthibitishwe na Jopo la Waganga chini ya Uenyekiti wa Mganga Mkuu wa Mkoa/Mganga Mkuu wa Wilaya.

Wafungwa wa kike walioingia na mimba gerezani, pamoja na wale walioingia na watoto wanaonyonya na wasionyonya.

Wafungwa wenye ulemavu wa mwili na akili (Physical disability and mental disability). Ulemavu huo uthibitishwe na Jopo la Waganga chini ya Uenyekiti wa Mganga Mkuu wa Mkoa/Mganga Mkuu wa Wilaya.

Aidha, Msamaha huu wa Mheshimiwa Rais hautawahusu wafungwa wafuatao:-

Wafungwa waliohukumiwa adhabu ya kunyongwa.
Wafungwa waliohukumiwa adhabu ya kunyongwa na adhabu hiyo kubadilishwa kuwa kifungo cha maisha au kifungo gerezani.

Wafungwa waliohukumiwa kifungo cha maisha gerezani.

Wafungwa wanaotumikia kifungo kwa makosa ya kujihusisha na usafirishaji na matumizi ya madawa ya kulevya kama vile cocaine, heroin, bhangi.

Wafungwa wanaotumikia kifungo kwa makosa ya kujihusisha na uombaji na upokeaji au utoaji rushwa.

Wafungwa wanaotumikia kifungo kwa makosa ya unyang’anyi na unyang’anyi wa kutumia silaha au kujaribu kutenda makosa hayo (robbery with violence, armed robbery and attempt robbery).

Wafungwa wanaotumikia kifungo kwa makosa ya kupatikana na silaha, risasi au milipuko isivyo halali (fire arms, ammunitions and explosives).

Wafungwa wanaotumikia kifungo kwa makosa ya shambulio la aibu, kunajisi, kubaka na kulawiti au kujaribu kutenda makosa hayo.

Wafungwa waliopatikana na hatia na kuhukumiwa kifungo kwa kosa la kuwapa mimba wanafunzi wa Shule za Msingi na Shule za Sekondari na ambao walitenda kosa hilo wakiwa na umri wa miaka kumi na nane (18) na kuendelea.

Wafungwa wanaotumikia kifungo kwa makosa ya wizi wa magari na pikipiki, uharibifu wa miundombinu au kujaribu kutenda makosa hayo.

Wafungwa wanaotumikia kifungo chini ya Sheria ya Bodi ya Parole (Act. No. 25/1994) na Sheria ya Huduma kwa Jamii (Act. No. 6/2002).

Wafungwa waliopatikana na hatia na kuhukumiwa kifungo kwa makosa ya kutumia vibaya madaraka yao.

Wafungwa waliowahi kupunguziwa kifungo na Msamaha wa Mhe. Rais na bado wangali wanaendelea kutumikia sehemu ya kifungo kilichobaki.

Wafungwa waliopatikana na hatia na kuhukumiwa kwa kosa la kuzuia watoto kupata masomo.

Wafungwa waliopatikana na hatia na kuhukumiwa kwa kosa la utekaji wa watoto, kupoka na kufanya biashara ya binadamu (Human Trafficking).

Wafungwa waliopatikana na hatia na kuhukumiwa kwa kosa la kukutwa na viungo vya binadamu.

Wafungwa wanaotumikia vifungo kwa makosa ya kujihusisha kwa namna yoyote ile na nyara za Serikali na ujangili (poachers).

Wafungwa wanaotumikia vifungo kwa makosa ya wizi/ubadhirifu wa fedha za Serikali.

Wafungwa wanaotumikia vifungo kwa makosa ya kutoroka au kujaribu kutoroka chini ya ulinzi halali.

Wafungwa walioingia gerezani baada ya tarehe 16/03/2017.

Wafungwa warejeaji wa makosa/wafungwa waliowahi kufungwa gerezani (Recidivists).

