MANENO YA MKURUGENZI WA THE GUARDIAN LTD KUHUSU KIFO CHA MWANDISHI MPOKI BUKUKU
Leo, kama ilivyo kwa wengine wengi, nimepokea kwa mshtuko
mkubwa na kutoamini, kuhusiana na kifo cha ghafla cha mmoja wa
wapigapicha waandamizi wa The Guardian Limited, Bw. Mpoki Bukuku (44),
aliyefariki asubuhi kwenye Hospitali ya Taifa Muhimbili.
Kwa familia yake, wamempoteza baba, mume na zaidi ya yote
rafiki wa kweli, lakini kwetu sisi The Guardian Limited, tumempoteza pia
rafiki wa kweli na nguzo katika tasnia ya uandishi wa habari.
Bukuku alikuwa ni mwanadamu tu kama ilivyo kwa yeyote
kati yetu, lakini katika uandishi wa habari, alikuwa ni mtu aliyeipenda
fani yake na hakuogopa kupambana alimradi apate habari nzuri. Ni kwa
sababu hiyo ndiyo maana kuna wakati kiu yake ya kupata habari nzuri
kuliko wengine wote ilimuweka matatani.
Wale wanaoelewa uandishi wa habari wa picha watabaini
kwamba ujasiri na kuipenda kazi ni sifa kuu mbili za kila mpigapicha ili
kupata habari nzuri na yenye nguvu. Bukuku alikuwa na sifa zote hizo
mbili. Alikuwa shujaa na mwenye mapenzi na kazi yake hasa wakati
akifuatilia habari kubwa kokote kule katika nchi hii.
Alipigwa na hata kuteswa na maadui wa uhuru wa vyombo vya
habari, lakini bado mahaba yake katika kufanikisha habari bora
hayakuzimwa. Alikuwa ni mwandishi wa habari siyo kwa bahati mbaya, bali
ni kwa kuchagua na ndiyo maana alikuwa na mapenzi wakati akitimiza
wajibu wake wa kutekeleza kazi mbalimbali za kihabari alizopangiwa na
wahariri wake.
Bukuku amemaliza safari yake duniani, kimwili hayuko nasi lakini kiroho na kiuweledi, mara zote atakuwa nasi daima.
Sisi katika Kampuni ya The Guardian Limited tunaungana na
famila, ndugu na marafiki katika kippindi hiki kigumu, kuombeleza msiba
wa mtu ambaye tumekuwa tukifanya naye kazi kwa miaka mingi. Kampuni
itaiunga mkono kwa ukamilifu familia ya marehemu Bukuku.
Kwa niaba ya wafanyakazi wote wa The Guardian Limited, kwa
heshima kubwa natoa salamu zangu za rambirambi kwa mjane wa Bukuku,
Lucy, watoto na wadau wote wa tasnia ya habari nchini Tanzania, kwa kifo
cha ghafla na kushtua cha mmoja wetu.
Richard Mgamba
Mkurugenzi Mtendaji,
The Guardian Limited
Desemba 23, 2016