Safari yake kwenda Taasisi ya Jakaya Kikwete
ADELADIUS MAKWEGA -MBEYA
Disemba 16 niliwasiliana na
ndugu yangu mmoja ambaye anaishi Lugoba Chalinze mkoa wa Pwani, ambaye siku
hiyo nzima nilimtafuta sikumpata, lakini jioni ilipofika nilimpata na nilipomuuliza
mbona alikuwa hapatikani? Ndugu yangu huyu alinijibu kuwa kwa siku nzima hiyo alienda
kuwapeleka muhimbili wazazi wake ambao walikuwa na ahadi ya kumuona tabibu na
kupata vipimo katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.
Ndugu yangu huyu aliniambia
kuwa ilikuwa kazi kidogo upatikanaji wake katika simu kwani aliiacha katika
gari kutokana na kuhangaika na wazazi wake hao, baba yake ana miaka 82 na mama
yake ana miaka 71 ambao ni watumishi umma wastaafu.
Ndugu yangu huyu alindokeza
kuwa wazazi wake hawa ni walimu wastaafu, kidogo matibabu yao kwa sehemu bima
ya afya inasaidia lakini kiyume na hapo mambo yangekuwa sawa na mtoto
anayejifunza kuandika, herufi hapo zingekuwa kichwa chini miguu juu, zingepiga
tikitaka. Kwa kuwa walitokea Lugoba, waliamka asubuhi sana na kuanza safari hiyo
saa 10 alfajiri na hii iliwasaidia kufika hospitalini mapema huku wakiyapita
maeneo ya Msata, Bagamoyo, Kawe na Mbezi kukiwa na kiza kinene na kweli asubuhi
na mapema walikuwa wamefika Muhimbili kwa matibabu.
Walipofika hapo waliingia na
kufuata utaratibu na kwa kuwa alikuwa na wazazi wawili, mama yake alienda
upande anaotakiwa, huku yeye akiongozana na baba yake kwani amepata tatizo la
kupoteza kumbukumbu, anahitaji mtu wa kusikiliza maelekezo ya tabibu na wakati
anatumia dawa akumbushwe vizuri.
Kweli alipokuwa katika
foleni, lilipokuwa likiitwa jina la baba yake kuelekea kwa tabibu, madaktari na
wauguzi walikuwa wakimwambia mbona unaambatana na baba yako kila sehemu, mbona
anajieleza vizuri? Kwanini usimuache yeye mwenyewe? Aliwaeleza ile shida ya
baba yake ya kupoteza kumbukumbu.
Kwa kuwa walikuwa wakipata
huduma hiyo Taasisi ya Jakaya Kikwete, ndugu yangu huyu ananiambia kuwa taasisi
hii ni kubwa na ya mfano. Anadai kuwa ni miongoni mwa kazi kubwa alizozijenga
Ndugu Jakaya Kikwete enzi ya serikali yake ya awamu ya nne.
Nilimuuliza mbona anamsifia
sana Jakaya au kwa kuwa ni ndugu yake? wanatoka wote Chalinze? Alnijibu hapana,
kwa kuwa yeye(huyu ndugu yangu) ni mtaalamu ya masuala ya tiba anakumbuka watu
walivyokuwa wakiteseka miaka ya nyuma. Huku akitolea mfano pia ujenzi wa
Hospitali ya Benjamin Mkapa ya Dodoma.
Ndugu huyu anasema kuwa
taasisi hizo ni sawa na kuku mweupe lakini kwa sasa kumekuwa na doa jeusi
katika suala la gharama za matibabu. Nilimuuliza kwani gharama zikoje?
Alinijibu kuwa siku hiyo akiwa hapo wakati baba yake anachukuliwa vipimo
aliisikia familia moja wakilalamika juu ya kupatikana pesa za kufanyiwa
oparesheni mzazi wao aliyelazwa hapo.
