Sheikh Gorogosi alivyojenga mahusiano kati ya Waislam na Wakristo Mtwara
ADELADIUS MAKWEGA-MBEYA.
Mahusiano baina ya dini na dini ni jambo la msingi japokuwa dini
zenyewe zinajenga misingi ambayo kila dini iwe zaidi ya mwenzake. Huku kukiwa
na mtazamo wa kujenga umoja wa dini. Mahusiano baina ya dini na dini huwa yanaweza
kujengwa na dini zenyewe pia na udugu wa binadamu na binadamu mwenzake. Huku
misimamo ya dini ikibaki kama ilivyo juu ya mahusiano ya jamii hizo.
Misimamo ya dini imekuwa ikisisitiza watu wasioleane baina ya mtu
wa dini hii na ile huku katika baadhi ya maeneo misimamo hiyo kubadilika na
kuruhusu kufungwa kwa ndoa hizo na kila mmoja kubaki na dini yake. Lakini
katika jamii yetu japokuwa kumekuwa na misimamo hiyo bado wapo watoto waliozaliwa
kutoka wazazi wa imani tofauti huku mtoto akichagua pa kwenda baada ya kuwa mtu
mtu mzima au kufuata dini ya mzazi /mlezi anayemlea na kukaa naye muda mrefu.
Hilo limefanya katika baadhi ya familia kuwa na ndugu wa baba
mmoja, mama mmoja au baba na mama mmoja lakini wamekuwa na imani za dini
tofauti. Huku wakishirikiana vizuri katika mambo yote ya kijamii na hata ya
kiimani. Kwa bahati nzuri nchini Tanzania imani za dini zimekuwa hata katika
taasisi za umma na binafsi mathalani shuleni, wanafunzi wamekuwa wanashiriki
imani zao kikamilifu. Huko masomo ya dini yamekuwa yakifundishwa na kutolewa
nafasi za kuabudi. Kwa mfano katika shule za msingi kumekuwa na desturi ya
walimu wa dini kufundisha somo la dini, japokuwa katika baadhi ya dini wamekuwa
wazito kupeleka walimu wao mashuleni. Lakini baadhi ya dini zimekuwa na utaratibu
wa kuwapeleka walimu wa dini katika shule zetu kila siku ya kipindi cha dini ambapo
huwa mara moja kila wiki.
“Mtu ambaye anafuata imani ya dini kwa kiasi huwa na roho wa hofu
wa Mungu na hofu ya maisha yake baada ya kufa, kwa hiyo popote alipo atakuwa
mtu mwenye kufanya mambo ya kujitathimi katika kila jambo, iwe kiongozi atakuwa
na woga wa kutokudhulumu nafsi ya mtu.” Ndivyo inavyoaminika na baadhi ya watu.
Nakumbuka mwaka 1997 nilipokuwa mwanafunzi wa shule ya sekondari
Ndanda mkoani Mtwara, tukiwa shuleni hapo wanafunzi wote tulipata nafasi
kushiriki masomo ya dini, ibada na ruhusu ya kusali siku ya ijumaa-misikitini
na jumapili-makanisani zilikuwa sehemu ya ratiba ya maisha ya shule hii ya
bweni.
Nakumbuka kulikuwa na umoja wa wanafunzi wa wakatoliki, umoja wa
wanafunzi wa kikristo waprotestanti, umoja wa wanafunzi wakisabato na umoja
wanafunzi wa kiisilamu.
Nakumbuka Ndanda sekondari ilikuwa sehemu ya Jimbo Katoliki la
Tunduru-Masasi, majukumu ya ulezi wa wanafunzi wakatoliki alisimamia Padri
Particki Mwaya na nina imani kuwa hata waisilamu walikuwa na mlezi wao wa
kimkoa, waprotestanti na wasabato pia.
Nikiwa Ndanda nilibaini kuwa mahusiano baina ya dini na dini yanaweza
kujengwa na lakini pia yanaweza kubomolewa na binadamu wenyewe kutokana na
sababu za mtu binafsi lakini hekima ndiyo silaha kubwa ya kuepusha mifarakano
ya dini.
Mwaka huo 1997 kulikuwa na sherehe ya vijana wa kiisilamu walikuwa
wanahitimu masomo ya kidato cha nne, ili kuipamba sherehe hiyo walikubaliana
sherehe hiyo ikafanyike Masasi Girls ambapo ni shule iliyopo mwendo wa kama saa
moja wakati huo kutokea Ndanda. Kwa kuwa sherehe hiyo ilikuwa kubwa ilikutanisha
wanafunzi wote wa kidatao cha nne wa kiislamu wa mkoa wa Mtwara. Tulipofika Masasi
Girls nadhani ukumbi ulikuwa mdogo. Kwa hivyo ulitafutwa ukumbi mwingine ambapo
ulikuwa eneo la juu kabisa la Masasi kama unaelekea Tunduru. Sikumbuki ulikuwa
ukumbi wa taasisi ipi lakini ilikuwa taasisi fulani.
