Tuwe na shabaha moja
ADELADIUS MAKWEGA-MBEYA.
Nilitoka Isimani Tarafani na
Kupanda Hiace moja iliyokuwa Ikifahamika kama Mwitula kuelekea Iringa Mjini,
kumbuka hiyo ilikuwa 2005 na mwaka huo ulikuwa ni mwaka wa Uchaguzi Mkuu, huku
njiani tukikutana na watu wakiwa wamevalia sare za CCM ambapo kwa wakati huo
tayari kampeni zilikuwa zimeshaanza.
Safari yetu iliendelea, huku
tukivuka kijiji cha Mkungugu, Ndolela mara Igingilanyi na sasa tukawa tunaingia
kijiji cha Nduli, hapa gari hili lilienda kwa sekunde kadhaa, upande wa kulia
kwangu wa dirisha kwa mbele niliona bendera ya TLP chapa Jogoo inapepea katika
nyumba moja barabarani, hii ilikuwa bendera pekee tangu nilipotokea Isimani. Wakati
natazama bendera hizo mara tunakasikaa mlio paaaaaaaaaaa…, gari lilienda kwa
sekunde 10-15 dereva akasimamisha na abiria tukiombwa kushuka.
“Nyielega! zemiyenu umutuka
upatiti pachaaa! Mwikie.”
Alisema kondakta wa Hiace
hii. Niliuliza anasema? Jirani yangu kwenye siti akaniambia gari imepata pacha,
tushuke, tulishuka harahaharaka, nilikumbuka hapa si ndipo nilipoziona bendera
za TLP? Nikaamua kuvuka barabara hii ya Iringa Dodoma nikaongee na wale wenye
nyumba yenye bendera za TLP. Nilifika nakuwasalimia watu wakubwa wawili mke na mume,
shikamoo! Wakajibu marahaba, nikawaambia naomba kujisaidia, wakaniekeza uani na
mimi kwenda huko, nilipomaliza nikarudi. Nikaambiwa kijana karibu benchi,
nikakaa. Huyu mzee akisema gari hilo bado hadi watoe tairi mpaka waweke itatumia
dakika kama 10.
“Pumzikaga baba!, gari
zenyewe zimechoka hizo na barabara yenyewe vumbi tupu, mwanzo mwisho.” Aliongea
mama ambaye alikuwa jirani na huyu mzee.
Mzee huyu ambaye alikuwa
mchangamfu sana, nyumba yake ilizungukwa na mianzi mingi ambayo ilipamba nyumba
yake vizuri huku ikionekana kuwa alikuwa akijapatia kipato cha kuvuna pombe ya
ulanzi kwani palikuwa mianzi mingi .
Mzee huyu aliniuliza na wewe
nani? Nilimjibu jina langu na mimi ni mwalimu. Nikaulizwa wa wapi? Nikamjibu wa
Isimani Sekondari, akaniambia karibu mwalimu. Pale shuleni kwenu kuna mwanangu
anasomo kidato cha pili anaitwa Zamoyoni.Tuliongea vitu vingi huku mzee huyu
akiwa mchokozi wa mada. Mimi nikaupata upenyo wa kumuliza juu ya TLP?
Kwanini wewe siyo CCM kama
hawa wenzako?Maana kote nitokako ni CCM tu.
“Unajua mwalimu sikiliza!
CCM wana shinda moja kubwa, wanadhani nchi hii ni mali yao, kumbe nchi hii si
maIi yao, bali wao wanapewa dhamana tu kwa kipindi cha miaka mitano mitano.” Alinijibu
mzee huyu kwa ujasiri.
Alisisitia kuwa yeye huwa
anagombea kwa nia moja ya kutoa elimu ya uraia kwa jamii si kwa kushinda,
akisema kuwa anaamini iko siku elimu hiyo ya uraia itazaa matunda. Basi dereva
wa Hiace hii ya Mwitula alipiga honi pipiiii… akitujulisha kuwa tayari
wameshabadilisha tairi, nikamuaga mzee huyu nikamwambia nashukuru kwa
kukufahamu.
“Mwalimu karibu sana,
ukirudi upitia nikupatie ulanzi.” Nikamjibu
asante sana.Tuliendelea na safari yetu na barabara ya vumbi, tukafika pahala
sasa palikuwa na lami ikianzia hapo hadi Iringa Mjini, tukiwa tumetapakaa
vumbi.