Wafungwa 2,219 watafaidika na msamaha huu na wataachiliwa huru. Ni mategemeo ya Serikali kwamba watarejea tena katika jamii kushirikiana na wenzao katika ujenzi wa Taifa na kwamba watajiepusha kutenda makosa ili wasirejee tena gerezani.

Meja Jenerali Projest Rwegasira
KATIBU MKUU
WIZARA YA MAMBO YA NDANI YA NCHI

26/04/2017

KIKWETE ASEMA BADO KUNA SHIDA KWENYE ELIMU,SOMA HAPO KUJUA

Suala la elimu kwa wote bado ni changamoto kubwa hususani kwa nchi masikini na za kipato cha wastani, amesema Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais mstaafu wa Tanzania na mjumbe wa Kamisheni ya kimataifa kuhusu ufadhili wa fursa za elimu duniani.

Kikwete ambaye alikuwepo Washington D.C kwenye mkutano wa ufadhili wa elimu wa mkakati mpya uliozinduliwa mwaka jana kwa nchi za Afrika "The Pioneer country Initiative" baada ya kuzuru nchi 14 zilizo katika mradi huo wa awali.

Dkt. Kikwete amesema alichobaini kuna matatizo makubwa matatu kwenye nchi masikini na nchi za uchumi wa kati ambapo vijana wengi wanaostahili kuwepo mashuleni hawapo mashuleni, lakini la pili ni kwamba wanafunzi waliopo mashuleni wengi wao hawamalizi masomo yao na jambo la tatu watu wanaomaliza masomo yao hawapati elimu wanayostahili kuipata.

Mbali na hilo Dkt Kikwete ameongeza kuwa tume imependekeza nchi husika zinapaswa kufanya mageuzi katika mifumo yao ya elimu ili kuweza kupata matokeo chanya katika sekta hiyo ya Elimu katika nchini zinazoendelea.

Nchi hizo ni pamoja na Botswana, Chad, Congo Brazzaville, Cote d'voire, Ethiopia, Gabon, Ghana, Malawi, Msumbiji, Namibia, Nigeria, Tanzania, Tunisia na Uganda.

CUF YA LIPUMBA YAKIRI,MLINZI ALIKONG'OLEWA KISIGINO NI MTU WAO,SOMA HAPO KUJUA

Upande wa Chama cha wananchi CUF wanaosapoti Mwenyekiti anayetambulika na Msajili wa Vyama vya siasa Nchini  Profesa Ibrahim Lipumba  umekiri kuhusika kwa tukio la vina Hotel.

Akizungmza na waandishi wa habari mapema leo hii Mkurugenzi wa Habari na Mawasiliono wa chama hicho Abdul Kambaya amefafanua uwepo wa walinzi wa chama Vina hotel ambapo ni kwa mujibu wa katiba ya Chama chao walinzi wa chama hicho hufanya doria kwa ajili ya viongozi na mali za chama hicho kwahivo ilikuwa halali wao kuwepo katika eneo hilo

Hata hivyo ameomba radhi kwa waandishi wa habari na kwamba kitendo kile cha wale walinzi kuitiwa kelele za wezi zilisababisha vurugu kwenye ukumbi huo

SAKATA LA KUFUKUZWA BOSI WA UN,WABUNGE WAIKOMALIA SERIKALI,SOMA HAPO KUJUA

Dodoma. Sakata la kufukuzwa nchini la bosi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) Tanzania, Awa Dabo, limetua bungeni.

Mbunge wa Mbozi, Pascal Haonga(Chadema) akizungumza bungeni leo,  aliitaka serikali kufafanua sababu za kumfukuza nchini Mkurugenzi Mkazi huyo wa UNDP Tanzania kwa kumpa saa 24.

Hata hivyo, Mwenyekiti wa Bunge, Andrew Chenge aliliambia bunge kuwa serikali ina mamlaka yote katika masuala ya kidiplomasia na hivyo bunge haliwezi kuhoji  sababu za mkurugenzi huyo kufukuzwa.

