Zinazobamba

DADA KULEMBWA NA KAKA, HII NI TABIA GANI

Naingia uwanjani, swali kukuulizeni.
Nimetoka kijijini, mjini mie mgeni.
Niyaonayo machoni, nashangaa kulikoni!.
Dada kulembwa na kaka hii ni tabia gani?.

Ukipita mitaani, ya hapa kote mjini. 
Pale Mwenge madukani, makumbusho kituoni.
Dada kakunja gauni, anaoshwa miguuni.
Dada kulembwa na kaka, hii ni tabia gani?.

Wavulana wa mjini, wameona hii fani.
Elimu si ya shuleni, ujanja wa mitaani.
Hupita barabarani, na kapu lake kwapani.
Dada kulembwa na kaka, hii ni tabia gani?.

Dada zangu jamani, naomba nikuulizeni.
Umetokaje nyumbani, na uchafu miguuni.
Uje oshwa hadharani, na yule kaka fulani.
Dada kulembwa na kaka, hii ni tabia gani?.

Huu ni ulimbukeni, kuiga mambo mageni.
Wala si utamaduni, wahapa kwetu nchini.
Mnajishusha thamani, kuchezewa maungoni.
Dada kulembwa na kaka, hii ni tabia gani?.

Kushikana mapajani, haya ni mambo ya ndani.
Mwayafanya hadharani, mmekuwa kama nyani!.
Wakaka wakusemeni, mwawapa mambo fulani.
Dada kulembwa na kaka, hii ni tabia gani?.

Ukisharudi nyumbani, kwa wako baba fulani.
Akuita wangu hani, njoo huku kitandani.
Wamfanyia kisilani, kama simba wa mwituni.
Dada kulembwa na kaka, hii ni tabia gani?.

Na wewe baba fulani, hii ni tabia gani?.
Unapoenda saluni, kuoshwa na Dada Jeni.
Asugua kidevuni, vidole masikioni.
Dada kulembwa na kaka, hii ni tabia gani?.

Tena we baba fulani, unawekwa mtegoni.
Akusugua shingoni, kichwa kipo kifuani.
Waisifu yake fani, na chenji wampa Jeni.
Dada kulembwa na kaka, hii ni tabia gani?.

Hizo Dawa za saluni, hebu ziweke nyumbani.
Mwambie mama Fulani, nisugue wangu hani.
Nimetokea saluni, nitoe taka usoni.
Dada kulembwa na kaka, hii ni tabia gani?.

Nimefikia mwishoni, kalamu naweka chini.
Ninarudi kijijini, kaeni nyie mjini.
Kushuhudia uhuni, nisije pazwa mbinguni.
Dada kulembwa na kaka, hii ni tabia gani?.

Hakuna maoni