Zinazobamba

Bima ya Kiislam (Takaful) kuanza kutumika Mei

 Hatimaye miongozo ya bima ya kiislam (TAKAFUL) iliyokuwa ikisubiliwa kwa hamu na waislam walio wengi imezinduliwa rasmi jana na kwamba sasa makampuni yanayotaka kufanya biashara hiyo yanaweza kupeleka  maombi TIRA kuanzia mwezi Mei 1, 2022 ili waweze kusajiliwa tayari kwa kufanya biashara.

Akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa miongozo hiyo iliyofanyika katika ukumbi wa Kimataifa wa Mwl. JK Nyerere uliopo Posta Jijini Dar es Salaam, Kamishna wa  bima kutoka mamlamka ya usimamizi wa bima Tanzania (TIRA)  Dkt Baghayo Saqware  alisema miongozo hiyo itasaidia kuwezesha wawekezaji wanaofuata misingi ya dini ya kiislam kuwekeza katika biashara ya bima.



“Muongozo huu utaanza kutumika Mei 1, 2022. Maana yake ni kwamba ikifika tarehe hiyo Makampuni yanayotaka kufanya biashara ya Takaful yanaweza kuleta maombi yaweze kusajiliwa na kuanzisha biashara. Bima ya Takaful inafuata misingi ya kisheria (sharia compliance),” alisema Saqware

Vilevile alisema kuzinduliwa kwa miongozo hiyo kunafungua milango kwa wananchi kuanza kupata huduma za bima kwa kufuata misingi ya Sharia Compliance.

“Ni mategemeo yetu kuwa sasa wananchi ambao wanahitaji huduma kutoka kwa taasisi za namna hiyo wataanza kujiunga ili kupata kinga na kuingia kwenye mfumo rasmi wa kifedha hapa nchini,” aliongeza.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Cifca, Aref Nahd alisema kuzinduliwa kwa miongozo hiyo ni hatua kubwa imepigwa, japo bado hawajafika katika hatua wanayo itaka.

Aidha Mwenyekiti huyo alisema Taasisi hiyo iko tayari kufanya kazi na Taasisi yeyote inayotaka ushauri wa Takaful, kwani wanao wataalam wa kutosha kutoa elimu hiyo.

Naye mratibu wa CIFCA Sheikh Muhammad Issa alisema Biashara ya TAKAFUL ni kwa faida ya watanzania wote, na ni matumaini yake kuwa mifuko itatuna Zaidi kama watu wataifanya biashara hiyo ipasavyo.

Kwa upande wake mratibu wa zoezi la uandaaji wa miongozo ya bima 2022, Muyenge Zakaria amewapongeza CIFCA kwa ushirikiano walio utoa hadi kukamilika kwa muongozo wa TAKAFUL.

Bw. Zakaria alisema kwa kiasi kikubwa Cifca walitoa maelekezo muhimu yaliyochangia kutengenezwa kwa muongozo huo ambayo unatarajiwa kuleta tija katika taifa.

“baada ya uzinduzi huu tutaanza kutoa mafunzo mbalimbali, kwenye muongozo wa Takaful tutashirikiana na CIFCA, kimsingi wawezeshaji wetu watakuwa CIFCA. Mafunzo yataanza na wasimamizi wa sheria (Regulator) na baadae tutawaendelea wadau wengine.

Wadau mbalimbali walioudhuria hafla hiyo sasa wanaoona wawekezaji wataongezeka hasa kutoka katika nchi zenye kufuata misingi ya dini tukufu ya Kiislam huku wakipanua wigo mpana wa utoaji bima kwa makundi yote

Inaelezwa kuwa mchakato wa takafuli ulianza toka mwaka 2014 huku kituo cha ushauri wa mfumo wa fedha wa Kiislam  CIFCA wakiwa na mchango mkubwa katika kueleza faida za biashara ya TAKAFUL.


No comments