Shida ambayo kwa Watanzania
wengi imekuwa mwiba unawasumbua mno, anasema kuwa familia hiyo waliamua kuuza
nyumba yao ili kuokoa uhai wa mzazi wao, huku wakisema kuwa nyumba siyo embe,
wakijiuliza kama mteja atapatikana mara moja. Kwa meelezo ya ndugu yangu huyu
anasema kuwa aliwaacha ndugu hawa wakiendelea kulijadili jambo hilo juu ya
kumnusuru ndugu yao mgonjwa namna ya kupata pesa, anadai kama walipata au la
pesa hizo, yeye hafahamu.
Ndugu yangu huyu kwa kuwa
alipokuwa katika benchi malalamiko ya familia hii na mjadala juu ya namna ya
kupata pesa ulimuhuzunisha sana, aliamua kutoka nje angalau muda uende ili baba
yake apimwe haraka waondoke.
Ndugu huyu alitoka nje ya Taasisi
ya Jakaya Kikwete ambapo ipo jirani sehemu ya kuhifadhia maiti ya Hospitali ya
Muhimbili, anasema kuwa hapo alikaribishwa na mandhari ya ndugu waliofiwa wakienda
kuchukua miili ya ndugu zao.
“Hapa niligundua jambo jipya
ambalo liliniumiza zaidi ya ule mjadala wa matibabu, mtu mwingine anakuja hiace
ambayo inabeba abiria, wengine malori,
wengine wakija na magari ya kifahari ya kila aina kuchukua maiti hizo. Wengine
wakiwa watu wengi na magari kadhaa, wengine watu wachache tu .” Aliendelea
kunisimulia ndugu yangu huyu.
Akiwa nje, kwa kando
alimsikia mtu mmoja akiongea na simu juu ya ndugu yake aliyefariki akisema kuwa
sasa jamani changisheni pesa haraka ili mje na gari tumchukue.
“Nendeni hapo Tandika Stendi
zipo hiace, ulizeni gharama yake ni kiasi gani kuubeba mwili, mimi tayari nina
elfu 50,000/-.”
Alisema ndugu huyo aliyekuwa
akiongea na simu.
Nilimsikiliza ndugu yangu
huyu na safari yake ya Taasisi ya Jakaya nikatafakari mno akilini mwangu.
Binafsi nilimwambia kuwa ni kweli Jakaya Kikwete alijenga Taasisi ya Jakaya
Kikwete (yenye jina lake), Benjamini Mkapa na Mlongazila zikawekwa vifaa tiba
na huduma kuanza kutolewa nia ni kusadia kupunguza adha ya kufunga safari India
na ughaibuni kupata matibabu hayo.
Nilimwambia kuwa Watanzania
tulio wengi ni masikini, lazima pawepo na utaratibu wa kila Mtanzania anapokuwa
mgonjwa apate nafasi ya kutibiwa kwanza, pesa ije baadae. Nilimuuliza vipi kama
mtu ambaye hakuwa mtumishi hali inakuwaje? Ndugu yangu huyu aliguna tu.
Katika suala la kusafirisha maiti
na wagonjwa nilishauri angalau kila kata kuwa na gari la wagonjwa la umma,
wananchi wao wachangie pesa ya mafuta tu kwa gharama ya chini.
Nilimwambia kuwa Ifahamike
wazi kuwa yanapokuwepo magari kama haya tunajiwekewa utaratibu wa huduma hiyo
sisi wenyewe kila mmoja katika maeneo yake, pale dharura inapotokea yanatumika
kwa wanaohitaji.
Kwa mfano Waziri, Mkuu wa
Mkoa, Mkuu wa Wilaya na hata mwananchi wa kawaida anaweza kupata tatizo vijijini
au njiani kutoka eneo moja kwenda lingine, kama ambulance ipo inaweza kuokoa
jahazi.
Kwa muda mrefu zinapotokea
ajali ni magari ya watu binafsi na Toyota Land Kruza za Jeshi letu la Polisi ndiyo
zinazotumika kubeba maiti na majeruhi, wakati si kazi yake kubeba maiti au
majeruhi.
Nilipokuwa namalizia
sentensi hiyo simu yangu ilikatika, maana chaji iliisha.
0717649257
Hakuna maoni
Chapisha Maoni