SAKATA LA POMBE ASKOFU MKUU KANISA LA KKKT AFUNGUKA
ASKOFU Mkuu wa zamani wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheli Tanzania (KKKT), Dk. Alex Malasusa, amebariki rasmi unywaji wa pombe katika kanisa hilo kongwe nchini, anaripoti Mwandishi Wetu.
Akizungumza katika mkutano wa 33 wa Dayosisi ya Mashariki na Pwani, wiki iliyopita, huko Seminari ya Kisarawe, mkoani Pwani, Askofu Malasusa amesema, ” katazo la unywaji wa pombe lililetwa na wamisionari, lakini pombe kama pombe haina tatizo.”
Askofu Dk. Malasusa, ndiye askofu mkuu wa kanisa la KKKT, Dayosisi ya Mashariki na Pwani.
Askofu Dk. Malasusa alikuwa akikamilisha majibu yaliyotolewa na
Askofu Keshomshahara wa kanisa hilo, Dayosisi ya Bukoba aliyoyatoa kwa
swali lilioulizwa na Prof. Mjema wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Katika swali lake, Prof. Mjema alihoji, nafasi ya pombe katika dhana
ya Mtume Paulo anapozungumzia kutiwa unajisi kwa vyakula na vinywaji
wanavyokunywa wakristo.
Alitaka kupata ufafanuzi wa msiamo wa kanisa juu ya msemo wa “kimuingiacho mtu na kimtokacho mtu.”
Awali katika majibu yake, Askofu Keshomshahara amesema, “pombe ni
kinywaji tu kama vinywaji na vyakula vingine” na kwamba pombe inapaswa
kutumiwa kwa kiasi na kwamba “hata sakramenti takatifu ya Meza ya Bwana
inayotumika kanisani mwao ni pombe.”
Baada ya majibu hayo, ndipo Askofu Dk. Malasusa aliposisitiza kuwa
makatazo ya pombe kanisani ni “busara ya wamisionari wa kwanza walioleta
injili Afrika baada ya kuona Waafrika walikuwa wakilewa bila kiasi na
kukosa ustaarabu.”
Aliendelea kusisitiza kuwa “pombe itumike kwa kiasi na hasa kwa wakristo wachanga.”
Majibu hayo ya maaskofu yaliwachanganya wajumbe wengi na kusababisha mijadala baada ya mkutano.
Mjumbe mmoja aliyeongea na gazeti hili huku machozi yakimlenga
anasema, “nimesikitika sana kuona maaskofu wetu wanalipotosha kanisa.
Hivi kweli sakramenti ni pombe?”
Dayosisi ya Mashariki na Pwani kupitia katiba yake, inapiga marufuku wazee wa kanisa kutomiliki vitega uchumi vinavyouza pombe.
Aidha, sherehe zote za kanisa haziruhusiwi kuwa na pombe huku baadhi
ya waumini wakipewa adhabu na wachungaji wao kwa kunywa pombe au kufanya
biashara ya pombe.
Msimamo wa maaskofu hawa wawili unaliweka kanisa Zima la KKKT katika
njiapanda ya kulifafanua jambo hili huku waumini wengi wakitishia
kuhamia makanisa ya kiroho kukimbia upotoshaji wa wazi wa maakofu wa
KKKT.
Mkutano huo wa 33 ulijaa vitimbi vingi vinavyoonyesha dayosisi hiyo haiko shwari.
Akiongea kwa uchungu kwenye mkutano huo, Mchungaji wa kanisa hilo
usharika wa Kigogo, jijini Dar es Salaam, Richard Ananja alimtaka Askofu
Dk. Malasusa kuachia kiti mara moja kwa kuwa amepoteza sifa kwa kashfa
za ngono zinazomkabili.
Amesema Dk. Malasusa anakabiliwa na tuhuma nzito za matumizi ya
madaraka, uvujaji wa fedha za dayosisi, hujuma kwa Benki ya Maendeleo,
kugushi vyeti ya elimu, ukabila, chuki na visasi kwa wachungaji.
Hivyo basi, ili kulinda hadhi na heshima ya kanisa na yeye binafsi,
ni vema Askofu Malasusa “akaachia ngazi kwa hiari, badala ya kusuburi
kufukuzwa.”
Hoja hiyo ilipozwa na katibu mkuu wa Dayosisi hiyo, Godfrey Nkini aliyedai kuwa kamati ya maadili inashughulikia tuhuma hizo.
Siku moja kabla ya kufungwa kwa mkutano, mchungaji wa kanisa la KKKT,
Usharika wa Kibaha, Amani Lyimo katika mahubiri ya ibada ya asubuhi,
aliushambulia utendaji wa Askofu Dk. Malasusa kuwa ni wa uonevu, usijali
kweli, uliojaa udhalimu, ubabe na matumizi mabaya ya madaraka.
Amesema uongozi wa Dk. Askofu Malasusa unakomoa watu kuliko uongozi wowote uliopita katika dayosisi hiyo.
Kabla ya kufungwa kwa mkutano huo, Mwenyekiti wa kamati ya maadili wa
dayosisi hiyo, Ibrahim Kaduma, alidai kuwa tuhuma juu ya Askofu Dk.
Malasusa, si za kweli na zinachochewa na gazeti moja (hakulitaja) lakini
akadai ni chuki ya uislamu dhidi ya kanisa.
Maelezo hayo yalipingwa na wachungaji wengi hali inayoonyesha kuwa Askofu Malasusa hayuko vizuri na wachungaji wake.
Wachungaji walidai kamati imeleta “majibu mepesi” kwa tuhuma za ngono
zinazomkabili Dk. Malasusa na kwamba kinachobakia sasa wao kumwaga
hadharani yaliyositiriwa kulilinda kanisa, alisisitiza mmoja wa
wachungaji wa kanisa hilo mwenye taaluma ya sheria.
Katika hatua nyingine, ajenda ya marekebisho ya katiba ya dayosisi
hiyo, iliburuzwa ili kumwepusha Askofu Malasusa na hoja ya ukomo wa
madaraka yake.
Siku za karibuni, Askofu Dk. Malasusa amekumbwa na tuhuma mfululizo, zikiwamo matumizi mabaya ya madaraka, ngono na ubaguzi.
Hata hivyo, Dk. Malasusa amekuwa akijibu tuhuma hizo kwa kuwanyooshea
kidole waumini wanaotoka mikoa ya Kaskazini kuwa wanamsakama kwa vile
katika uchaguzi mkuu uliyopita, limuunga mkono Rais Magufuli na
kumsaliti swahiba wake wa miaka mingi, Edward Lowassa.
Source mwanahalisionline