SAKATA LA KUFUKUZWA BOSI WA UN NCHINI,SERIKALI YAIBUKA NA KUTOA NENO,SOMA HAPO KUJUA


TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Serikali yamuondoa Mkurugenzi wa UNDP nchini 
 
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeliagiza Shirika la Umoja wa Mataifa la Programu ya Maendeleo (United Nations Development Programs – UNDP) kwa upande wa Tanzania kumuondoa nchini Mkurugenzi wa Shirika hilo Bi Awa Dabo.
 
Serikali ilifikia uamuzi huo kutokana na  Bi Dabo kutokuwa na maelewano mazuri na baadhi ya Watumishi wenzake na Menejimenti ya Shirika hilo, hivyo kupelekea kuzoretesha utendaji wa shirika hilo nchini na kupunguza kasi ya kuleta maendeleo kwa Watanzania endapo hatua za haraka zisingechukuliwa.
 
Baada ya kuthibitishiwa kuondoka nchini, Serikali kupitia Wizara ya Mambo ya Nje imetoa rai kwa UNDP kuwakumbusha Watumishi wake kuwa kipaumbele chao ni kufanya kazi na Serikali ili kufikia malengo yaliyoainishwa kwenye Dira ya Maendeleo ya Mwaka 2025, Mpango wa Maendeleo wa Miaka mitano na Malengo ya Maendeleo Endelevu ambayo yamefafanuliwa katika Agenda ya Mwaka 2030. 

Mwisho.
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasili ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Dodoma, 25 Aprili 2017.

CCM WAMCHOKA NAPE ,WAJIPANGA KUMSHITAKI,SOMA HAPO KUJUA


Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Humphrey Polepole amelaani vikali kauli iliyotolewa na mtangulizi wake ambaye ni mbunge wa jimbo la Mtama, Nape Nnauye kuwa alisaidia kukitoa chama hicho shimoni.

Nape alitoa kauli hiyo dakika chache baada ya mkutano wake na waandishi wa habari kuzuiwa na kutishiwa bastola na mtu mmoja, siku moja baada ya kuondolewa kwenye nafasi ya Uwaziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo.

Polepole alisema kuwa kauli hiyo ya Nape sio kauli sahihi ya kiongozi na kwamba yeye pekee hawezi kukitoa chama shimoni huku kukiwa na wanachama milioni nane na maelfu ya viongozi.

“Mwanachama anayejitambua hawezi kusema anakibeba chama, wanachama wote milioni nane walikuwa wapi? Viongozi wote maelfu walikuwa wapi? Nape ni kiongozi wetu kwenye chama, kama kweli alisema maneno hayo alikengeuka sana,” Polepole anakaririwa na Mwananchi.

Katibu huyo wa Itikadi na Uenezi wa CCM alisema kuwa Kamati ya Maadili inapaswa kuliangalia suala hili na kumchukulia hatua Nape.

“Tuna kila sababu za kumshauri Mzee Mangula wa Kamati ya maadili kuwa hatuwezi kuwa na viongozi wa aina hii. Chama chenye watu milioni nane unakitoa shimoni na nini? Unakitoa na ngazi, ulitumia kamba kukitupia shimoni, uliita zimamoto? "Alihoji.

Hata hivyo, Polepole alisema kuwa hatua zinazopaswa kuchukuliwa kwa viongozi kama Nape sio za kuwawekea ukomo bali kuwalea kimaadili kwa kutumia hekima na busara ili watambue kuwa chama sio punda anayeweza kutumbukia shimoni. 

Hivyo, alisema CCM iko kwenye mpango wa kuanzisha chuo kikuu kitakachotoa mafunzo kwa makada wake kuhusu nidhamu na maadili.

SERIKALI YAKUBALI OMBI LA ASKOFU GWAJIMA KUNUNUA TRENI YA UMEME,SOMA HAPO KUJUA

Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima amekaribishwa kuwa anaweza kuendesha huduma ya usafiri wa treni na kutaka wadau wengine wenye nia kama hiyo wajitokeze.

