Zinazobamba

Polepole yamemkuta vipi kwa Falahi?

 


 


ADELADIUS MAKWEGA-MBEYA

 

Disemba 17, 2021 Kamati ya Maudhui ya TCRA imetoa hukumu dhidi ya Runinga ya Mtandaoni ya Mbunge wa Bunge la Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Ndugu Humphrey Polepole kwa kituo hicho kupewa onyo kali, pili kipindi cha Shule ya Uongozi kusisimashwa kwa muda hadi awe na wafanyakazi wa taaluma ya uhandishi wa habari na utangazaji ili kuleta ufanisi na tija katika kazi yake na vipindi vyake visingatie misingi ya uhandishi wa habari.

 

Kama nionavyo mimi maamuzi haya ya kamati hii hayakuwa na haki bali ni uonevu kwa kuwa wajumbe wawili Haji Gunze na Jacob Tesha hawakutumia ipasavyo taaluma zao na uzoefu wao kuliamua jambo hilo.

 

Kulingana na taaluma ya habari na utangazaji, kuna aina mbambali ya vipindi katika Redio/Runinga kwanza kuna vipindi vya mahojiano haya yanakuwa katika mtindo wa maswali na majibu huku muda wake unategemea mahitaji ya chombo. Pili kuna vipindi vya makala hapa inategemea na maamuzi ya mtayarishaji na kuna wakati mwingine hata maswali na majibu inaweza kuwa makala huku ikiwa na vyanzo vya kutosha, muda wa makala unategema chombo husika.

 

TBC 1/TBC Taifa makala zao ni kati ya dakika 5-29.Tatu kuna ripoti za kawaida kama zile za matukio mbambali kwa kina inaweza kuwa ya kati ya dakika 2-4, lakini pia kuna habari za taarifa ya habari ambazo hizo Jacob Tesha mjumbe mmojawapo wa kamati hii ndizo alikuwa anazisoma tangu External service/RTD/DW KISWAHILI hapa msikilizaji  atasiki Lindi–Watu 100 hawana…Nairobi-Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya amekutana…,  Dar es Salaam-Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Ndugu Godwin Gondwe ametoa wiki…

 

Kuna kitu kingine ambapo huwa kuna vipindi vinavyofanywa na wenye taaluma /ujuzi huo. Hapa ndipo unapokutana na vipindi vya shule ambavyo vinakuwa kwanza vya muda mrefu kati ya dakika 40-120. Kwa kuwa kunakuwa na muhtasari(silabasi) ilikuukamilisha huo muhtasari kunakuwa na vipindi 1-40 kulinga na mahitaji ya muhtasari huo. Episode moja muda wake unategemea sana hiyo redio /Runinga inarusha matangazo yake kwa muda gani. Mathalani TBC episode moja inaweza kuwa kati ya dakika 14(15), 28 (30) au dakika 54 (60) kwa kuwa TBC wanatangaza saa 24.(Muda nilioweka katika mabano unahusisha na dakika za viashiria /signature tune vya katika kila episode moja.

 

Hapo nikumbushe jambo moja enzi za RTD kulikuwa na vipindi vya shule ambapo mwalimu alikuwa akifundisha na baadhi ya shule walikuwa wakifuatilia hilo. Palikuwa inasikika mandhari ya darasa huku wanafunzi wa studio wakiulizwa maswali na kujibu naye mwanafunzi anayesikiliza akiulizwa maswali na badaye majibu sahihi kutolewa kwa somo hilo. Hapa masomo kama Historia, Jiografia, Kiswahili,Kiingereza nakadhalika yalifundishwa. Nakumbuka hata baadhi ya shule walikuwa na ratiba ya vipindi vya redio kwa masomo yaliyokosa walimu na ratiba hizo zilikuwa zikitolewa na RTD tu mara baada ya shule kufunguliwa.

 

“Utasikio leo ni Jiografia darasa la tano, wanafunzi…”

 

Hata katika redio za kimataifa mathalani NHK, BBC, na DW wanavyo vipindi vya Jifunze lugha na michezo maalumu ya maigizo yenye lengo maalumu. Haya ni madarasa yenye kutoa elimu kama shule yakiwa na vipindi 1-30 (Episode) kulingana na mahitaji yao nakulingana nafasi wanavyokuwa hewana. Vipindi hivi vina nia ya kueneza utamaduni wao wa kutumia lugha, kufundisha juu ya magonjwa mbalimbali na hata siasa.

 

Mfano mzuri kabisa ambao naukumbuka ni madarasa yale ya RADIO D yalikuwa mafunzo ya Kijerumani ya hatua A1 na A2. Hatua A1 ilikuwa na kipindi cha 1 hadi 26 na hatua ya A2 ilikuwa na kipindi cha 27-52.

