Zinazobamba

WAMACHINGA KARIAKOO WATAKIWA KUSHIKAMANA ILI KUFIKIA MALENGO YAO KIUCHUMI


Na Mussa Augustine

Mwenyekiti  wa Chama Cha wafanayabiashara wadogo( Wamachinga)Mkoa wa Dar es salaam( KAWASO) Stevin Lusinde amewasihi Wanachama wa Chama hicho kushikamana , Kupendana na kua kitu kimoja katika kuendeleza maendeleo yaliyofikiwa na chama hicho mpaka sasa.

Lusinde ametoa nasaha hizo hivi karibuni katika Mkutano Mkuu wa Kikatiba wa chama hicho ulifanyika katika Ukumbi wa Sabasaba jijini Dar es salaam nakubainisha kuwa kuna baadhi ya Wanachama wa KAWASO wameanza kutumika vibaya na baadhi ya wanasiasa wenye nia ovu kuwachafua viongozi wa KAWASO kwa maslahi yao binafsi hivyo amewasihi kuwapuuza watu hao nakuomba wawe kitu kimoja kuendeleza KAWASO ambayo imeanza kupata mafanikio makubwa kwa sasa tangu 2017 ilipoanzishwa.

"Tushirikiane kujenga kawaso yetu, sisi tumetoka katika mazingira ambayo hayaeleweki kabisa,lakini kwasasa tulipotoka,tulipo na tunakoelekea tumepiga hatua kubwa za mafanikio tusikubali kufarakanishwa na watu ambao wanataka maslahi yao binafsi"amesisitiza Lusinde 

Amesema kuwa Maisha ya Wamachinga wa kariakoo yapo mikononi mwao hivyo wakikosea kuwasikiliza wale wanaotaka kubomoa chama chao watakua wameshindwa kupata fursa zao za kimaendeleo ambazo kwa sasa zimeanza kujitokeza chini ya uongozi wa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan

Lusinde kupitia Mkutano huo ametangaza kua Mkutano maalumu wa uchaguzi wa Viongozi wa KAWASO utafanyika April 19 , 2024 huku akiwasisitiza wanachama kuchagua viongozi wenye maono ya kukifikisha mbali chama hicho.

"Viongozi ambao watachaguliwa tarehe 19 wawe ambao kauli yao ya pamoja ni kutengeneza kariakoo ya pamoja,kariakoo ya upendo,Mshikamano,na kufikia ndoto za maendeleo yetu" amesema Lusinde.

Awali akisoma taarifa ya mafanikio na changamoto tangu kuanzishwa kwa KAWASO  Mwenyekiti wa KAWASO Namoto Yusuph Namoto amesema mpaka sasa Chama hicho kimepata mafanikio makubwa licha ya baadhi ya watu wanaobeza mafanikio hayo.

Amesema KAWASO imefanikiwa katika mambo mbalimbali ikiwemo kuondoa migogoro kati ya Machinga na uongozi wa halmashauri ya wilaya, kua na kanzi data ya kuwatambua wamachinga, kupata vitambulisho vya NIDA na TRA , kupata mikopo ya mitaji na viwanja kutoka taasisi za kifedha ikiwemo Benki ya Maendeleo, pamoja na kuhakikisha utunzaji wa mazingira unatekelezwa ipasavyo.

Namoto pia amesema mafanikio yamekua mengi lakini changamoto kubwa inayoikabili chama hicho ni kukosekana kwa vyanzo vya mapato, ambapo amewashauri wanachama washikamane kuanzisha vyanzo hivyo akitolea mfano SACCOS ili kusaidia kujiwezesha wenyewe kupata mikopo bila riba.
Katika hatua nyingine Namoto amewasisitiza wamachinga kumuunga mkono rais Dkt Samia Suluhu Hassan kulinda amani na kuacha kutumika na watu wenye nia ovu ya kuvunja amani ya Taifa la Tanzania ambalo linasifika kwa tunu za Amani, Mshikamano na Upendo.

" Sisi haya ndio maisha yetu, tuache kutumika vibaya wale wanaotaka tuvunje amani yetu hatuko tayari kufanya hivo, tumekua tukifanya makongamano ya amani katika moja ya mafanikio yetu mfano tarehe 25, 10, 2023 tulifanya pale viwanja vya mashujaa ikiwa lengo ni kuunga mkono serikali ya Dkt Samia ambaye anapenda maridhiano na sio machafuko kwenye taifa letu.

Mkutano huo umehudhuriwa na wanachama zaidi ya elfu mbili(2000) huku wanachama  hao wakionyesha kuwa na matumaini makubwa na uongozi uliopo baada ya kuzungumza na chombo hiki cha habari kwa nyakati tofauti.

Hakuna maoni