Mafunzo ya Takaful yazidi kusambazwa
Taasisi mbalimbali zimeendelea kuandaa mafunzo ya bima ya Kiislamu, Takaful, nchini ili kuongeza uelewa kwa wadau mbalimbali
Mafunzo haya yanaandaliwa kufuatia mafanikio ya juhudi za Kituo cha Usimamizi na Ushauri wa Masuala ya Huduma za Kifedha za Kiislamu Tanzania (CIFCA) katika kuunganisha nguvu za wadau katika kupigania serikali iruhusu bima hiyo.
Mafunzo ya hivi karibuni yaliandaliwa na Kampuni ya
Bima ya Zanzibar (ZCI), ambayo mwakilishi wake alisema anaamini soko la bima ya
Kiislamu ni kubwa kwa vile huduma hiyo imekuwa ikiulizwa na wateja.
Kutokana na hitajio hilo, Meneja wa ZCI kanda ya Dar
es Salaam na Pwani, Majda Issa, alisema wameandaa mafunzo hayo ya siku moja kwa
wadau wakiwemo madalali, mawakala na makampuni ya bima. Lengo la mafunzo hayo
limetajwa kuwa ni kuwajengea uelewa wadau hao.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi, mwezeshaji
wa semina hiyo ambaye pia ni Mratibu wa CIFCA, Sheikh Muhammad Issa alisema
katika semina hiyo, mada mbalimbali ziliwasilishwa ikiwamo kuhusu tofauti ya
takaful na bima za kawaida; na namna kampuni na wadau wengine wanavyoweza
kupata faida.
“Katika semina hii tulifundisha mfumo mzima wa
takaful unavyofanya kazi, na pia namna bima hii itatanua wigo wa matumizi ya
huduma za bima kwa ujumla wake kwani kwa sasa bado hali hairidhishi,” alisema
Sheikh Muhammad.
“Takwimu zinaonyesha kwamba mchango wa sekta ya bima
katika pato la taifa ni asilimia 0.5, lakini malengo ya Mamlaka ya Bima (TIRA)
ni kukuza sekta hiyo angalau iweze kuchangia asilimia 1.5,” alisema Sheikh
Muhammad.
“CIFCA inafurahishwa kuendesha semina hizi kwa
sababu wanakuwa sehemu ya kukuza sekta ya bima hapa nchini na hivyo kuchangia
ukuaji wa pato la taifa,” alisema aliongeza Sheikh Muhammad na kuongeza kuwa
tayari kuna mabadiliko ya kuongezeka mwamko, licha ya changamoto zilizopo.
“Mwamko ni mkubwa. Kama unavyoona, watu wanajitokeza
kwenye semina wakitaka kusikia takaful ni kitu gani hasa, tumeshafanya semina
takribani nne na nyingine zinakuja. Kikubwa sasa ni kuongeza jhudi ya kutoa
elimu kwa umma naoi li wafahamu takaful,” alisema.
Ataja changamoto
Akitaja baadhi ya changamoto zinazokabili bima hii
mpya, Sheikh Muhammad alisema idadi ya Masheikh watakaoshiriki moja kwa moja
kama wakuu wa bodi ni wachache kwa sababu wengi wao hawajasomea mambo ya
takaful.
Katika kukabiliana na changamoto hiyo, Sheikh
Muhammad alisema tayari wameanza kuwajengea uwezo masheikh kuhusu uendeshwaji
wa biashara ya bima na ana imani kuwa baada ya muda kila kitu kitakuwa sawa.
“Baadhi ya taasisi za wanazuoni wa Kiislamu zimeanza
kutoa mafunzo ili kuziba pengo hilo la wataalamu, ambapo moja ya taasisi hizo
ni Hay-atul Ulamaa.’ Kama hatua ya mpito ya kutatua tatizo la kukosekana
wataalamu Sheikh Muhammad alishauri wataalamu waliopo wahudumie zaidi ya
kampuni moja kwani sio dhambi kufanya hivyo.
“Kwa wakati huu ambapo tunafanya jitihada za
kuongeza wataalamu wa kuziba pengo la masheikh watakaosimamia takaful, haina
maana soko lisimame. Tunaweza kuwatumia waliopo. Imefanyika kwenye benki za
Kiislamu na mambo yamekwenda vizuri. Leo hii tunazo huduma za benki za
Kiislamu,” alifafanua.
Mshiriki mmoja katika mafunzo hayo Marley Shabaan
kutoka taasisi ya Af-Marzom Insurance alisema bima ya takaful ina manufaa
makubwa kwa mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.
“Licha ya kwamba bima hii ina jina la Kiislamu,
haina maana kuwa wanunuzi wake ni Waislamu pekee. Hii ni bidhaa kama bidhaa
nyingine na anaweza kununua Mtanzania yeyote. Watu wasiogope,” alisema.
Kwa upande wake, Abdallah Rashid Khamis, Mkurugenzi
wa FAM Insurance Broker alisema bidhaa ya takaful ni mpya hapa nchini lakini
anaamini wateja wapo wengi na biashara itakuwa kubwa zaidi.
Alisema bima ya takaful imekuja kuondoa pengo
lililopo la bima, kwani kulikuwa na watu wengi hawatumii bima za kawaida kwa
sababu inaenda kinyume na mafundisho ya dini yao, hususan Waislamu.
Itakumbukwa hivi karibuni mamlaka ya TIRA ilizindua
miongozo ya bima ya Kiislamu na kinachoendelea sasa ni watu kujipanga kwa ajili
ya kusajili kampuni za kutoa huduma hizo.
TIRA ilitangaza kuanzia Mei 1, 2022 kama tarehe ya
kuanza kupokea maombi ya kampuni zinazotaka kufanya shughuli hizo. Mchakato wa
kuanzisha takaful ulianza toka mwaka 2014 huku CIFCA wakiwa na mchango mkubwa
katika kushauri serikali ikubali huduma hizi.





No comments
Post a Comment