Katibu Mkuu wa Chama cha ACT Wazalendo Ado Shaibu akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.

NA MWANDISHI WETU

CHAMA cha ACT Wazalendo kumejitoa kwenye Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar kutokana na kutotekelezwa kwa makubaliano yaliyoingiwa na Marehemu Maalim Seif Sharif Hamad kwa niaba ya Chama hicho na Rais Dkt. Hussein Mwinyi kabla ya ACT Wazalendo kujiunga na Serikali hiyo.

Hayo yamebainishwa leo Machi 8, 2024 na Katibu Mkuu wa ACT Wazalendo Ado Shaibu akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kueleza maazimio ya Kikao cha Halmashauri Kuu ya Chama kilichofanyika Machi 7 mwaka huu katika Ukumbi wa Hakainde Hichilema uliopo katika Jengo la Maalim Seif (Makao Makuu ya Chama) Dar es Salaam.

"Halmshauri Kuu ya Chama Taifa kwenye kikao chake cha tarehe 7 Machi, 2024 ilitoa agizo kwa Kamati ya Uongozi Taifa kuonana na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Rais wa Zanzibar kuwaeleza juu ya uamuzi wa ACT Wazalendo kujitoa kwenye Serikali ya Umoja wa Kitaifa kutokana na kutotekelezwa kwa makubaliano yaliyoingiwa na Marehemu Maalim Seif Sharif Hamad kwa niaba ya ACT Wazalendo Rais Mwinyi kabla ya ACT Wazalendo kujiunga na Serikali ya Umoja wa Kitaifa," amesema Shaibu.

Shaibu amesema kuwa hatua hiyo imekuja baada ya kufanya tathmini ya kina iliyofanywa na Halmashauri Kuu ya Chama juu ya Mwenendo wa Serikali hiyo ambao unaonesha kuwa, ukiacha suala la kuachiwa huru kwa wanachama wa Chama hicho waliokuwa wanashikiliwa kutokana na Uchaguzi Mkuu 2020, hakuna hoja hata moja ya mageuzi ya kimfumo kati ya hoja tatu zilizowasilishwa ambayo imefanyiwa kazi na Rais wa Zanzibar Dkt. Hussein Mwinyi. 

Kwamba hoja zilizowasilishwa ni fidia kwa wahanga wa Uchaguzi Mkuu 2020, kuundwa Tume ya Kijaji kuchunguza uvunjifu wa haki za binadamu kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2020 na mageuzi katika mfumo wa uchaguzi.

Ameeleza kuwa katika Kikao hicho cha Halmashauri Kuu ya Chama ambacho kimekutana baada ya Mkutano Mkuu Taifa uliofanyika Machi 5 na 6, 2024 katika ukumbi wa Mlimani City, Dar es salaam, pamoja na mambo mengine, Halmashauri Kuu imefanya uchaguzi wa Wajumbe wa Kamati Kuu ya Chama wa kuchaguliwa kutoka kwenye Kanda 10 za Chama na teuzi mbalimbali zikiwemo za Uteuzi wa Katibu Mkuu na Manaibu Katibu Mkuu, Uchaguzi wa Wajumbe wa Kamati Kuu, Uteuzi wa Wajumbe wa Halmashauri Kuu, Uteuzi wa Sekretarieti ya Chama na Uteuzi wa Mkaguzi Mkuu wa Ndani.