Nondo 6 za ACT Wazalendo kwa Wizara ya Maendeleo ya jamii, jinsia, wanawake na makundi maalum mwaka wa 2022/23
OFISI
YA WASEMAJI WA KISEKTA.
HOTUBA YA MSEMAJI WA SEKTA YA MAENDELEO YA USTAWI WA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO- ACT WAZALENDO NDG. JANETH J. RITHE KUHUSU MPANGO NA BAJETI YA WIZARA YA MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WANAWAKE NA MAKUNDI MAALUM KWA MWAKA WA FEDHA 2022/23.
Jana tarehe 30 Mei, 2022 Waziri wa Maendeleo ya jamii, jinsia,
wanawake na makundi maalum Dkt. Dorothy Gwajima (Mb), aliwasilisha Bungeni
mpango wa wizara na makadirio ya mapato na matumizi ya fedha kwa mwaka 2022/23.
Bunge lilipokea, kujadili na kuidhinisha makadirio ya mapato na matumizi ya
shilingi bilioni 43.4, kati ya hizo shilingi bilioni 32.31 ni fedha za matumizi
ya kawaida na shilingi bilioni 11.09 ni kwa ajili ya miradi ya Maendeleo. Katika
kuendeleza utaratibu wetu wa kufanya uchambuzi wa kila bajeti ya wizara. Sisi,
ACT Wazalendo kupitia Kamati ya Wasemaji wa kisekta ya kuisimamia, mimi Janeth
Joel Rithe ambaye ni Msemaji wa Sekta ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii,
Wanawake na Watoto nimesikiliza na kuichambua hotuba na kufuatilia mwenendo wa
utekelezaji wa bajeti za wizara hii kwa miaka iliyopita. Ninafahamu kuwa wizara
hii changa lakini katika mfumo wa kibajeti ilikuwa inategemewa bajeti kupitia
fungu la 53 wakati ikiwa kama idara kuu katika wizara ya afya.
Hivyobasi, katika hotuba yangu nimeweka hoja kuuu sita (6) kuhusu
mpango na makadirio ya mapato na matumizi ya fedha kwenye wizara hii kwa mwaka
wa 2022/23.
1. Ufinyu wa bajeti unaifanya
wizara kubaki kuwa ni idara
Pamoja na wadau mbalimbali kupokea kwa furaha
hatua za uundwaji wa wizara ya Maendeleo ya jamii, jinsia, wanawake na makundi
maaalum. Mpango na makadirio ya mapato na matumizi yaliyowasilishwa jana
bungeni na Waziri inaonyesha wazi kuwa serikali haijajiandaa kuifanya hii ni
wizara itakayoweza kukabiliana na changamoto ambazo hapo awali zilishindikana. Ni
wazi kuwa bajeti ni nguzo muhimu sana katika kuhakikisha
vipaumbele na mipango iliyowekwa inatekelezwa.
Ukitazama,
katika mwaka huu bajeti iliyoidhinishwa na bunge ni shilingi Bilioni 43.4 kiasi ambacho
ni pungufu kwa asilimia 5.6 kwa kulinganisha na bajeti ya mwaka 2021/22 (ambayo
ilikuwa sh, bilioni 45.97) wakati ikiwa ni idara kwenye iliyokuwa wizara ya
afya, Maendeleo ya jamii, jinsia, wanawake, wazee na watoto. Aidha, kwa
kulinganisha kiasi kilichotengwa kwa ajili ya wizara hii na bajeti kuu ya
serikali ni sawa na asilimia 0.11 pekee kwa mwaka huu. Kati ya fedha zote,
fedha zilizotengwa kwa ajili ya miradi ya Maendeleo ni kiasi cha shilingi Bilioni
11.09 sawa na asilimia 25 ya bajeti ya wizara ikiwa ni kiwango pungufu kwa bilioni
3.81 ukilinganisha na fedha zilizotengwa kwa ajili ya maendeleo mwaka 2021/22
ambapo ilitengwa bilioni 14.90 upungufu huu sawa na asilimia 25.5.
Hivyobasi, ufinyu huu wa bajeti unaipotezea
serikali uhalali wa kuifanya hii ni wizara inayojitegemea ikiwa mpango wake,
vipaumbele na utengaji wa bajeti unafuata mwenendo ule ule kama ilivyokuwa ni
idara kuu kwenye wizara.
ACT Wazalendo tunaishauri serikali kuhakikisha
inatenga fedha za kutosha kwa ajili ya miradi ya Maendeleo kwenye wizara hii
ambayo inashughulikia mafunzo ya uanagenzi, uhamasishaji wa Maendeleo na
uratibu wa fedha za mikopo ya vijana, wanawake na walemavu.
2. Uhaba mkubwa wa
maafisa ustawi na Maendeleo ya jamii
Uhaba wa
rasilimali watu kwenye sekta hii muhimu unapelekea kushusha ufanisi wa utendaji
na kukwamisha utekelezaji wa mipango na majukumu.
