Sauti za Busara 2026 Yathibitisha Ratiba Kamili, Tiketi Zakimbia Kuelekea Tamasha la Februari Zanzibar
Na Mwandishi Wetu,Zanzibar, Tanzania
Zikiwa zimesalia wiki mbili tu kabla ya kuanza kwa toleo la 23 la tamasha la Sauti za Busara, shamrashamra zinaendelea kuongezeka Zanzibar na nje ya nchi, huku maandalizi ya mwisho yakikamilika kwa ajili ya tamasha hilo maarufu linalojulikana kama “Tamasha Rafiki Zaidi Duniani.”
Tamasha litafanyika kuanzia Alhamisi tarehe 5 hadi Jumapili tarehe 8 Februari 2026, likitanguliwa na ufunguzi mdogo Jumatano tarehe 4 Februari, katika makazi mapya ya Viwanja vya Mnazi Mmoja, Stone Town.
Busara Promotions imethibitisha kuwa kuhamia katika eneo jipya lenye ukubwa zaidi kumeipa Sauti za Busara fursa ya kuongeza uwezo wa kupokea hadhira kubwa, kuboresha usalama na mtiririko wa watu, pamoja na kuinua uzoefu wa wasanii na watazamaji.
Kwa zaidi ya miaka 22, Ngome Kongwe ilikuwa kitovu cha kihistoria cha tamasha, ikitoa mazingira ya ukaribu na urafiki.
Hata hivyo, mwaka 2026 unaashiria hatua mpya ya ukuaji kupitia Viwanja vya Mnazi Mmoja, vinavyotoa nafasi pana, mandhari ya kijani, hewa ya bahari na mazingira rafiki kwa maendeleo ya baadaye ya tamasha.
Zaidi ya majukwaa makuu ya muziki, programu shirikishi za Sauti za Busara zinaendelea kuongeza thamani na athari za kijamii. Carnival Parade huligeuza Jiji la Stone Town kuwa jukwaa la wazi la burudani, likivunja mipaka kati ya wasanii na hadhira. Swahili Encounters huwakutanisha wanamuziki kutoka mataifa tofauti kwa mazoezi na maonyesho ya pamoja, yakilenga ushirikiano wa kisanaa.
Vilevile, majukwaa ya kitaaluma kama Movers & Shakers huimarisha mijadala ya sekta ya ubunifu na uchumi wa sanaa.
Kupitia Busara Plus, tamasha linafika pia nje ya Stone Town kwa kuandaa jukwaa la bure la jamii katika Fumba Town Nyamanzi. Hatua hii inalenga kusambaza fursa za kitamaduni kwa jamii pana zaidi, hasa vijana na wasanii chipukizi, bila vikwazo vya kifedha.
Masuala ya usawa wa kijinsia yanaendelea kupewa uzito mkubwa. Wanawake wanashiriki kikamilifu si tu kama wasanii, bali pia kama waandaaji, watayarishaji, wasimamizi na mafundi wa matukio. Sauti za Busara inaendelea kuwa mfano wa kuigwa katika kuhakikisha uwakilishi wa kijinsia unakuwa sera na vitendo.
Viwanja vya Mnazi Mmoja vitakuwa na majukwaa mengi ya muziki, maeneo yenye vivuli chini ya miti ya asili, soko lililopanuliwa la vyakula na bidhaa za mikono, pamoja na maeneo ya mitandao ya kitaaluma na upatikanaji bora wa usafiri.
Mahitaji ya tiketi za Sauti za Busara 2026 yamevunja rekodi, ambapo tiketi za Early Bird tayari zimekwisha, huku Advance Tickets zikiendelea kuuzwa kwa kasi.
Tamasha linatarajiwa kuwakutanisha zaidi ya wanamuziki 400 kutoka nchi 21 barani Afrika na duniani. Kinara wa tamasha ni gwiji wa muziki kutoka Mali, Salif Keita, ambaye umaarufu wake unaendelea kukua kufuatia wimbo wake uliotikisa dunia, “Yamore.”
Akizungumza kuhusu maandalizi hayo, Mkurugenzi wa Tamasha la Sauti za Busara, Journey Ramadhan, amesema mwitikio wa mwaka huu ni wa kipekee kutokana na mchanganyiko wa eneo jipya, orodha bora ya wasanii na kuongezeka kwa mvuto wa kimataifa, huku akisisitiza ushirikiano mzuri na Serikali ya Zanzibar katika kuhakikisha usalama na mafanikio ya tamasha.
Mbali na burudani, Sauti za Busara 2026 inaendelea kuimarisha mchango wake wa kijamii kupitia programu ya Inspire to Lead!, iliyoanza Januari 17, 2026 katika Viwanja vya Kibanda Maiti. Programu hiyo inatekelezwa kwa kushirikiana na Serikali ya Zanzibar, Umoja wa Ulaya na UN Women, ikiwa ni sehemu ya Gender Transformative Action Programme inayolenga kupinga ukatili dhidi ya wanawake na watoto na kukuza uongozi wa wanawake kupitia kampeni kama Tokomeza Vitendo vya Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto na Rijali Anajali.
Aidha, Busara Promotions imeripoti mwitikio mkubwa wa mpango wa GenderWork Tanzania, uliopokea maombi 179 kutoka nchi 11, ukilenga kuwajengea wanawake uwezo katika fani za kiufundi na kitaaluma ndani ya tasnia ya muziki na matukio. Kupitia ushirikiano na Music In Africa Foundation na ufadhili wa UNESCO, wanawake 30 tayari wamehitimu na wengi wao sasa wanafanya kazi kikamilifu katika sekta hiyo.
Kadri Zanzibar inavyojiandaa na msimu wake mkubwa wa matukio ya kitamaduni, Sauti za Busara 2026 inaahidi siku nne za muziki wa nguvu, mshikamano wa kitamaduni, athari za kijamii na sherehe kubwa katika Viwanja vya Mnazi Mmoja, Stone Town.
Waandaaji wanawahimiza wadau kununua tiketi mapema kutokana na mahitaji makubwa yanayoendelea kushuhudiwa.
Sauti za Busara 2026 si tamasha tu, bali ni taswira hai ya ubunifu wa Afrika, umoja na mustakabali wa pamoja.

No comments
Post a Comment