Watoto waelezwa umuhimu wa baba
NA ABRAHAM NTAMBARA
JESHI la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limeadhimisha Siku ya Baba Duniani kwa kuandaa na kushiriki chakula cha mchana na watoto yatima na wanaoishi katika mazingira magumu zaidi ya 200.
Akizungumzia na waandishi wa habari katika hafla hiyo jana jijini Dar es Salaam, Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam ACP Muliro Jumanne Muliro alisema Siku hiyo ni Maalum kwao.
“Sisi kwa Kanda Maalum leo (jana) ni Siku Maalum sana, tumeona tuwe karibu na watoto yatima na wengine wanaoishi katika mazingira magumu,” alisema ACP Muliro.
Kamanda Muliro alieleza kwamba wamefuatilia wakati wa utekelezaji wa majukumu yao na kubaini kwamba watu ambao wamekuwa wakifanya vitendo wa kikatili na uhalifu wamekuwa wakieleza kwamba hawana baba wala mama.
Hivyo kama Jeshi la Polisi wameona kwamba sio kweli kwamba hawana wazazi kwa sababu hata wao ni baba na mama, kwamba wanastahili kuwa wazazi wao.
Alisema kwamba watoto hao wamekuwa wakijiingiza katika vitendo vya uhalifu kwa sababu ya kukosa misngi bora ya malezi ya kikatiba na Sheria za kimataifa.
“Watoto wanahitaji Elimu, kuishi na chakula, hizi ni haki za msingi, kwahiyo unakuta mtoto anakwambia sasa mimi nitafanya mini lazima nike, hivyo analazimika kuiba,” alisema ACP Muliro.
ACP Muliro alisisitiza kwamba Jeshi la Polisi limeguswa wao kama Binadamu kutokana na hali wanayokutana nayo wakati wakifanya uchunguzi.
Hivyo kwa kutumia Mishahara yao wakaamua kuchanga fedha zao ili kuandaa chakula na kushiriki na watoto hao ili kuonyesha hisia zao za kuwa karibu na jamii.
“Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam linaunga mkono watu wanaojitolea kuwalea watoto hawa, linaunga mkono watu wengine ambao ni kina baba na kina mama wa Tanzania wapate hisi kwamba kwa mtazamo wa Jeshi watoto hawa Wana wazazi. Kila baba na mama wa kitanzania anao wajibu wa kuwalea,” alisema ACP Muliro.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Sauti ya Yatima Tanzania Mariamu Saada alilishukuru Jeshi la Polisi kwa kuweza kushiriki nao chakula cha mchana.
“Ukweli sisi tunasema asante, wameonesha moyo mkubwa sana, hivyo tunaamini kwa sasa jamii inaweza kujifunza kwa Polisi,” alisema Saada.
Alitoa wito kwa Watanzania wote kuwa walezi wa watoto yatima na wanaoishi katika mazingira magumu ili kuwapa furaha kama watoto wengine.
Alisema anaamini kila Mtanzania akiamua kulea na kuishi naye mtoto yatima mmoja, hakuna atakayeishi kituoni nchini.

No comments
Post a Comment