Wanafunzi wa Ndanda waisilamu walikuwa wengi kwa hiyo walimuona mkuu
wa shule ya Ndanda wakati huo Mwalimu James Mwassy, akaruhusu kutolewa Lori la
shule aina ya Isuzi kuwapeleka wanafunzi hao. Kwa utaratibu katika mahafali ya
dini yoyote wanafunzi pale Ndanda tulijiwekea utaratibu wa kualikana kulingana
na umoja unaofanya mahafali au sherehe yoyote ya kidini na pia kunatolewa
mwaliko kwa serikali ya wanafunzi. Hata kupatikana kwa Lori lililowabeba
wanafunzi wa kiislamu kwenda Masasi liliombwa kupitia serikali ya wanafunzi
shuleni hapo na mkuu wa shule hakuwa na tatizo.
Kabla ya kuanza safari ya Masasi, katika Lori hilo walipanda
wanafunzi wa kiislamu wenye mahafali tu (wengine walibaki Lori lilikuwa dogo)
na viongozi wa wao ambao hao hawakuwa wahitimu, pili walipanda waalikwa, hapa
walikuwa wale viongozi wa wanafunzi wa vikundi vya dini zingine na madhehebu
yao, mwakilishi wa serikali ya wanafunzi katika mahafali hayo (mimi) na pia
alipanda mwalimu msimamizi wa wanafunzi waisilamu. Kweli sherehe hizo zilianza
kwa kuchelewa sana maana mgeni rasmi alikuwa ni marehemu Selemani Gorogosi nadhani
alikuwa ni shehe mkuu wa Mkoa wa Lindi/ Mtwara huku akiwa Mufti Msaidizi kama
sijakosea.
Tulishiriki mahafali hayo vizuri, yakipambwa na kaswida, wanaume
wengi wakivalia kanzu na akina dada wakivalia hijabu zao na baibui. Wapo
waliokosa mavazi hayo wakivalia kanga na kujitanda na vilemba juu na mimi
sikujaliwa kuwa na kanzu bali angalau kuendani na mandhari sherehe hii nilipata
baraghashea.
Mahafali hayo yaliendelea huku nje kukipambwa na harufu nzuri ya
pilau ambayo ilinivutia mno na kuyahamisha mawazo yangu kwenye chakula hicho
ambacho nilikuwa sijakula muda mrefu, maana tukiwa Ndanda mlo ulikuwa ni Ugali
na Mbaazi kila siku.
Shekhe Gorogosi alikuwa si mtu mgeni sana kwangu kwani alikuwa
akifanya vipindi vya dini ya kiislamu (RTD) kama vile Maswali ya Dini ya Kiisilamu sauti yake na jina vilikuwa ni vitu
ninavyovifahamu. Kati ya watu walioshiriki mahafali haya, miongoni mwa watu
walikuwa wakubwa kwa kuwatazama nadhani shekhe huyu alikuwa miongoni mwao. Sasa
ulikuwa wasaa wa kupokea salamu kutoka katika waalikwa mbalimbali, nakumbuka
mtu wa kwanza kutoa salaam alikuwa Christopher Ungani (sasa ni miongoni wa
mchungaji katika kanisa la wasabato Tanzania) akiwawakilisha wasabato shuleni
Ndanda.
Ndugu Ugani alivalia suruali ya rangi kijani, shati jeupe ambalo
lilifungwa tai moja ndefu pana ambapo kwa kawaida wasabato huwa mara zote
nadhifu, ndugu huyu hakuvunjwa mwiko huo wasabato. Katika kutajwa kwa madhehebu
ya dini yaliyoalikwa ilibainika kuwa wakatoliki hawakuwa na mwakilishi wao, jambo
hilo lilimuibua shekhe Gorogosi. Aliuliza vipi kwanini hawakualikwa? Hoja hiyo
ilijibiwa kuwa mwaliko ulitolewa, aliuliza yule aliyepokea mwaliko huo alikuwa
nani? Swali hilo pia lilijibiwa. Shekhe Gologosi hakulidhishwa na majibu hayo.
Shekhe Gorogosi aliuliza katika wanafunzi mnaotokea Ndanda
Sekondari yupo mkatoliki yoyote alikuja kushiriki Mahafali haya nasisi? Hapo
palikuwa kimya baadhi ya wanafunzi wakinibonyeza. Shekhe Gorogosi alisimama na
kukabidhiwa mikrofone akauliza kweli hakuna mkatoliki aliyeshiriki mahafal haya
kwa kualikwa? Jambo hilo lilimuinua mwalimu anaowasimamia wanafunzi waisilamu
ambaye tuliambatana naye aliyefahamika kama Mwalimu Athumani Ali Nakalipa
aliokoa jahazi hilo na akasema yupo bwana Makwega.
