ZANZIBAR HAKUPIKIKI NA HAKULIKIKI,NI MATESO TU,POLISI WAHAHA KUVAMIA OFISI ZA CUF,SOMA HAPO KUJUA
![]() |
Askari wa Vikosi vya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar wakiwa katika moja ya poresheni zao |
MAKUNDI ya
askari wanaotajwa kama kutoka vikosi vya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar
wakichanganyika na vijana wasiokuwa na mafunzo halisi ya kiaskari wamekuwa
wakihaha kutaka kuvamia ofisi kuu za Chama cha Wananchi (CUF) mjini hapa. Anaandika Jabir Idrissa, Zanzibar … (endelea).
Uongozi
wa chama hicho umeikiambia Chanzo chengu kwamba baada ya askari hao wanaoitwa
kwa umaarufu kwa jina la “Mazombi,” kushindwa kuvamia ofisi za Makao Makuu
zilizoko mtaa wa Vuga, katikati ya Mji Mkongwe, juzi, jana usiku walijaribu
kuvamia Makao Makuu yaliyopo mtaa wa Mtendeni.
Taarifa
zilizotolewa na Ofisi ya Mkurugenzi wa Habari na Mawasiliano ya Umma wa CUF,
zimesema askari wengi walifika Mtendeni usiku wa manane na kuwateka walinzi
waliokuwa nje ya ofisi.
Walihangaika kutaka
kuwalazimisha kufungua mlango lakini waliwekewa ngumu kwa walinzi walioko nje
kusema hawana mamlaka hayo kwa kuwa wao walisema, “mamlaka yetu ni kulinda
nje.”
Mwandishi wa habari
hizi alifahamishwa kuwa mazombi waliokuwa wamebeba silaha za moto na za jadi,
mara kadhaa walisukuma mlango mkuu wa jengo la makao makuu bila ya mafanikio.
Waliamua kupayuka
wakitoa amri kwa walinzi waliokuwa ndani ya jengo kuwa wafungue au watavunja,
lakini hawakuzingatiwa.
Watu wanaoishi
jirani na makao makuu ya CUF, ambao walikuwa wakifuatilia kilichoitwa na baadhi
yao kama “sinema ya usiku” wamesema walishuhudia mazombi wakipiga kelele kutaka
wafunguliwe mlango.
“Niliwasikia
wanataka walioko ndani watoke watano watano, lakini kutokea ndani nikawa
nasikia mtu akisema hatoki mtu na atakayevunja na kuingia atakula naye sahani
moja,” amesema shuhuda.
“Nasema hatoki
mtu na atakayeingia ndani atakuwa mali yangu,” shuhuda amesema akimnukuu mtu
aliyekuwa ndani ya ofisi hizo.
Zogo lilitulia pale
walipofika askari wa kikosi cha kuzuia ghasia (FFU) ambao taarifa zinasema
waliamrishwa na IGP Ernest Mangu aliyepigiwa simu kutoka mjini hapa kuarifiwa
kuhusu tukio hilo.
Taarifa za ndani
zinasema IGP Mangu alichukua hatua baada ya kupata taarifa kutoka kwa uongozi
wa juu wa CUF kwa kuwa haukuamini kama wangepata msaada wa maana kwa Kamishna
wa Polisi Zanzibar (CPZ), Hamza Omar Makame.
Askari wa FFU walifika ndani ya magari mawili na kuharakia
kuwatimua. Mazombi walipobaini sauti za magari yakienda kwa kasi walipata hofu
na kuitana na kukubaliana kuondoka.
Siku mbili
zilizopita, mazombi ambao wamekuwa wakisababisha usumbufu kwa wananchi kwa
kuwavamia majumbani na kuwapiga, walikwenda ofisi za Vuga na kujaribu kuzivamia
waingie ndani, lakini hawakufanikiwa. Ofisi zote zinalindwa na walinzi wa chama
chenyewe, wakiwemo wenye mafunzo ya kijeshi kwa kuwa wapo waliofukuzwa kazi
vikosi vya serikali.
