SIKU 100 ZA DKT.SAMIA YOMBO VITUKA YAENDELEA KUTEKELEZA MIRADI YA MAENDELEO KWA KISHINDO.
Na Mussa Augustine.
Akizungumzia na Waandishi wa habari katika mahojiano maalumu Diwani huyo amesema kuwa utekelezaji wa miradi hiyo unaendelea huku akiwaomba Wananchi kuendelea kumpa ushirikiano ili kuweza kufanikisha malengo yake ya kuwaletea maendeleo.
Akizungumzia kuhusu miundombinu amesema kuwa utekelezaji huo umelenga katika miradi ya barabara,Vivuko,pamoja na Maji,ili kuwaondolea adha mbalimbali wanazopata Wananchi.
"Katika kipindi hiki cha miaka mitano,tutakua na barabara tatu za DMDP awamu ya pili,hizi barabara zitajengwa kwa kiwango cha lami,tunayo barabara ya Msikitini(Malawi Msikitini) yenye urefu wa Kilometa 0.45,itagharimu zaidi ya shilingi bilioni 1.3,pia tuna barabara ya Nyika Mwembeni yenye urefu wa Kilometa 0.44 ambayo itagharimu zaidi ya shilingi bilioni 1.5,pamoja na barabara ya Malawi West ambavyo itakua ya kiwango cha lami,mifereji pamoja na taa za barabarani,ina urefu wa Kilometa 0.28, itagharimu zaidi ya shilingi bilioni 1.9." amesema Kashakala.
Aidha kuhusu ujenzi wa vivuko amesema kuwa kuna ujenzi wa kivuko cha Mbeda mtaa wa magogoni,kivuko cha Mpeta pamoja na kivuko cha Bajuni,ambapo ujenzi huo ukikamilika utasaidia kuondoa changamoto mbalimbali zinazowakumba Wananchi hususani katika kipindi cha msimu wa mvua.
Katika upande wa Sekta ya afya Diwani Kashakala amemshukuru Rais Dkt.Samaia Suluhu Hassan kwa kuwapendelea kwani wanatarajia kutekeleza mradi mkubwa wa kujenga hospitali ya ghorofa tano,itakayogharimu zaidi ya shilingi bilioni tano nakwamba itajengwa katika eneo la sigara stendi.
"Kama rais Dkt.Samia alivyotoa ahadi yake ya siku mia moja,tayari tumeanza kuona baadhi ya mambo aliyoahidi yameanza kutekelezwa kwa kasi kubwa sana katika upande wa sekta ya Afya kwa mantiki ya Wafanyakazi,Vitendeakazi na Madawa." Amesema
Nakuongeza "katika upande wa afya kwa sasa kata ya Yombo Vituka tuna Zahanati ya Sigara,pamoja na kituo cha Afya Malawi,hivyo katika kipindi hiki cha miaka mitano tukipata hospitali ya Wilaya kata yetu inaenda kufunguka zaidi.".
Aidha Diwani huyo ameendelea kusema kuwa katika upande wa sekta ya Elimu,atasimamia ujenzi wa vyoo vya watumishi wa shule ya Sekondari Rumo,ambapo ujenzi tayari umeshaanza kwa zaidi ya asilimia 70,na fedha tayari imeshatumwa kwenye akaunti ya shule,pia atasimamia ukarabati wa madarasa 10 katika shule ya msingi uwanja wa Ndege,ambapo ujenzi utagharimu kiasi cha shilingi milioni 125.
Aidha ameongeza kuwa atasimamia watoto wa kike wapatao 44 wanaotoka kwenye familia duni kwa ajili ya kuwawezesha chakula na nauli katika Shule ya Sekondari Rumo.
Vilevile kuhusu masuala ya kiuchumi kwenye kata hiyo amesema kata ya Yombo Vituka ina wakazi wengi ukilinganisha na kata zingine Wilayani Temeke,hivyo kumekuwepo na changamoto kubwa ya ajira kwa vijana,akina mama na akina baba.
"Yombo Vituka kwa kila mwezi tunazalisha wastani wa watoto mia mbili arobaini(240)ambapo kwa mwaka sawa na wastani wa watoto elfu tatu mia mbili (3200),mimi kama diwani nitaanzisha kanzi data kwa ajili ya kutambua Vijana wote waliopo kwenye kata yangu,pamoja na taaluma zao na vipaji vyao hatua itakayowezesha kuongea na Serikali na wadau mbalimbali ili kuwasaidia kupata ajira.
Halikadhalika kuhusu mikopo ya asilimia kumi inayotolewa na halmashauri kwa Vijana,akina mama na watu wenye ulemavu, Diwani huyo amesema kwa sasa anaendesha kampeni kwa kushirikiana na maafisa maendeleo kwa ajili ya kuwahamasisha kutengeneza vikundi na kuvisajili,pamoja na kupewa Elimu ya biashara ili kuondoa tatizo la urejeshaji wa mikopo.
Hata hivyo kuhusu ulinzi na usalama amesema kuwa wamekua wakisisitiza ulinzi shirikishi,nakutoa elimu kwa Wananchi kutambua umuhimu wa kuchangia ulinzi shirikishi.
"Katika Mitaa yetu mitano hali ni shwari,lakini bado tuna malengo na tumeshapata eneo tunataka kujenga kituo cha Polisi kikubwa chenye hadhi ya Wilaya katika kata ya Yombo Vituka." amesema
Amehitimisha kwa kusema kuwa kata hiyo haitobaki nyuma katika sekta ya michezo,hivyo ametoa ahadi kwa Vijana kwamba itaundwa kamati ya Michezo ambayo itashirikisha makundi mbalimbali katika kata hiyo ili kuweza kuwaunganisha Vijana kupitia michezo mbalimbali.

No comments
Post a Comment