Katika ibada iliyofanyika juzi, Askofu Gwajima aliwaambia waumini wake kuwa amedhamiria kununua treni ya umeme itakayogharimu Sh11 bilioni, baada ya Rais John Magufuli kuzindua mradi wa ujenzi wa reli pana (standard gauge) itakayokuwa na kasi zaidi ya treni ya sasa na uwezo wa kuchukua shehena kubwa.

Ujenzi wa reli uliozinduliwa na Rais Magufuli Aprili 12, utakamilika ndani ya miezi 30 na awamu ya kwanza itaanzia Dar es Salaam hadi Morogoro, treni yake itakuwa na kasi ya kilomita 160 kwa saa, ikibeba mabehewa 100.

Msemaji wa Kampuni Hodhi ya Rasilimali za Reli (Rahco), Catherine  Moshi alisema kampuni hiyo  imebariki uamuzi huo wa kuwekeza katika usafiri wa reli, lakini askofu huyo anatakiwa kuomba kibali  Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.

“Tunamkaribisha mchungaji, hii ni biashara kwetu na huyu ni mwekezaji tena wa ndani. Hatuwezi kumuangusha cha muhimu ni kufuata utaratibu tu,’’ alisema Catherine.

JESHI LA POLISI YAKIRI KUWAKAMATA 'MUNGIKI' WA LIPUMBA,SOMA HAPO KUJUA


Na Karama Kenyunko, Blogu ya jamii. 
Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam linawashikilia watu watano kwa tuhuma za kushiriki tukio la uvamizi wa Mkutano wa wanachama wa CUF uliofanyika Vinna Hotel Mabibo, jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki. 

Kamanda wa Polisi Kanda maalumu ya Dar es Salaam Simon Sirro amesema hayo leo wakati akiongea na waandishi wa Habari jijini hapa. Amesema kuwa. Aprili 22 mwaka huu majira ya mchana, walipokea taarifa ya kuwa watu wasiofahamika wakiwa na silaha walivamia mkutano huo na kujeruhi baadhi ya watu. 

Kamanda Sirro ameongeza kuwa, mpaka sasa watuhumiwa watatu waliokamatwa wanaendelea kuhojiwa na upelelezi utakapokamilika hatua za kisheria zitafuatwa juu yao na amewasihi watu kutii sheria bila shuruti kwani hakuna mtu au kikundi chochote cha watu wanaoweza kuwa na mamlaka ya kushambulia wengine. 

"Kama unamalalamiko pitia polisi, au mahakamani siyo kuvamia kundi la watu wengine kama wako juu ya sheria, tunafuatilia wale wote waliohusika katika kufanya shambulio hilo na mtu mmoja aliyejeruhiwa sana anataja watu walioshambulia" amesema Sirro. 

Kamanda Sirro, amesema jeshi la polisi linaamini kuwa watu waliofanya uvamizi huo walifanya kwa utashi wao wenyewe na kwamba pindi upelelezi ukikamilika watachukuliwa hatua za kisheria ikiwemo kupelekwa mahakamani. 


Aidha amewaonya baadhi ya viongozi wa CUF waliotangaza kuwafuata watu fulani na kuwawajibisha ni vema wakumbuke kuwa hakuna mtu aliyeko juu ya sheria kwani hakuna mtu aliyeko juu ya mamlaka. 

Mapema wiki iliyopita, watu wasiojulikana wakiwa na bastola walivamia mkutano wa wanachama wa CUF ambao wanamuunga mkono, Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Shariff Hamad na kuwapiga wanachama wa CUF pamoja na waandishi wa habari ambao walikuwepo eneo hilo. 

Mkutano huo ambao ulikuwa na lengo la kumtambulisha Katibu Mkuu wa CUF , ulivurugika baada ya vurugu kubwa zinazodaiwa kufanywa na wanachama wa CUf ambao wanamuunga mkono Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba. 

katika vurugu hizo, Mtu mmoja ambaye bado hajafahamika jina lake miongoni mwa waliovamia mkutano wa wanachama wa CUF ameshambuliwa na wananchi wakati akijaribu kutoro

CUF YA MAALIM SEIF YATOA NENO JIONI HII KUHUSU RAFU YA POLISI ,SOMA HAPO KUJUA

Kutoka kwenye ukurasa wa Facebook wa Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi ya Muda wa CUF bwana Julius Mtatiro

"Mwanasheria Mkuu wa chama chetu, Wakili Msomi HASHIM MZIRAY yuko katika kituo cha Polisi Magomeni ambako amemsindikiza Mwenyekiti wetu wa Wilaya ya Kinondoni, Mhe. Juma Mkumbi.

