Zinazobamba

DIWANI KATA YA BUYUNI AZUNGUMZIA UTEKELEZAJI WA MIRADI YA MAENDELEO NDANI YA SIKU 100 ZA RAIS DKT. SAMIA.


Na Mussa Augustine.

Kata ya Buyuni imeendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo ndani ya siku 100 za uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan,miradi inayolenga kuboresha huduma za Elimu,Afya, Miundombinu pamoja na kuimarisha ulinzi na usalama kwa wananchi.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Januari 15,2026 Ofisini kwake,Diwani wa Kata hiyo,Mh.Jesica Mahmoud Msolla, amesema kata hiyo imebahatika kuanza utekelezaji wa hatua mbalimbali muhimu, ikiwemo kuhakikisha wazee wanapatiwa bima ya afya, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa ahadi ya Rais Dkt. Samia.

Amesema Buyuni yenye mitaa nane tayari imeanza mchakato wa kuwatambua wazee wote wanaohitaji bima ya afya, zoezi linaloratibiwa na wenyeviti wa mitaa kwa lengo la kuhakikisha wanapata huduma salama wanapofika katika vituo vya kutolea huduma za afya.

Katika eneo la kuinua uchumi wa wananchi, Diwani Msola amesema Serikali kupitia Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam imeshatoa angalizo kuhusu utoaji wa mikopo ya asilimia 10 kwa wanawake, vijana na makundi maalumu ikiwemo watu wenye ulemavu.

“Hadi sasa tumeshaanza kuandaa na kuratibu vikundi vyote vinavyostahiki kupata mikopo hii ya asilimia 10, ikihusisha makundi ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu,” amesema Msola, akiongeza kuwa jukumu lililobaki ni kuendelea kuweka mazingira wezeshi yatakayowawezesha wananchi kunufaika na fursa hizo za kiuchumi.

Akizungumzia sekta ya elimu, amesema mchakato wa ujenzi wa shule ya watoto wa makundi maalumu tayari umeanza, ikiwa ni utekelezaji wa maelekezo ya Serikali ya Awamu ya Sita ya kuhakikisha haki ya elimu inapatikana kwa watoto wote bila ubaguzi.

“Ninamshukuru sana Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, lakini pia naushukuru uongozi wa Wilaya ya Ilala kupitia Mkuu wa Wilaya, Edward Mpogolo, kwa kuwa mstari wa mbele kusikiliza na kushughulikia mahitaji ya kata yetu,” amesema.

Aidha, amesema kata hiyo imepewa kipaumbele cha kujenga shule kubwa ya ghorofa ili kupunguza msongamano wa wanafunzi na kuboresha mazingira ya ufundishaji na ujifunzaji, huku fedha za utekelezaji wa mradi huo zikiwa tayari zimetengwa.

Katika sekta ya afya, Diwani Msolla amesema zahanati ya Buyuni imeboreshwa na sasa imepanda hadhi kuwa Kituo cha Afya Buyuni, ambacho kipo katika hatua za mwisho za kukamilika. Kituo hicho kinatarajiwa kutoa huduma za mama na mtoto pamoja na huduma za upasuaji kwa wajawazito, hatua itakayosaidia kupunguza vifo vya mama na mtoto.

“Naishukuru sana Serikali kwa kuendelea kuzingatia afya ya mtoto chini ya miaka mitano pamoja na mama mjamzito,” amesema.

Kuhusu miundombinu, amesema tathmini ya barabara na madaraja yaliyoharibika imekamilika kwa kushirikiana na Ofisi ya Mbunge, na ujenzi wake unatarajiwa kuanza rasmi Februari 15. Amesema barabara ya eneo la Njia Nne hadi barabarani Italia, mpakani mwa Jimbo la Kivule na Ukonga, itajengwa kwa kiwango cha lami na kuwekewa taa.

“Ni hatua kubwa sana kwa wananchi wetu, na tunashukuru Serikali kwa kutupa fursa hiyo,” amesema.
Ameongeza kuwa tayari kifusi cha muda kimeshawekwa katika baadhi ya barabara za ndani ili kurahisisha usafiri hasa kipindi cha mvua, huku madaraja yanayokuwa kikwazo kwa wananchi yakishafanyiwa tathmini kwa ajili ya ukarabati.

Diwani Msolla amesema ifikapo Februari 15,mwaka huu kazi za kushughulikia barabara za ndani zitakuwa zimeanza rasmi,na kumshukuru Mbunge wa Ukonga, Bakari Shingo, kwa ushirikiano wake.

Katika masuala ya ulinzi na usalama, amesema kata hiyo imeimarisha mfumo wa ulinzi shirikishi kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi, wenyeviti wa mitaa pamoja na wananchi. Amepongeza Jeshi la Polisi Kata ya Buyuni kwa juhudi zao katika kuhakikisha usalama wa raia.

“Mimi nimeweka kipaumbele kikubwa kwenye ulinzi na usalama. Kulikuwa na changamoto awali, lakini kwa sasa tumerejesha hali ya utulivu na tunaendelea kuimarisha mifumo yetu,” amesema.

Amehitimisha kwa kuwahakikishia wananchi wa kata ya Buyuni kuwa ataendelea kusimamia na kufuatilia utekelezaji wa miradi ya maendeleo na kijamii,kwa kuzingatia mwelekeo na falsafa ya Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.

No comments