MAKUMBUSHO YA VITA VYA MAJIMAJI KIELELEZO CHA UZALENDO NA URITHI WA TAIFA
Na Saidi Lufune – Ruvuma
Tamasha la kumbukizi ya vita vya majimaji ni urithi adhimu na wa kihistoria kwa Watanzania, Mhifafhi Mambo ya Kale Mwandamizi wa Wizara ya Maliasili na Utalii Bi. Rahel Kisusi amesema.
Akizungumza leo Februari 25,2025 mkoani Ruvuma ameeleza kuwa kumbukizi hiyo ni fursa kwa Watanzania na dunia kutafakari mchango mkubwa uliotolewa na mashujaa wazalendo katika kupigania utu na heshima ya Watanzania.
“Vita vya Majimaji ni moja ya kumbukumbu muhimu katika historia ya mapambano ya ukombozi wa bara la Afrika dhidi ya ukoloni, Mashujaa wetu walipigana kwa dhamira thabiti wakitetea uhuru, mila, utambulisho na rasilimali za Taifa letu dhidi ya ukandamizaji wa wakoloni wa Kijerumani” Amesema Kisusi
Kwa kuzingatia kauli Mbiu ya mwaka huu “Makumbusho ya Majimaji na Malikale zetu, kwa Maendeleo ya Utalii na Uchumi”. Bi. Rahel, amewataka Watanzania kutafakari jinsi historia na urithi wetu wa kihistoria unavyoweza kutumika kama chachu ya maendeleo ya utalii na Uchumi na kuongeza kuwa, Makumbusho ya Majimaji, pamoja na Malikale nyingine zilizopo nchini, ni hazina kubwa ya maarifa na vivutio muhimu vya utalii wa kihistoria.
"Kwa kuitangaza na kuwekeza katika maeneo haya, tunaunda fursa za kiuchumi kupitia utalii wa ndani na wa kimataifa. Hivyo, sekta ya utalii wa urithi wa malikale unaweza kuwa chanzo kikubwa cha mapato, ajira na maendeleo ya jamii zinazozunguka maeneo haya". Aliongeza Bi. Kisusi
Katika hatua nyingine Bi. Kisusi alieleza kuwa, Serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii, inaendelea na mikakati mbalimbali kuhakikisha Malikale na historia nchini zinatumika kwa maendeleo ya utalii na Uchumi wa Taifa.
“Wizara inaendelea kuchukua hatua Madhubuti zikiwemo kuimarisha uhifadhi na uendelezaji wa makumbusho na maeneo ya kihistoria; kushirikiana na sekta binafsi na wadau mbalimbali wa maendeleo; kuhamasisha tafiti na elimu kuhusu vita vya Majimaji na historia nyingine muhimu; na kuongeza juhudi za utangazaji wa maeneo ya kihistoria kama vivutio vya utalii.” Alisisitiza Bi. KisusiKwa upande wake Kaimu Mhifadhi Mkuu wa Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Makumbusho ya Taifa Bi. Frola Vicent, amesema tangu kuanza kwa tamasha hilo la Maadhimisho ya Vita vya Majimaji katika Mkoa huo, mwitikio wa wananchi umeendelea kuwa mkubwa kila mwaka kutokana na ushirikishwaji wa moja kwa moja wa wazee wa kimila na Machifu wa Makabila ya Kusini mwa Tanzania, kwa kuwa vita hivyo vilishirikisha viongozi wa kimila, machifu na matumizi ya silaha za jadi wakati wa vita.
"Awali midahalo hii ilikua inafanyika katika eneo moja tu, tofauti na sasa ambapo umekuwa ukifanyika katika kila Wilaya za Mkoa wa Ruvuma, ambapo mwaka 2024 ulifanyika Wilayani Nyasa, na leo tupo hapa Wilayani Namtumb. Lengo likiwa ni kuwajengea uwelewa wananchi juu ya maana halisi ya ya vita ya Majimaji na kujenga uzalendo juu ya kutembelea Makumbusho ya Majimaji kama sehemu ya kujifunza, kufahamu historia ya nchi husausan kwa wanafunzi ambao ndio Taifa la baadae” Amesema Bi. Frola
Wakizungumza wakati wa mdahalo huo baadhi ya wananchi na wanafunzi walioshiriki katika majadiliano, wamesema wamejifunza mengi kupitia mada mbalimbali ambazo ziliwasilishwa katika mdahalo huo sambamba na kupongeza juhudi zinazofanywa na serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii, zikiwemo uboreshaji wa miundombinu katika vivutio vya kihistoria na katika Makumbusho ya Majimaji
Hakuna maoni
Chapisha Maoni