BASATA YAPIGA MARUFUKU DISKO TOTO
Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA)
ambalo ni msimamizi wa sekta ya Sanaa na burudani nchini linawakumbusha
wamiliki na waendeshaji wa kumbi za burudani kufuata sheria, kanuni na
taratibu walizopewa kwenye vibali vyao vya uendeshaji wa kumbi.
Wanaelekezwa kuhakikisha wanakuwa
na vibali halali vya uendeshaji wa kumbi zao, kuzingatia muda wa
utumizi wa kumbi, kuepuka kelele zinazosumbua kwenye maeneo maalum hasa
makazi ya watu na kuhakikisha ulinzi na usalama wa maisha ya watu na
mali zao.
Aidha, BASATA linawakumbusha
wamiliki wote wa kumbi za sherehe na burudani kwamba ni marufuku
kukusanya watoto katika kumbi zao kupitia kile kinachoitwa ‘Disko Toto’
katika msimu huu wa Sikukuu ya Christmas na Mwakampya ili kuepuka maafa
yanayoweza kujitokeza.
Uzoefu unaonesha kwamba, nyakati
za sikukuu kama hizi wamiliki wa kumbi wamekuwa wakijisahau na kuandaa
madisko ya watoto hali mbayo imekuwa ikisababisha maafa ambayo
yangeepukika kwa kufuata sheria, kanuni na taratibu.
Aidha, baadhi ya wamiliki na
waendeshaji wa kumbi wamekuwa wakijisahau na kuendekeza faida pasi na
kujali maelekezo ya vibali vyao wamekuwa wakijaza watu kupita viwango
vya madaraja waliyopangiwa na BASATA.
BASATA kama mtoaji wa vibali vya
kumbi za sherehe na burudani linasisistiza kwamba halitafumbia macho
ukumbi wowote utakaokiuka maelekezo haya sambamba na kuruhusu maonesho
machafu yenye kudhalilisha utu wa binadamu hasa yale yanayoonesha maungo
ya ndani. Hatua kali na za kisheria zitachukuliwa kwa yeyote
atakayekiuka maagizo haya.
BASATA linawatakia wasanii na wadau wote wa Sanaa Heli ya Christmas na Mwakampya