Mhe. Juma Mkumbi ndiye aliyevamiwa na Mungiki wa Lipumba, akiwa anaongoza Mkutano na vyombo vya habari pale Vina Hotel. Polisi walipofika wakamshauri arejee nyumbani akapumzike (ana diabetes) kisha wakamshauri akaripoti kituoni jana kwa ajili ya ku LODGE malalamiko yake rasmi ili yaunganishwe na malalamiko ya waandishi wa habari na viongozi waandamizi waliovamiwa juzi.

Jana mhe. Mkumbi alishindwa kwenda kufungua kesi kwani hali yake ya afya haikuwa nzuri na leo ndipo alipanga kwenda. Ikumbukwe pia simu za jana za OCD na OCCID za kutaka kuwapatanisha na wale wavamizi.

MAAJABU YA DUNIA...
Leo amekwenda Magomeni Polisi ili kuripoti tukio zima lilivyokuwa (kwani Juzi Polisi walichukua maelezo ya wanahabari na viongozi waandamizi tu wale waliokuwa wamepigwa, kuumizwa au kujeruhiwa).

Mkumbi amefika Magomeni Polisi ili kufungua mashtaka yake kama muathiriwa lakini OCD na OCCID wa Magomeni wameelekeza ahojiwe kama Mtuhumiwa. Hivi tuzungumzavyo Juma Mkumbi ndiye anahojiwa kwa tuhuma za kumjeruhi yule MUNGIKI aliyekatwa mguuni na Wananchi (Mlinzi wa Lipumba).

MAELEKEZO WALIYOPEWA POLISI..
Niliwaeleza hapa, kwamba Polisi wameelekezwa wahakikishe aidha upande ULIOVAMIWA (Chama) unakubali kukaa meza moja na wale WALIOVAMIA (Lipumba na Mungiki) AU Upande wa chama ndiyo unapewa kesi ya kujeruhi lile jambazi lililojeruhiwa na wananchi.

HURUMA INAPONZA
Wananchi wenye hasira walipokuwa wanaliadhibu "ZOMBI" lile, liliokolewa na viongozi wale wale walioshuka haraka chini na kuomba waitwe polisi. Yaani, kama si juhudi za kina Juma Mkumbi na wenzao, zombi la Lipumba lingeliuawa. Huruma yao kuingilia kati na kulikokoa na wakaita polisi likakamatwa, ndiko kumewaponza. Polisi wanatufundisha kuwa the next person wa Lipumba ambaye atatuvamia basi viobgozi waache auawe maana wakimsaidia wao wanageuziwa kibao. Sawa tumeelewa somo!

BASTOLA
Hadi sasa, polisi hawaelezi lile ZOMBI lililokuwa na Bastola liko wapi na hawasemi ile bastola iko wapi pia. Kwa kifupi Polisi hawataki kuzungumzia masuala ya Bastola ile. Badala ya kushughulikia mambo makubwa, sasa wana-deal na upande wetu.

WITO
Natoa wito kwa wanachama wa CUF kukaa STANDBY, tunataka kuona Zombi/Mungiki lililokamatwa na wananchi linafikishwa mahakamani.

Tunataka kuona wale wote waliokuwa na Zombi hilo wanakamatwa pia na kufikishwa mahakamani. Wanafahamika kwa majina, kwa sura na kwa makazi.

Tunataka kuona ile BASTOLA inasakwa na aliyekuwa nayo anapatikana. Uzuri aliyekuwa na bastola alipanda kwenye yale magari mawili yaliyotumika kwenye uvamizi.