Nilipofika Iringa Mjini
nilikutana na bendera nyingi za CCM kama kawaida yake, huku pia zikiwamo
bendera za TLP na wakati huo Mchungaji Peter Msigwa akigombea ubunge kwa tiketi
ya TLP na hata nilipokuwa nikienda chuoni jirani na chuo cha Tumaini kulikuwa
na bendera moja moja za NCCR na CHADEMA.
Nilipata nyumba ya kuishi
maeneo ya Mtwivila-Mwangingo ambapo kulikuwa jirani mno na Makaburi ya Mtwivira/
Kihesa. Eneo hili lilikuwa na mianzi mingi ambapo nilipata nyumba kwa Mzee mmoja
maarufu kama George, huyu alikuwa dereva wa mabasi ya King Cross haya yalikuwa yanafanya
safari zake Iringa Dodoma kila siku..
Mzee huyu alikuwa muisilamu
safi, ambapo kila ibada alikuwa anashiriki. Nilipomzoea nilimuuliza mbona jina
lako la kikristu na ni muislamu ? Alinijibu tu kuwa alikuwa mkristu kweli lakini
kuna wakati alifanya kazi wa tajiri wake mmoja, alikuwa mtu mwema na mkarimu
kwa hiyo alivutiwa na maisha hayo ndiyo maana sasa ni muisilamu. Mzee huyu
alikuwa na watoto wakubwa aliyozaa na mke wake wa kwanza ambaye wakati nafika
hapo niliambiwa alifariki kitambo na walikuwa aidha madereva wa mabasi,
makondakta au mafundi mabasi ya safari ndefu.
Watoto wa mzee George
walikuwa wakristu wakishiriki dominika na hawakugombana hata siku moja nikiwa
pale na baba yao. Lakini nilimkuta na mke mwingine ambaye nayeye alikuwa ni
mkarimu sana, huku akifanya biashara sokoni Iringa Mjini. Alikuwa akiishi na
watoto wawili mmoja wa kike na mmoja wakiume ambao walikuwa watoto wa mwisho kwa
mkewe wa kwanza wa Mzee George.
Nikiwa naishi hapo huku
nikisoma Chuo cha Tumaini Iringa, Mzee George alifariki na tukamzika vizuri kwa
mama yake mzazi huko Makanyagio. Mzee huyu alipofariki ilibainika kuwa
aliwaagiza watoto wake wamtunze mama yao hadi tamati ya uhai wake huku akisema
kuwa wasimfukuze mama huyu katika nyumba hiyo hasa katika chumba alichokuwa
akiishi naye. Kwa kipindi chote nilichokuwa hapo agizo hilo nilibaini kuwa
walilitekeleza. Nyumba hii ilikuwa na pande mbili, kulikuwa na upande wake
mwenyewe mwenye nyumba(marehemu mzee George) na upande wapangaji, tulikuwa
hatukutani.
Upande wa wapangaji ulikuwa
na vyumba nane viwili kwa familia moja. Kulikuwa na familia nne kimoja mimi, kimoja
alikuwa kaka mmoja na mkewe wafanyabiashara wazuri sana wa vifaa vya ujenzi,
kulikuwa na muuguzi mmoja na kaka mmoja mpishi katika hoteli moja Iringa Mjini.
Nilipofika katika nyumba hiyo nilimzoea muuguzi kwa kuwa nilibaini kuwa kaka
yake niliwahi kufanya kazi na kaka yake alikuwa mwalimu mwezangu huko kijijini
nilipokuwa. Huyu mwaliimu mwenzangu wa Isimani alikuwa na mkewe alikuwa akifika
kumsalimia wifi yake.
Ahh mwalimu Makwega unakaa
hapa? Nikasema ndiyo, masomo yanaendaje? Nikasema yanaenda vizuri, aliniambia
kuwa nimekuja kumsalimia wifi yangu huyu nesi, nikajibu sawa. Kwa mimi binafsi sikuwa
na budi nilimzoea huyu nesi akawa kama ndugu yangu.
Nilipoondoka isimani,
nilikuwa na kuku kadhaa wa kienyeji, nilipokaa katika nyumba hii kwa muda niliona
kuna wafugaji wezangu kwa hiyo nilienda Isimani kuwachukua kuku wangu kama 24
na kumuomba muuguzi huyu ambaye alikuwa na banda kunisaidia kuwachanganya na
kuku wake. Nilikaa kwa muda wa mwezi mmoja nikaenda Mbagala kupiga kura mwezi
Oktoba, 2005. Wakati huo Mbagala ilikuwa sehemu ya jimbo la Kigamboni ambapo
kwa nafasi ya Ubunge Jimbo la Kigamboni alishinda Mwichumu Abdul-raham Msomi
huku ukizijumlisha kura za CUF na CHADEMA wakati huo zilizidi kura za ndugu
yangu huyu wa CCM Mheshimiwa Mwinchumu. Huku vyama vya upinzani vikiwa na
wagombea lukuki kila mmoja luwake kwa nafasi ya urais, ubunge na udiwani.