 

Hili kuitendea haki matini haya naomba nikumbushe tu hatua A1 kipindi cha 24, kipindi hicho kilipewa jina Dawati la Mhariri, kilizungumzia habari juu ya waandishi Paula na Philipo walivyoripoti nadhani habrai ya nyangumi aliyeonekana jirani na ufukwe na mizengwe kadhaa iliyotokea.

 

“Unasikiliza Radio D mafunzo ya Lugha ya redio ambayo ni mafunzo ya ubia baina ya taasisi ya Goethe na Deutsche Well ambayo yameandikwa na Bibi Merald Meeze…” Ndivyo yalivyonza mafunzo hayo ya lughwa yaliyowahi kurushwa hewani na DW Kiswahili.

 

Katika vipindi kama hivyo mfundishaji anaweza kuzungumza mwanzo hadi mwisho, anaweza akatumia michoro, picha kama anatumia runinga, pia anaweza akatumia vichekesho, michezo ya kuigiza, mashairi na nyimbo ilimradi ujumbe kufika kwa mwanafunzi wake.(hadhira)

 

Ndiyo kusema hii Shule ya Uongozi ilikuwa kama madarasa ya Radio D ya Bibi Merald Meeze, pia kama vile vipindi vya shuleni vya RTD na TBC na STARTV na ITV wakati wa wimbi la kwanza la Korona ambapo shule zilifungwa, runinga na redio zilikuwa sehemu ya madarasa kwa masomo mbalimbali.

 

Ndugu Polepole amekuwa Katibu wa Uenezi wa CCM na sasa ni mbunge na amefanya kazi kwa karibu sana na Marehemu John Magufuli anatambua mambo yanavyofanyika katika siasa za Tanzania kwa kina, kwa hiyo akaamua kutoa elimu kwa nduguze Watanzania.

 

Vipindi hivi vimekuwa vya saa karibia mbili na mwisho alitoa nafasi ya maswali ambapo alipata mrejesho iwe kwa ujumbe, kupigiwa simu au watu kutoa maoni katika kurasa zake za mitandaoni ikiwa sawa sawa na vipindi vile vya Radio D vya DW vya Bi Merald Meeze ambapo msikilizaji aliyekuwa anajifunza Kijerumani aliweza kuandika barua ya maswali kwa mtayarishaji na akajibiwa.

 

Kumbuka jambo moja la msingi msomaji wa matini haya kuwa huyu Ndugu Polepole yeye anafundisha darasani na ndiyo maana alikuwa na ubao wake kupitia runinga. Yeye hapa hafanyi ripoti kwa ajlii ya taarifa za habari, hafanyi ripoti kwa ajili kipindi cha majira, hafanyi kipindi cha maswali na majibu na wala hafanyi makala kama zile za TBC ambazo nilizielezea kwa kina kule juu. Yeye anafundisha kama darasani katika shule yake ambayo muhtasari wake au mwongozo anao yeye mwenyewe kama yalivyokuwa mafunzo ya jando na unyago.

 

Kwa sasa watu wengi wamesoma, shuleni mwalimu anatayarisha somo lake alafu anaenda kulifundisha fu darasani, kisha anatoa nafasi ya maswali mwishoni akimaliza atafunga kipindi mtakutana naye kipindi kijacho kwa mujibu wa silabasi yake.

 

Kwa hoja ya maadili ya uandishi wa habari katika shule ya uongozi nadhani siyo pahala pake kabisa kama ilivyo kwa watayarishaji wa vipindi vya RTD vya shule na kipindi cha Radio D cha Bi Merald Meeze labda yale maadili ya ualimu na sina hakika kama kama Ndugu Polepole alinukuliwa akitoa tusi.

 

Kwa hoja ya misngi ya uhandishi wa habari ya mizania hapa haisuki kabisa. Kwa mfano mwalimu wa Historia darasa la sita anayefundisha namna wamisionari walivyoshiriki katika ukoloni alafu unamwambia aletwe pardiri aje kusema upande wake, hapo haikubaliki kabisa ni kuliharibu darasa hilo. Hapo linalo fundishwa ni kulingana na muhtasari wake wa somo hilo.

 

Kwa hoja juu ya kuajili watangazaji wenye sifa za utangazaji na uandishi wa habari si sahihi hii ni shuleni. Runinga, redio, youtube na mitandao ya kijamii inapitia tu na ndiyo maana Ndugu Polepole anaweza hata akafundisha katika chumba au ukumbi na shule ikaendelea kama alivyokuwa akifanya baadhi ya maeneo aliyoalikwa.

 

Hapo ninavyoona kwa maamuzi wa TCRA ni kama wanamwambia kuwa Ndugu Polepole aende akajifunze taaluma ya uandishi wa habari au awe aje mtu aliyesoma taaluma hiyo alafu amualika yeye kama mgeni ambalo nadhani hilo ni jambo halikubaliki.