Tunataka kuona magari yaliyotumika kwenye uvamizi ule yakikamatwa NA madereva wa magari yale (wanafahamika) wanakamatwa haraka.

Tunataka kuona mkuu wa wavamizi wale anakamatwa haraka na jana alionekana AZAM TV akitamba kuwa mazombi yake yataendelea na oparesheni ya kuvamia na kupiga watu, (na polisi wana clips zote).

Kwa sababu leo tumekutana na Kamishna Sirro tunajipa muda kuona hatua zipi zitachukuliwa. Kama hatua hazichukuliwi na Polisi, basi, sisi tutawaambia wanachama wetu WASIFE KIKONDOO huko mitaani, tutawaomba wajilinde kwa nguvu zote kwani hiyo ni haki yao ya kikatiba. Kile kijikundi cha MUNGIKI na LIPUMBA kina watu wachache sana, lakini UJINGA wetu ni kuendelea kuheshimu sheria za nchi.

Mtatiro J,

WABUNGE WA UPINZANI WAIGOMA KUISOMA BAJETI YA HII LEO,SOMA HAPO KUJUA


Msemaji wa upinzani katika Ofisi ya Makamu wa Rais, Mazingira na Muungano, Ally Salehe amesusa kusoma hotuba yake ya upinzani kuhusu wizara hiyo baada ya kulazimishwa kuacha kusoma baadhi ya maneno yakiwamo yanayohusu Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar na mgogoro wa CUF.

Hali  hiyo imetokea bungeni leo Jumatatu baada ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali(AG), George Masaju kusimama na kupinga baadhi ya maneneo aliyotumia kama “Kila wizara imekiona cha moto, wamebanwa mpaka wamevunjwa mbavu” na kuwa Ofisi ya Makamu wa Rais imeathirika vibaya na kisu cha ngariba kwa kukata bajeti yake.

Baada ya malumbano, Mwenyekiti wa Bunge, Musa Zungu alitoa uamuzi kuwa maneno yaliyoandikwa kuanzia ukurasa wa tatu hadi wa saba kwenye hotuba hiyo yasisomwe wala kurekodiwa kwenye kumbukumbu rasmi za Bunge.

Baada ya uamuzi huo, Salehe alisema basi asingeendea kuisoma hotuba yake na yaliyobaki anamwachia ngariba afanye anavyotaka

'MUNGIKI WA PROF LIPUMBA';WALANIWA KILA KONA,MSAJILI WA VYAMA VYA SIASA NA IDARA YA HABARI MAELEZO VYATOA TAMKO KALI,SOMA HAPO KUJUA


SIKU chache kupita baada ya watu wanaotajwa kutumwa na Mwenyekiti wa  Chama cha Wananchi (CUF) ambaye anatambuliwa na Ofisi ya Msaji wa Vyama vya Siasa nchini ,Profesa Ibrahimu Lipumba kuvamia mkutano wa Mwenyekiti wa Chama hicho wilaya ya Kinondoni na kupelekea kuwajuluhi waandishi wa habari na viongozi kadhaa wa CUF ambao wanaumuunga mkono Katibu Mkuu wa Chama hicho,Maalim Seif,

Hatimaye Sakata Hilo Limeibua Msajili wa vyama vya siasa nchini,Jaj Francis Mtungi na Kulaani tukio hilo huku akiwataka wanachama na viongozi wa Chama hicho wangojee hatma ya Mahakama ndio itakayomaliza mgogoro huo,

 TAMKO LA MSAJILI HILI HAPA 

Nimesoma na kuona katika vyombo mbalimbali vya habari kuhusu vurugu zilizotokea tarehe 22 Aprili, 2017 katika hoteli ya Vina, Mabibo hapa Dar es salaam, zinazosemekana kuhusisha wanachama wa CUF.