Hapo niliitwa mbele nakukabidhiwa mikrofone kusema neno. Niliwasalimu
Salaam Aleikum! Wakaijibu Aleikuum Salaam.
“
Niliungama mbele ya Shehe Gorogosi kuwa kweli mimi ni mkatoliki
kama ulivyoambiwa, lakini mimi siyo kiongozi wa wakatoliki shuleni, nimekuja
hapo kuiwakisha serikali ya wanafunzi. Wanafunzi wakatoliki tunasimamiwa na
Padri Patriki Mwaya kwa jimbo la Tunduru Masasi(Shekhe Gorogosi alisema
namtambua vizuri).Sasa niianza kuwatetea viongozi wangu.
“Natambua viongozi hawa hawakufika pengine kutokana na changamoto
za usafiri tu, hilo lisikupe shaka Shekhe maana mahusiano yetu (Wakatoliki na
Waisilamu) ni mazuri sana ndiyo maana wamenikabidhi na mimi hii kofia (nilisema
huku naishika kofia yangu kichwani).” Hadhara ya mahafali walikuwa wanacheka tu.
Nilimwambia shekhe Gorogosi kuwa kiongozi wa wanafunzi alihama na
anayeikaimu nafasi hiyo ni muisilamu ambaye anatuongoza sote bila maneno. Nilimueleza
shekhe Gorogosi kuwa mimi nipo kidato cha sita na nyumbani ni Mbagala-Jimbo
Katoliki Dar es Salaam, kwa mazingira ya Mbagala Wakristu tunashirikiana vizuri
na waisilamu katika kila jambo.
Mimi katika michezo ya utoto nilikuwa nachezea timu ya mpira wa miguu
ya madrasa, lakini mie mkristo, wezangu wanasomo chuo mie niko nje, nawasubiria
wakitoka tunacheza pamoja. Hata nakumbuka nilishawahi kusafiri umbali mrefu
kucheza mechi na timu ya madrasat -Sinina ya Mbagala-Mangaya bila hata
wachezaji madarsa moja ya Mtoni Kijichi kutambua kama mimi mkristu.
Shekhe Gorogosi, naomba kumalizia kwa mfano mwingine kuwa Mbagala
wakati wa Ramadhani kunakuwa na ngoma ya kula
daku tukiwa watoto tulishiriki kuipiga na kuicheza ngoma hiyo na wakati
mwingine wengine tulikuwa vinyango na hata siku ya iddi tunaipiga na tunakusanya
pesa alafu tunagawana. Bila ugomvi na bila ya kujali dini ya wachezaji wa ngoma
ya hii. Nilimalizia kwa kumuhakikishia shekhe Gorogosi kuwa yale mahusiano
mazuri tuliyonayo majumbani kwetu ndiyo tunayajenga shuleni Ndanda pia.
Sherehe hiyo ilimalizika kwa vyeti vikatolewa, tukapiga picha na
tukala pilau vizuri na kupanda Lori letu kurudi Ndanda. Balaa huku ndani ya
Lori nikitaniwa sana kuwa Makwega leo kawa muisilamu, nikipewa majina mara Ali,
mara Jumaa, mara Mohammedi na wakinichagulia mchumba ambaye alikuwa dada mmoja
wa kidato cha sita ambaye alikariri mwaka huo kwani mwaka aliotakiwa kufanya
mtihani alipata shida ya ugonjwa ambaye alikuwa mzaliwa wa Lindi.Tulipofika
shuleni niliwauliza wenzangu (Wakatoliki) jamani mbona hamkushiriki mahafali ya
waisilamu? Nilibaini kuwa kumbe viongozi wa waislamu na wakatoliki waliotutangulia
yaani waliohitimu mei 1997 walikuwa na mambo yao binafsi tena si ya msingi
ambayo hayafai kusimuliwa yakayaingizwa katika vikundi vya dini. Tulilizungumza
hilo chini ya mwenyekiti wa wanafunzi wakatoliki shuleni Ndanda Robert Mtuya
ambaye alikuwa Mhehe wa Iringa Tosamaganga na namna nilivyookoa jahazi na tangu
hapo mashirikiano yalikuwa mazuri hadi tunamaliza shule hiyo mwaka1998.
Leo hii nalikumbuka tukio hilo kwa umuhimu wa maelewano ya dini na
dini. Natambua wapo leo ambapo ni Mapadri, wachungaji, masista, mashekhe katika
kundi hilo wakizishika imani zao vema. Pia nimeandika tukio hilo kama kumbuka
ya Shekhe Seleimani Gologosi alivyokuwa akiheshimu mahusiano mema ya dini moja
na zingine na leo hii ni miaka zaidi 12 tangu afariki dunia kiongozi hiyo
waisilamu nchini Tanzania Juni 26, 2009.
0717649257
Hakuna maoni
Chapisha Maoni