 

Kuhusu watumishi wake kuwa na taaluma ya habari na utangazaji waliokuwa wanatumika ni wajuzi wa sauti, michoro na picha za mnato na video tu. Yeye hana shida ya mhariri. Kama walivyofanya RTD na TBC kwa mafundi mitambo ambao wanafanya vipindi vya shule kwa kurekodi.

 

Niliwahi kuambiwa na rafiki yangu mmoja ambaye wakati huo akiwa mwanafunzi wa sheria Hendry Msaki ambaye sasa amefariki kuwa panapofanyika maamuzi yoyote juu ya jambo lolote lile hulka ya yule anayeamua  jambo hilo huwa ni kitu cha msingi sana hata katika muktadha wa kimahakama.

 

Aliniambia kuwa mathalani katika kesi za mauwaji kuna majaji huwa wana hulka mara zote katika kuhukumu kesi hizo za mauwaji wapo wanaotoa hukumu ya kifungo cha maisha badala ya ile ya kunyongwa hadi kufa. Wengine akigundua kuwa mshitakiwa kulingana na ushahidi ameua kwa kukusudia lazima hukumu ya kunyongwa hadi kufa itatolewa. Bila ya kujali kuwa hapa jaji sheria inampa nafasi ya kuchagua upande fulani.

 

Binafsi naona kamati chini ya Mwenyekiti Haji Gunze na wajumbe wake Jacob Tesha na Dereck Mujuruni hawakutumia vizuri nafasi zao na taaluma zao katika kuliamua jambo hilo. Kitendo cha kuitumia sheria kila mara katika taaluma ya habari kinadumaza kazi hii, kwa kuwa sheria ni sehemu ndogo sana ya uwanahabari.

 

Katika wajumbe wa kamati hii ambaye kidogo anaonekana anafahamu suala la utangazaji ni Jacob Tesha. Yeye kulingana na wasifu wake ana Shahada ya Kwanza Uongozi na Mahusino ya Kimataifa na Shahada ya Pili ya Mawasiliano ya Umma. Ambapo kwa utafiti wangu nilibaini kuwa elimu hiyo aliipata akiwa tayari mtumishi wa RTD.

 

Nimebaini kuwa kwa sehemu kubwa utangazaji alijifunzia akiwa kazini RTD huku sauti yake iliwavutiwa RTD kumuajili kama mtangazaji wakati huo. Pia amewahi kufanya kazi ya Shirika la Utangazaji la Ujerumani (DW Kiswahili). Nionavyo mimi kwa sehemu kubwa Jacob Tesha alitakiwa kuwaongoza wenzake katika kusaidia kuutatua mgogoro huo ambao ulikuwa ni mdogo tu.

 

Kwa mfano kwa heshima yake Ndugu Polepole angeshauriwa kipindi chake kisiwe darasa sasa kiwe kama Makala, hapo mngemtafutia vijana wazuri kutoka TBC, Azam TV, ITV au STAR TV wakamuongoza kwa muda wa mwezi mmoja mkatazama muelekeo wake hakika angekuja na makala nzuri sana. Au Tanzania kwa sasa mtu akitoka katika nafasi yake hapaswi kuheshimika?

 

Katiba yetu ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania 18 (2) kuna wakati iliesema kuwa

 

“Kila raia anayo haki ya kupewa taarifa wakati wote kuhusu matukio mbalimbali nchini na duniani kote ambayo ni muhimu kwa maisha na shughuli za wananchi, na pia juu ya masuala muhimu kwa jamii.”

 

Kukimbilia kufungia vyombo haina tija kwa kuwa wenye vyombo binafsi wanaisadia mno serikali ila wanapaswa kulelewa vizuri kwa kuaminiana, Kwa mfano kama Ndugu Polepole ambaye ni Mbunge wa kuteuliwa na Rais na amewahi kuwa katibu uenezi wa CCM taifa, TV yake inafungiwa kwa hoja hizo inakuwaje kwa mtu wa kawaida anaweza kuwekeza katika biashara ya vyombo vya habari? Sote ni Watanzania tujitahidi kulitazama hili kwa kina.

 

Wizara husika na TCRA wajitahidi sana kuwa na aina ya wajumbe wa Bodi/kamati wenye mchanganyiko mzuri siyo tu wale waliowahi kufanya kazi na serikali na kuwa jirani na viongozi wakubwa mathalani haji Gunze amefanya kazi na Waziri Mkuu enzi za Jaji Warioba kama msaidizi wa Habari na Jacob Tesha kafanya kazi na Mizengo Pinda.. Wakiwa na mlengo wa utii wa kila jambo. RTD /TBC na sasa ITVna magazeti mengi ya zamnai wanao watumishi wengi waliostaafu na wana uzoefu mkubwa watumiwe katika Bodi/kamati za utangazaji wapo majumbani wakicheza na wajukuu watumike na siyo majina yaleyale. Kwa leo naweka kalamu yangu chini hapo, nikukutakia siku njema.

makwadeladius@gmail.com

0717649257

 

No comments