Simu, kutoaminiana vyatajwa kupasua ndoa · Takwimu zinatisha
MWANDISHI WETU
Imeelezwa kuwa migogoro ya ndoa ni moja ya matatizo sugu yanayoikabili jamii ya Kiislamu kwa sasa. Takwimu zilizopatikana kutoka wilaya kadhaa zineonesha idadi kubwa ya migogoro inaishia kwenye talaka.
Katika Wilaya ya Ilala pekee, katika kipindi cha mwaka 2020 Baraza la Bakwata Wilaya hiyo lilipokea kesi 440, ambapo kati yake kesi 158 ziliishia kwenye talaka baada ya suluhu kushindwa kupatikana.
Sheikh wa Wilaya ya Ilala, Adam Yusuph
Mwinyipingu ameliambia gazeti hili kuwa taasisi ya ndoa inayumba mno huku
sababu kuu zikitwajwa kuwa ni simu na kutokuaminiana baina ya washirika yaani
mume na mke au wake zake.
Akifafanua kuhusu takwimu za wilaya ya Ilala,
Sheikh Mwinyipingu alisema katika kesi 440 zilizopokelewa, ni mashauri 24 tu yaliyofanikiwa
kusuluhishwa.
Pia, ilielezwa kuwa kati ya mashauri yote
yaliyopokelewa, 157 yalipelekwa mahakama ya kadhi kwa ajili ya maamuzi na
nyingine 101yalipelekwa katika mahakama ya kawaida, alisema Sheikh Mwinyipingu.
Mchanganuo zaidi wa kesi hizo unaonesha kuwa ni wanaume 45 pekee ndiyo waliopeleka
madai ukilinganisha na mashauri 395 yaliyowasilishwa na wanawake.
“Kwa takwimu tulizonazo, inaonekana ni wanaume ndiyo wanawanyanyasa zaidi wanawake, ingawa uchache wa wanaume wanaopeleka madai unaweza kuwa pia umesababishwa na wanaume kutotaka kuchekwa mbele ya wanajamii na kuonekana dhaifu," alifafanua zaidi.
Sheikh Mwinyipingu alisema jamii inaona kuwa
ni haki ya mwanamke kwenda kulalamika katika vyombo vya kisheria, lakini
mwanamme anatakiwa awe na moyo mgumu na uvumilivu au amalize matatizo yake
mwenyewe.
Akielezea walivyojipanga kumaliza tatizo hilo
kwenye wilaya yake, Sheikh Mwinyipingu alisema wameamua kujikita katika kutoa
elimu ya ndoa kuanzia ngazi ya msikiti, kata hadi wilaya kupitia semina za mara
kwa mara.
Sheikh Mwinyipingu alisema miongoni mwa
walengwa wa semina hizo ni wanandoa watarajiwa.
“Watu wanaingia katika ndoa hali hawajui
wajibu na haki zao hivyo wanajikuta hawajibiki ipasavyo,” alisema.
Akitoa mfano, alisema inafikia hatua mahala
mwanamke anaamua kufanya kitu fulani na mume hataki. Mwanamke akilazimisha,
ugomvi unaanzia hapo.”
Sheikh Mwinyipingu alisema suala la uaminifu
ni muhimu. “Unakuta simu ya mwanamke haishikwi na mwanaume. Simu imejaa nywila
za kutosha basi hapo inakuwa tena hakuna amani. Muda wowote kutatokea
mtafaruku,” alisema.
Sheikh Mwinyipingu pia alielezea masikitiko
yake kwa vitendo vya baadhi ya watu kujiua kwa sababu ya mapenzi; na akatoa
wito kwa viongozi wa dini kulitafutia ufumbuzi jambo hilo.
Ripoti ya Jeshi la Polisi ya mwaka 2020 imetaja
wivu wa mapenzi kuwa moja ya sababu mbili kuu zilizochangia vifo vingi, kwa
baadhi watu kujiua au kudhuru wengine.
sababu nyingine ni watu kujichukulia sheria
mkononi wanapokamata mhalifu.
Kamishna wa Operesheni na
Mafunzo Makao Makuu ya Polisi, Liberatus Sabas, aliyewasilisha ripoti hiyo
jijini Dodoma alitoa wito kwa viongozi wa dini kuingilia kutoa elimu kwa
Waumini wao ili kupunguza matukio hayo.

.jpg)
.jpg)
No comments
Post a Comment