Zinazobamba

KC MABWEPANDE WAADHIMISHA SIKU YA MWANAMKE DUNIANI KWA KUTOA ELIMU NA MSAADA ZAHANATI YA MABWEPANDE

Baadhi ya Wanachama wa Kituo cha Taarifa na Maarifa kata ya Mabwepande, Viongozi wa Serikali ya Mtaa wa Mbwepande, Mtoa huduma na wapewa huduma wa Zahanati ya Mabwepande wakiwa katika picha ya pamoja baada ya Elimu ya Wanawake na Uongozi pamoja na Elimu ya ukatili wa kijinsia iliyotolewa na Kituo hicho.

Na. Vicent Macha DSM.

Wanawake wa kata ya Mabwepande wametakiwa kupendana, kuheshimiana na kushirikiana ili kuweza kuleta mageuzi katika nafasi za uongozi na hatimaye kuwa wengi katika nafasi za maamuzi.

hayo yameelezwa mapema jana Machi 8, 2024 na Mwenyekiti wa Kituo cha Taarifa na Maarifa wa Kata kata hiyo Bi. Fatuma Radhamani Nuru katika maadhimisho ya Siku ya Mwanamke Duniani, ambapo wao wameadhimisha kwa kwenda kutoa msaada katika Zahanati ya Mabwepande.

Mwenyekiti huyo amasema kuwa wao wameamua kuadhimisha kwa njia hiyo lengo likiwa ni kutoa msaada, lakini pia kutoa elimu ya Ukatili wa Kijinsia kwa Wapewa huduma na watoa huduma wa Zahanati hiyo ili kupunguza vitendo hivyo katika kata yao Mabwepande.

Ameongeza kuwa wametoa Msaada wa vitu mbalimbali kama vile Sabuni, Toilet Paper na dawa mbalimbali kwa ajili ya wagonjwa, na hii ni njia moja wapo ya kuendelea kumuunga Mkono Rais Dkt. Samia kwani yeye ni Mwanamke na ameonyesha kuweza hivyo ni vema kumuunga mkono kama Watanzania na siyo kumkatisha tamaa.

Bi. Fatuma ameendelea kuwasisitiza wanawake waweze kujitokeza kugombea nafasi mbalimbali za uongozi na ukizingatia mwaka huu kuna uchaguzi wa Serikali za Mitaa na Mwakani uchaguzi wa Madiwani, Ubunge na Urais na kuwataka wanawake waweze kujitokeza kwa wingi kugombea nafasi hizo.

Aidha amewataka wazazi kutofumbia macho vitendo vyote vya ukatili vinavyofanywa katika mitaa yao na kuwaomba wanapoona hali hiyo waweze kutoa taarifa Serikali za Mitaa, Polisi au kwa Mwana kituo cha taarifa na Maarifa ili kuweza kupata msaada wa haraka.

Na mwisho ametoa wito kwa wazazi na viongozi wa kata pamoja na mitaa hiyo kuweza kuungana ili kutokomeza ukatili kwa Wanawake na Watoto kwani Kata ya Mabwepande bado inaukatili huo ingawa siyo mkubwa sana lakini wakishirikiana wataweza kuutokomeza kabisa.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Mabwepande Mwalimu Mussa Mangwala amesisitiza suala la utoaji wa taarifa endapo mtu anaona kitendo cha ukatili basi asikae kimya aweze kutoa taarifa na wao kama serikali watahakikisha hatua stahiki zinachukuliwa kwa mtenda kosa.

Ameongeza kuwa ujumbe wake katika maadhimisho ya siku ya wanawake Duniani ni kuwa na upendo, kwani ukiwa na upendo jirani yako au Mtoto wa jirani akifanyiwa ukatili uwezi kukaa kimya lazima utatoa taarifa sehemu husika.

Hakuna maoni