Makamu Mwenyekiti Bara wa Chama cha ACT Wazalendo Isihaka Mchinjita, akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.

NA MWANDISHI WETU

CHAMA cha ACT Wazalendo kusikitishwa na mwenendo usioridhisha wa chaguzi za marudio zilizofanyika mara sita tangu Serikali ya Awamu ya Sita iingie madarakani mwaka 2021. 

Hayo yamebainishwa leo Machi 24 na Makamu Mwenyekiti Bara wa Chama hicho Isihaka Mchinjita, akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.

Mchinjita amesema kuwa katika chaguzi zote za marudio zilizofanyika ni wazi kwamba hakuna tofauti hata ya msingi katika kuendesha na kusimamia uchaguzi.

"Mfano hivi karibuni Tume ya Taifa ya Uchaguzi iliitisha uchaguzi wa marudio wa Udiwani uliofanyika kwenye Kata 23 siku ya tarehe 20 Machi, 2024. Chama cha ACT Wazalendo kilisimamisha wagombea kwenye Kata 6 (Chipuputa, Wilaya ya Nanyumbu; Kabwe, Wilaya ya Nkasi; Kasingirima, Manispaa ya Kigoma Ujiji; Mlanzi; Wilaya ya Kibiti, Kamwene; Wilaya ya Mlimba na Bukundi Wilaya ya Meatu)," amesema Mchinjita na kuongeza,

"Kwa matokeo tuliyokusanya, licha ya hujuma mbalimbali zilizofanyika kabla ya uchaguzi, Chama cha ACT Wazalendo kilistahili kushinda kwenye Kata tatu za Kasingirima  (Kigoma), Kabwe (Nkasi Kaskazini) na Chipuputa (Nanyumbu). Hata hivyo, Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ambayo ndio yenye dhamana ya kuhakikisha kuwa uchaguzi unakuwa huru wa haki na wa kuaminika (free, fair and credible), imeshirikiana na Chama cha Mapinduzi (CCM) kuhakikisha kuwa CCM inatangazwa kushinda kwenye Kata zote,".

Mchinjita ameeleza kuwa kupitia chaguzi hizi za marudio wamejiridhisha kuwa licha ya kauli za kufungua ukurasa mpya wa siasa za kistaarabu kupitia falsafa ya Rais Samia Suluhu Hassan ya 4R, hali halisi kupitia chaguzi za marudio ni tofauti. 

Kwamba vitendo vyote vya kiharamia na wizi wa kura vilivyofanyika kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020 vinaendelea kufanyika kupitia chaguzi za marudio.

Ameainisha mapungufu yaliyokuwepo kwenye uchaguzi huo wa Machi 20 mwaka huu ambayo ni pamoja na Polisi kutumia mabavu kukamata viongozi wa ACT Wazalendo ambapo amedai kuwa tukio hilo limefanyika Halmashauri ya Kigoma Ujiji kwenye Kata ya Kasingirima. 

Kwamba Viongozi waliokamatwa kwa kuzuia kura feki zisidumbukizwe kwenye masanduku ni Abdul Nondo  (Mwenyekiti wa Ngome ya Vijana Taifa, Karama Kaila (Mjumbe wa Kamati Kuu Kanda ya Magharibi), Alhaj Selemani Simba (Mwenyekiti wa Ngome ya Wazee Mkoa wa Kigoma), Alumbula Khalidi aliyekuwa Mgombea Udiwani Kata ya Kasingirima, na Wanachama Ntakije Ntanena na Ndugu Khamis Mzungu.

Mapungufu mengine ni Tume ya Taifa ya Uchaguzi kugawa karatasi za kupigia kura kwa makada wa CCM ili wazitumbukiza kwenye masanduku ya kura ambapo amaedai jambo hilo limefanyika kwenye Kata zote zilizorudia uchaguzi. Jitihada za viongozi wa ACT Wazalendo kuripoti suala hilo kwa Maafisa wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi halikusaidia kitu kwani hakuna hatua yoyote iliyochukuliwa. Pia, viongozi waliojaribu kuwadhibiti makada wa CCM kutumbukiza kura hizo kwenye masanduku walikutana na mkono wa chuma wa Jeshi la Polisi.

Mengine ni Viongozi wa ACT Wazalendo kutekwa na kuteswa na Jeshi la Polisi au  vikundi vya Chama cha Mapinduzi, kwamba hilo limejitokeza kata ya Kabwe ambapo Katibu wa Chama mkoa Januari Yamsebo alitekwa na vikundi vya vijana wa CCM. Vilevile, Mgombea wa Udiwani wa kata ya Bukundi  Paulin Richard Mayila alitekwa, kuteswa na kupora fedha taslimu kiasi cha shilingi 350,000 na kwenda  kutupwa katika milima ya Bukundi.

Kwamba wasimamizi wa Uchaguzi kubadilisha matokeo kwa kuongeza au kubadili namba kwenye fomu zote za matokeo na hilo limefanyika kwenye Kata ya Kabwe Jimbo la Nkasi Kaskazini.