Zinazobamba

WAISLAMU TANZANIA WATAKIWA KUACHA KUSHEHEREKEA SIKUKUU ZA MWAKA MPYA NA KRISMAS

Amiri wa Baraza Kuu la Jumuiya na Taasisi za Kiislamu nchini, Sheikh Mussa Kundecha amewataka vyombo vya habari vya Kiislamu kuelimisha jamii kuhusu uharamu wa sherehe za mwaka mpya usio wa Kiislamu na Chrismass.

Wakati wasiokuwa Waislamu wakijiandaa kusherehekea sikukuu za mwisho wa mwaka, yaani Krismas na mwaka mpya, masheikh na viongozi wa dini nchini wamewataka Waislamu kuepuka kushiriki katika sherehe hizo kwani zinaenda kinyume na misingi ya Uislamu. Badala yake, Waislamu wametakiwa kutumia fursa hiyo kujifanyia tathmini ya amali walizozitenda mbele ya Mwenyezi Mungu. 

Wakizungumza na gazeti la wiki, kwa nyakati tofauti masheikh na viongozi hao wa dini wamesema ni vema Waislamu watumie wakati huu kujitafakari kwa makini na kuangalia ni namna gani wataweza kusawazisha makosa yao, kuzidisha ibada pamoja na kufanya toba badala ya kujiingiza kwenye uovu na sherehe za maasi. 

Mmoja wa wanazuoni hao ni Sheikh Jabir Katura kutoka Mwanza ambaye amebainisha wazi kuwa ni haramu na pia haifai kwa Muislamu kusherehekea mwaka mpya usio wa Kiislamu au sherehe yeyote inayokwenda kinyume na mila ya Kiislamu.

 Sheikh Katura aliendelea kusema si katika mafundisho ya Uislamu kusherehekea Krismas au mwaka mpya kwani ni sherehe zimefungamanishwa na ibada na kuabudu ndiko kunakotofautisha misingi ya dini za watu.

 Aidha, mwanazuoni huyo alionekana kusikitishwa na hali mbaya za kimaadili kwa Waislamu wengi waishio vijijini hivyo kutaka kuwepo juhudi za makusudi za kuwalingania Waislamu kuhusiana na kadhia hiyo. 
“Waislamu wengi huko vijijini ndiyo ambao kwa kiasi kikubwa wanaojitumbukiza kwenye sherehe hizi bila kujua kuwa wanachofanya ni makosa.
Naye Amiri wa Baraza Kuu la Jumuiya na Taasisi za Kiislamu nchini, Sheikh Mussa Kundecha, amevitaka vyombo vya habari vya Kiislamu kuwa mstari wa mbele katika kuwaelimisha Waislamu juu uharamu wa sherehe hizo.