Ni ukweli usiopingika kuwa, suala la mgogoro wa uongozi katika chama cha CUF lipo mahakamani, lakini nikiwa msimamizi wa Sheria ya Vyama vya Siasa na kutambuliwa na jamii kuwa ni mlezi wa vyama vya siasa; nimelazimika kuwasihi wadau wa siasa hususani wanachama wa chama cha CUF, kutambua kwamba, kuwapo kwa shauri mahakamani siyo fursa ya kufanya vitendo vya uvunjifu wa amani, kwani jambo hili ni uvunjifu wa sheria na linaleta sura mbaya kwa jamii.

Hivyo, ninalaani vurugu hizo, ambazo zilionekana kuvunja amani na utulivu na watu kuumizwa, tofauti na tunu zetu za taifa za amani na utulivu. Pia, nawaasa wanachama wa CUF pamoja na tofauti walizonazo, madhali masuala haya yapo mahakamani hebu tuheshimu utawala wa Sheria.

Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa na hata Jeshi la Polisi lipo kushughulikia malalamiko yoyote yanayohusu uendeshaji na shughuli za chama chochote cha siasa. Hivyo, hakuna haja ya wanachama wa chama cha CUF kukiuka taratibu za kuendesha chama hicho au kujichukulia Sheria mkononi.

Aidha, ninaviasa vyama vya siasa kuelewa kuwa havipo juu ya Sheria, vinapaswa kuheshimu na kufuata Sheria za nchi, ikiwamo kutunza amani na utulivu tulionao.

Mwisho, ninaomba vyombo vya ulinzi na usalama katika nchi yetu kulifanyia kazi tukio hilo, ili wahusika wafahamike na kuchukuliwa hatua za kisheria. Kwa upande wa Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa inayosimamia utekelezaji wa Sheria ya Vyama vya Siasa, haitasita kuchukua hatua stahiki kwa mujibu wa Sheria.

Jaji Francis S.K. Mutungi                            
MSAJILI WA VYAMA VYA SIASA
24 Aprili, 2017
IDARA YA HABARI YATOA TAMKO KIPINGA HATUA YA KUVAMIWA WAANDISHI WA HABARI
Serikali imepokea kwa masikitiko taarifa za kushambuliwa na kujeruhiwa baadhi ya waandishi wa habari katika mvutano uliotokea juzi jijini Dar es Salaam kati ya wafuasi wa pande mbili zinazokinzana za Chama cha Wananchi (CUF). Tumechukua muda kidogo kulifuatilia suala hili na kubaini licha ya baadhi yao kujeruhiwa na kuripoti polisi, wapo waandishi ambao vifaa vyao vya kazi pia vililengwa katika shambulizi hilo.

Tunachukua fursa hii kulaani kitendo cha kuumizwa wanahabari tena waliokuwa wamealikwa kuhudhuria mkutano huo. Ifahamike kuwa uandishi wa habari ni taaluma adhimu na nadhifu inayopaswa kuheshimiwa, kuenziwa, kulindwa na kutoingizwa katika migogoro ya pande zinazofarakana katika jamii.

Kifungu cha 7 (1) (a) cha Sheria ya Huduma za Habari Na. 12 ya mwaka 2016 kinaainisha uhuru wa wanahabari katika kukusanya habari kwa muktadha wa kuwepo katika maeneo ya matukio kama hakuna sababu nyingine za kuzuiwa. Misingi ya uhuru huu wa kitaaluma pia imesisitizwa katika Ibara za 18 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 1977 na 19 ya Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Kiraia na Kisiasa wa mwaka 1966 ambao nchi yetu imeuridhia.

Tunawatakia nafuu ya haraka wanahabari waliojeruhiwa na wenzao wengine waliopatwa na jakamoyo katika tukio hilo. Kwa kuwa suala hili tayari limeripotiwa polisi, tunawaomba wadau wote wa habari na wanasiasa kwa sasa kutulia na kuviachia vyombo husika vilifanyie kazi ili hatua stahiki za kisheria zichukuliwe.

Imetolewa na:
Dkt. Hassan Abbasi
Mkurugenzi, Idara ya Habari-MAELEZO na Msemaji Mkuu wa Serikali