Zinazobamba

Kituo cha Kimisri chawanoa maimam, viongozi wa dini


Kituo cha kiislam cha Kimisri tawi la Tanzania kimeendesha mafunzo ya siku moja kwa maimam na viongozi wa dini juu ya nafasi ya viongozi katika kueneza usamehevu wa uislam na kuhuisha uzalendo kwa lengo la kuishi pamoja kwa upendo.

Katika mafunzo hayo ambayo yalifanyika April 30, 2022 katika ukumbi wa mikutano wa kituo hicho, jumla ya maimam na viongozi wa dini 170 walihudhuria.

Akizungumza katika mafunzo hayo, mmojawa wa watoa mada ambaye pia ni katibu wa baraza la ulamaa Bakwata Sheikh Khamis Mataka aliwataka viongozi hao kuenenza fikra sahihi zinazofudishwa na chuo cha Azhar kwani huo ndio msingi wa uislam.

“Toka chuo hiki cha Azhar Sharif kuanzishwa kwake hatujawahi kuona wanafunzi wake wakiwa sehemu ya kusambaza mafunzo yasio sahihi, tunawaomba endeleeni na tabia hiyo kwani huo ndio msingi wa Bakwata,” alisema Mataka

Kwa upande wake Mufti na Sheikh Mkuu wa Tanzania Sheikh Abubakar Zubeir bin Ali wa Mbwana aeungana na Katibu wake, Sheikh Khamis Mataka kwa kusisitiza kuwa Manhaji ya Bakwata ni mafunzo yanayotolwa na Chuo cha Azhar.

Alisema chuo hicho kinaeneza fikra sahihi za wastani, na zisizo za kuchupa mipaka, jambo linalosaidia kuleta amani na utulivu katika jamii.

 

 

Sheikh Zubeir alisema Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) ambalo yeye ndiye kiongozi wake mkuu, lina furaha kushirikiana na kituo hicho katika kufanikisha jitihada zake za kutoa elimu sahihi ya Uislamu.

 

Katika hafla hiyo, Mufti aliambatana na wasaidizi wake kadhaa akiwemo Sheikh wa Mkoa wa Bakwata, Alhadi Mussa Salum, ambaye naye alipopata nafasi ya kuzungumza aliwasisitizia na kuwakumbusha maimamu hao kuwa  Uislamu ni dini ya amani.

 

Kwa upande wake Mkurugenzi wa kituo hicho Sheikh Kamal Abdul-Mu’ty Abdul-Wahed alisema viongozi wa dini wana majukumu makubwa katika kuongoza jamii zao kwenye uongofu na ustawi na kuisukuma nchi mbele kimaendeleo.

 

Aidha, Sheikh Kamal alisema semina hiyo waliyoiandaa ni muendelezo wa shughuli na harakati za kituo chao katika kuimarisha uhusiano na taasisi nyingine za kidini, hususan taasisi kongwe zaidi ya Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA).

 

Semina hiyo iliyosimamiwa na mshereheshaji, Sheikh Hussein Mohammed Afif, ilifunguliwa kwa kisomo cha Qur’an Tukufu kilicholetwa na mwanafunzi wa kidato cha kwanza cha sekondari, Salim Masoud.

 

Mshereheshaji wa semina hiyo, Afif, ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya BAKWATA mkoa wa Dar es Salaam.

 

Miongoni mwa masheikh wengine waliohudhurisha mada katika semina hiyo ni pamoja na Sheikh Hany Mohammed Abdul-Latweif kutoka kituo cha Kimisri aliyezungumzia umuhimu wa uzalendo na kuishi pamoja kwa amani.

 

Sheikh Abdul-Latweif alisema dini ya Kiislamu na sheria zake zimesisitiza umuhimu wa kuzungumza na kuheshimiana katika kuhakikisha amani na utulivu katika  jamii na miongoni mwa makundi. Aliongeza kuwa sheria ya Kiislamu inawataka wafuasi wake washirikiane na wengine bila kujali tofuati za kidini, kikabila au nyinginezo kwa faida ya jamii.

Sheikh Mussa Hemed BiN Juma

Kwa upande wake Katibu wa Mufti Sheikh Mussa Hemedi bin Jumaa amewashauri waislam na wasio waislam kujenga tabia ya kusema neon asante kwa kila jambo wanalofanya kwani malezi hayo yatasaidia kusema Alhamdullah kwa kila jambo litakalo kufika.

Alisema jamii kwa sasa inakumbana na changamoto ya kusema neon asante hata kama amefanikiwa, tatizo hilo linawafika watu wa rika lote hata wazee.

“hatuna utaratibu wa kushukuru, jambo hili ni kinyume na mafundisho ya Allah, imefika wakati hata kumshuru Mungu kwa anayotutendea bado tunaona shida, kupitia ofisi ya Mufti niwaombe mkaenenze faida za kusema shukru kwa umma,” alisema

 

Pia, kiongozi huyo kwenye ofisi nyeti ya Mufti aliwahimiza Waislamu wawe wasamehevu kwa wasio waislamu. Alisema kwamba sheria ya Kiislamu inahimiza kusaidiana na kuelewana. Alisema mizozo, migogoro na mapambano haifai kwa sababu vinachangia amani na utulivu wa jamii.

Naye Dkt Mahmoud Shawky Attiya ambaye ni Naibu Mkurugenzi wa Kituo cha Kiislamu cha aliwahimiza maimamu kuhubiri tabia ya kusameheana na kupinga vurugu za kidini.

 

Washiriki wa semina hiyo walipata fursa ya kupatiwa cheti za mahudhurio kutoka kwa Mufti, pia katika hafla hiyo kiongozi mkuu wa kiislam hapa nchini, Mufti na Sheikh Mkuu wa Tanzania Sheikh Abubakar Bin Zubeir alitunukiwa kofia ikiashiria kupatiwa shahada ya udaktari kutoka chuo cha Azhar. Sasa Mufti nahesabika kama Dkt wa Heshma wa chuo cha Azhar Sharif.


No comments