Taarifa hizi
zinakuja wakati ikifahamika kuwa askari hao walivamia ofisi kuu za Tume ya
Uchaguzi Zanzibar (ZEC) na kutapanya makaratasi waliyoyakuta.
Kwa mujibu wa
vyanzo vya habari, askari hao wamekuwa wakitafuta nyaraka zinazohusu matokeo ya
uchaguzi wa rais, lengo likihisiwa kuwa ni kuyapeleka kwa uongozi wa juu wa
CCM.
Kulikuwa na
taarifa kwa siku kadhaa kwamba CCM ilituma mawakala wake wa Idara ya Usalama wa
Taifa kisiwani Pemba ili kuwapata mawakala wa uchaguzi upande wa CUF na
kuwasainisha fomu za matokeo yasiyokuwa sahihi.
Chanzo cha
habari ndani ya Serikali na CCM kimesema baada ya kutofanikiwa kumpata hata
wakala mmoja, CCM ilifuta mpango wa kutaka kuchezea matokeo ili kulazimisha
Tume imtangaze Dk. Ali Mohamed Shein kuwa ndiye mshindi, na ikaagiza kutumika
kwa nguvu ambapo ndiyo akashuhudiwa Mwenyekiti wa ZEC, Jecha Salim Jecha
akitangaza taarifa ya kufuta uchaguzi akidai “umeharibika.”
Jecha ambaye amelalamikiwa kukimbia kazi kwa siku mbili
mfululizo, Oktoba 26 na 27, alitangaza Oktoba 28 kufutwa kwa uchaguzi wote
Zanzibar na kwamba utarejewa.
Wanaojua wanasema alichukuliwa kwa nguvu na kupelekwa Ofisi Kuu
za ZEC Maisara, mjini hapa, na kurekodiwa akisoma tamko linalotajwa kuwa
hakuliandika yeye wala ofisa yeyote wa Tume.
Tayari Mwenyekiti Jecha amerudi kazini lakini jana aliripotiwa
kuanza vibaya kikao na makamishna kwa kuwa alifanya ushawishi kuwa wamuunge
mkono kwa hoja yake hiyo ya kufuta uchaguzi.
“Unaloniuliza ni kweli. Alifika ofisini na kukutana na wenzake
lakini akaanza vibaya kwa kuwashawishi makamishna wamuunge mkono. Walimkatalia
kwa sababu wameshindwa kupata kifungu cha sheria cha kuridhia ufutaji wa
uchaguzi,” amesema mtoa taarifa ndani ya Tume ya Uchaguzi.
Wanasheria wametaka Jecha achukuliwe hatua za kisheria kwa
kuundiwa tume ya majaji kuchunguzwa kuhusu kitendo alichokifanya ambacho
wanaamini ni “uvunjaji wa katiba wenye kuashiria kusababisha machafuko nchini.”
Kadhia yote hii imetokana na kitendo cha Jecha aliyetoa tangazo
lake akiwa ameshatoa matokeo asilimia 70, siku ya mwisho akisubiriwa kumaliza
ili atangazwe mshindi wa urais.
Jumatatu ya Oktoba 26, Mgombea urais wa CUF, Maalim Seif Shariff
Hamad, aliwaambia waandishi wa habari kuwa mwelekeo wa kura ulionesha amepata
kura nyingi kiasi cha asilimia 52.87 dhidi ya 47.13 za Dk. Shein na kutaka Tume
isicheleweshe kutangaza matokeo.
Alisihi CCM wakubali na akamuomba Dk. Shein naye aridhie kama
alivyoridhia yeye mwaka 2010, kukubali matokeo ya kushindwa uchaguzi, ili
washirikiane kujenga nchi.
Kumekuwa na jitihada zinazoongozwa na Jumuiya ya Kimataifa hapa
kutaka kurejesha utaratibu wa kukamilisha kazi ya kujumuisha na kutangaza
matokeo ya kura zilizobaki katika majimbo 22, baada ya majimbo 32 kutangazwa
tayari na Jecha mwenyewe kupitia kituo cha utangazaji wa matokeo
kilichofadhiliwa na ofisi ya Umoja wa Mataifa nchini Tanzania.
Habari hii kwahisani ya Mwanahalisi Oline
No comments
Post a Comment