Ulipokwisha uchaguzi nikarudi chuoni Iringa kuendelea na masomo na ilipofika
Disemba nikarudi tena Mbagala na kula Krisimasi.
Kabla ya kuondoka kwenda Dar
es Salaam nilibaini kuwa nyumba hii ilikuwa na shida moja ya kuwepo kwa panya
ambao walikuwa wanaharibu sana vitu. Hapa kila mmoja alikuwa anapambana
kivyake, ukiingia chumbani kwako ukimkuta panya unamuua, kama unaweza kuweka
mtego, unamtega lakini njia hizo hazikuwa na tija. Mimi niliamua kuchukua
chakula kidogo na kutafuta sumu ya panya na kuwatega chumbani kwangu na
kuondoka zangu Dar es Salaam.
Siku niliporudi kweli
nilikutana na panya wengi wakiwa wamekufa niliwakusanya kutoka kila kona
nyanyua viti na vitanda huku nikifanya usafi maana harufu ilikuwa ya kutosha.
Niliwakusanya na kuwachimbia shimo na kuwafukia.
Sote kwenye nyumba hii kila
mmoja anapambana na panya kivyake akifa anamtupa ajuavyo. Sasa hakuna anayetambua
kama mwenzake kaweka sumu au katumia mtego wa panya na kwa bahati mbaya panya
hawa walikuwa na uwezo wa kuingia kila chumba. Sumu inawezekana nimetenga mimi
panya akafika kwa muuguzi au kwa mfanyabiashara. Kumbuka msomaji wangu kuwa
mimi nina kuku nimeziweka kwenye banda la muuguzi kuku hawa kule tunapotupa
uchafu ndiyo malishio yao.Kuna siku tuliamka asubuhi na kukuta kuku 48
wamekufa.
Kuku karibu 48 walikuwa
wenye thamani ya kama 336,000/ kama wangeuzwa kwa 7000/ walikufa ambapo
mshahara wa Afisa Elimu Msaidizi daraja wa tatu ulikuwa ni 108,000/.
Sasa muuguzi akawa anasema
kuwa hawa kuku itakuwa wametolewa kafara na huyu mfanyabiashara na ndiyo maana
duka lake linajaa vifaa si bure, haiwezekani kufa pamoja kuku wote, kwa kuwa
ugonjwa ulishapita, na hata kama ugonjwa wangekufa mmoja mmoja. Ugomvi ukawa
mkubwa watu hawasalimiani. Kwa kuwa hasara tuliopata ni mimi na muuguzi, mimi
nikawa bize na chuo, huku nyumbani narudi usiku, kumbe watu hawana amani. Niliongea
na niliyekuwa nimemzoea yaani muuguzi, nikamwambia dada mimi nadhani kuku wetu
watakuwa wamekula sumu tu. Mimi nilitenga sumu chumbani kwangu na niliporudi
nilifanya usafi. Muuguzi alisema mwalimu hilo hapana hapa pana mkono wa mtu
mbona mimi kila mara natega sumu mbona kuku hawafi? Sikuwa na jibu.Balaa lilizidi
na mimi kumaliza Chuo na kurudi Dar es Salaam, huku kila mmoja akiikimbia
nyumba hii.
Naona leo hii naiweka kalamu
yangu chini hapo, nia ilikuwa ni kuwaua panya ambao walikuwa wakiharibu vitu
vya thamani ndani ya nyumba hii ya Mzee George. Sasa kitendo kilisababisha kuku
wetu 48 kufa na sie kupata hasara. Huku amani ikitoweka katika nyumba hii. Yote
hii ilitokana ni kisa cha kila mmoja kupambana na panya hawa kivyake, huyu
kaweka sumu, huyu kaweka mtego huyu kamuua kwa kumbahatisha kimeleta shida na
migogoro ndani ya hii nyumba hadi wengine wakiikimbia na kutafuta nyumba
zingine.Tungefanikiwa kuwamaliza panya wale kama tungekaa pamoja na tungekuwa
na shabaha moja kwa hakika panya wale wangekufa.
0717649257
No comments
Post a Comment