SIKU 100 ZA DKT.SAMIA,KATA YA KIWALANI YAPIGA HATUA KUBWA KIMAENDELEO.
Kata ya Kiwalani Jijini Dar es salaam,imepiga hatua kubwa za maendeleo katika sekta mbalimbali ikiwemo Miundombinu,Afya,Elimu, Biashara pamoja na Ulinzi shirikishi ikiwa ni utekelezaji wa siku miamoja za uongozi wa Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan.
Hayo yamesemwa hivi karibuni na Diwani wa Kata hiyo,Mh.Idd Burah wakati akizungumza na waandishi wa habari Ofisini kwake nakubainisha kwamba suala la ulinzi shirikishi Mtaa wa Yombo ambao awali ulikuwa na changamoto kutokana na mfumo wa zamani kutokua rafiki kwa wananchi,hivyo umefanyiwa maboresho kwa kuanzishwa mfumo mpya unaoendana na mitaa mingine.
"Kwa sasa wananchi wanachangia huduma za ulinzi shirikishi kwa njia rasmi kupitia risiti za kawaida,hali iliyosaidia kuondoa malalamiko na kuongeza uwazi,mfumo huu mpya umekuwa nafuu na unakubalika kwa wananchi wa mtaa huo"amesema Diwani Burah
Kuhusu miundombinu,Diwani huyo amesema barabara ya Relini hadi Matangini ambayo imekuwa korofi kwa muda mrefu,tayari ukarabati wake umeanza kwa kutumia greda ili kuhakikisha inapitika kwa urahisi na kuboresha shughuli za usafiri na biashara.
Aidha amemshukuru Rais Dkt. Samia kwa kuwezesha utekelezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo katika Kata ya Kiwalani,nakuongeza kuwa katika mpango wa muda mfupi kila barabara za mtaa zitawekewa lami,jambo litakaloboresha taswira ya kata hiyo na kuinua maisha ya wananchi.
Kwa upande wa Sekta ya afya,amesema kituo cha afya cha Kiwalani kimekamilika kwa asilimia 99,huku changamoto iliyobaki ikiwa ni miundombinu ya vyoo,nakwamba Mkurugenzi wa Jiji la Dar es salaam Elihuruma Mabelya ameahidi marekebisho hayo kufanyika mwaka huu ili kituo hicho chenye vifaa vya kisasa vilivyotolewa kwa uwezeshaji wa Rais Dkt.Samia kianze kutoa huduma.
Akizungumzia sekta ya elimu na biashara, Mh.Burah amesema takwimu zinaonesha ufaulu umeongezeka ikilinganishwa na mwaka jana,huku uongozi wa kata ukijipanga kuongeza mapato kupitia masoko ya Bomubomu na Kigilagila.
"Kata ya Kiwalani tumejipanga katika kila sekta kuhakikisha inapiga hatua za kisasa kwa maendeleo ya wananchi'amesisitiza Diwani huyo.


No comments
Post a Comment