Zinazobamba

TGNP yawakutanisha wakazi wa kata ya Mzinga kujadili changamoto za Hedhi kwa watoto wa kike.

Na Vicent Macha

TGNP kwa kushirikiana na wanaharakati wa ngazi ya jamii imeendesha mdaharo kuhusu suala la hedhi salama kwa wasichana katika mtaa wa Mwanagati kata ya Mzinga jijini Dar es salaam.
Baadhi ya washiriki wakifuatilia mchezo wa Drafti huku semina ikiendelea.
Lengo la Mdaharo huo ni kuongeza uelewa kwa wakazi Mwanagati kuhusu masuala ya ukatili wa kijinsia pamoja na muendelezo wa maadhimisho ya siku ya hedhi duniani ambapo uadhimishwa kila ifikapo mei 28.

Akiongoza madharo huo Kiongozi wa Kituo cha Sauti ya jamii Kipunguni Bw. Selemani Bishagazi aliwapa historia kwa ufupi kuhusiana na siku hiyo na kuwaweka katika mjadala mpana wa kuwa je? kuna umuhimu wa wanaume kuweza kufahamu mambo mbalimbali kuhusu masuala ya hedhi?

Washiriki wengi wa mkutano huo walisema ndio ni vema kwa mwanaume kuweza kufahamu masuala ya hedhi na wachache pia walisema si vyema kwa wanaume kuweza kufahamu kwa kuwa haya mambo ni ya wanawake peke yake, na ikafikia hata baadhi ya wamama wakaamua kuondoka na kususia kikao kwa sababu wamewekwa pamoja na wanaume kuweza kujadili changamoto za hedhi.

Waliyokubali kuwa Wanaume wanapaswa kufahamu masuala ya hedhi walisema kuwa itasaidia kwanza kuweza kupanga uzazi kwa kuzingatia kalenda na kujiepusha na mimba zisizotarajiwa, lakini pia kwa vijana wadogo wa kiume wanaweza kuwa msaada mzuri kwa dada zao kuwastili pale wanapotokewa na hali hiyo na siyo kuanza kuwacheka kama ilivyo kwa watoto wengi wa hivi sasa.

Lakini pia kwa wazazi wa kiume wanatakiwa kufahamu ili wanapopanga bajeti wa watoto wao waendapo mashuleni watenge na pesa ziada kwa ajili ya taulo za kujistilia za watoto wao wakike na siyo kutoa fedha sawa kwa mtoto wa kike na wakiume kana kwamba hawajui mtoto wa kike kuwa anahitaji ya ziada kwa kazi hiyo.

kwa upande wa wale wanaopinga kuwa mwanaume haruhusiwi kufahamu masuala hayo wametoa hoja ya kuwa kwanza mila na desturi zinakataa baba au mwanaume kujihusisha na masuala hayo na kudai kuwa, Binti endapo atapitia katika hali hiyo amfuate Mama yake au kama Mama hayupo basi amtafute hata Mama mtu mzima yoyote ili amfundishe namna ya kukabiliana na hali hiyo.

Mwajuma Hassan ambaye nae ni mkazi wa mtaa huo ametoa mfano wa kwao pwani wanavyofanya na kusema yeye mwanae alivunja ungo hivi karibuni na yeye akiwa safarini, Na alichoweza kukifanya ni kuwapigia simu dada zake waje ili kuweza kukaa naye na kumfundisha nini cha kufanya, Na hata yeye alipojaribu kumgusia baba yake alisema hayo ni mambo yenu Wanawake mimi hayanihusu malizeni wenyewe.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa mtaa huo wa Mwanagati Mh. Ramadhani Kinyaiya amesema kuwa amefurahishwa sana na mjadala huo kwani unaibua mambo mengi mazuri na yenye manufaa kwa jamii kwani jamii ikielimika vitendo vya ukatili vitapungua kama siyo kuisha kabisa.

Na kuwaomba TGNP pamoja na wadau wengine kuendelea kujitokeza kutoa elimu mbalimbali za ukatili na pamoja na malezi mema kwa watoto hususani wakike ambao inaonekana kama jamii imewasahau kwa kiasi kikubwa.


Habari katika Picha.

Mwenyekiti wa Serikali ya mtaa wa Mwanagati Mh. Ramadhani Kinyaiya akifungua mkutano wa majadiliano ya Hedhi Salama uliyofanyika katika mtaa wake mapema jana jijini Dar es salaam.
Inspekta Peter Malonga, Polisi kata wa kata ya Mzinga akitoa elimu kwa wakazi wa kata hiyo kuhusiana na vitendo vya ukatili vinavyoendelea kuleta athari kubwa ndani ya jamii.
Mkazi wa mtaa wa Mwanagati kata ya Mzinga, Benny Mwasongwe akitoa hoja yake katika mkutano wa siku ya hedhi duniani. 
Mratibu wa Semina za Jinsia na maendeleo (GDSS) Jackson Malangalila akitoa neno kwa niaba ya uongozi wa TGNP.
Majadiliano yakiendelea katika mkutano.
Mwanaharakati/Mkurugenzi wa Taasisi ya Binti Makini Foundation Janeth John Kiko, akiwashirikisha uzoefu wakazi wa mtaa wa Mwanagati kata ya Mzinga jijini Dar es salaam. 
Washiriki wakiwa katika mchezo wa drafti ikiwa ni njia moja wapo ya kuwaunganisha wakazi ya kata ya Mzinga ili kuweza kushiriki mjadala wa siku ya hedhi salama.
Tausi Msangi kutoka kikundi cha Sauti ya Jamii Kipunguni akiwasilisha jambo kwa washiriki wa mkutano wa Hedhi Salama uliyofanyika mtaa wa Mwanagati kata ya Mzinga jijini Dar es salaam.
Wakazi wa mtaa wa Mwanagati kata ya Mzinga wakifuatilia mkutano.
Mkutano ukiendelea.



No comments