Kwa mujibu wa
taarifa ya wizara kupitia hotuba ya bajeti mwaka 2022/23, Waziri anaonyesha
upungufu mkubwa wa maafisa wa ustawi na maafisa wa Maendeleo ya jamii hususani
katika ngazi ya vijiji na kata. Taarifa zinaonyesha kuwa mahitaji ya maafisa
Maendeleo ya jamii ni watumishi 5,296 idadi ya maafisa waliopo kwa sasa ni
3,014, kwahiyo kuna upungufu wa maafisa wa Maendeleo ya jamii 2,282 sawa na
asilimia 43. Kwa upande wa maafisa wa
ustawi wa jamii wanaohitajika ni 23,135 waliopo ni 740 na kufanya upungufu wa
watumishi 22,395 sawa na asilimia 97 ya upungufu.
Katika bajeti ya
mwaka hakuna kiasi cha fedha kilichotengwa kwa ajili ya kuajiri maafisa wa
ustawi na Maendeleo ya jamii ili kukabiliana na upungufu huu. Waziri, Dkt.
Gwajima ameishia tu kutaja changamoto bila kutenga fedha kukabiliana na
changamoto yenyewe.
ACT Wazalendo,
tunaishauri serikali kuweka mkakati wa kukabiliana na changamoto hiyo kwa awamu
ya miaka minne kwa kuhakikisha inatoa ajira kwa wastani wa watumishi 6,169 kila
mwaka.
3.
Ukatili
dhidi ya wanawake, wazee na watoto
Vitendo vinavyosababisha athari za kimwili, kingono,
kisaikolojia au mateso kwa wanawake
na watotoi, ikiwa ni pamoja na kutishiwa maisha, kunyimwa
uhuru, iwe hadharani au kwa kificho vinazidi kuongezeka nchini kwetu.
Ukatili dhidi ya wanawake kupitia mitandao ya kijamii, ubakaji, ukeketaji,
vipigo kwa wanandoa, mauaji ya wanawake na watoto imekuwa ni jambo
linaloonekana kuzoeleka nchini. Pia, matukio ya ulawiti na ubakaji kwa watoto
vinazidi kushamiri tena vitendo hivyo vinafanywa na watu wao wa karibu kabisa,
baba mzazi, baba wa kambo na ndugu wa karibu (walezi wao).
Utafiti huo ulifanywa mwaka 2021 wa Shirika la kuhudumia Watoto Duniani (UNICEF – Tanzania) na Shirika la ECPAT International na INTERPOL unaonyesha kuwa silimia 4 ya watumiaji wa mtandao
wenye umri wa miaka 12 – 17 nchini Tanzania
ni manusura wa ukatili wa mtandaoni; Watoto wengi hufanyiwa vitendo vya ukatili kupitia mitandao ya kijamii kama vileWhatsApp, Instagram, Facebook,
Tik Tok,
wanaofanya vitendo vya
ukatili ni watu
wanaofahamika na watoto
wakiwemo Ndugu
wa karibu na marafiki. Aidha watoto wanaofanyiwa ukatili hawajui namna na sehemu ya kutoa taarifa ili wapate msaada.
Pamoja na takwimu
za Jeshi la Polisi kuhusu Hali ya uhalifu
na matukio ya usalama
barabarani kuonesha
kupungua kwa matukio ya ukatili yaliyoripotiwa
mwaka 2021 ikilinganishwa na miaka iliyopita,
bado tumeendelea kushuhudia matukio ya
vitendo vya ukatili mara kwa mara kwenye
vyombo vya habari hususan kupitia mitandao ya
kijamii. Aidha,
ripoti ya jeshi la polisi inataja miongoni mwa ukatili dhidi ya watoto
ulioripotiwa kwa kiwango kikubwa kuwa dhuluma za kingono ambapo katika mwaka wa
2020 kuliripotiwa visa 7263 ikiwa ni ongezeko la asilimia 26 ikilinganishwa na
mwaka 2015 ambapo vilirikodiwa visa 5803, hii ikiwa ni sawa na visa 615 kwa
mwezi jambo ambalo linatajwa kuwa linahatarisha mustakabali wa ustawi kwa
watoto nchini humo
ACT Wazalendo inaitaka serikali kuweka mikaka Madhubuti ya kukomesha
ukatili dhidi ya
wanawake na watoto, hasa ukatili wa kingono, kimwili na udhalilishaji kwenye mitandao kwa kuboresha madawati ya jinsia, kuweka mifumo rahisi ya kuripoti na kudhibiti ukatili. Pia, tunaishauri serikali kuunda tume maalumu ya kudhibiti
ukatili wa kijinsia na kuhakikisha vyombo vya mahakama vinawezeshwa kimafunzo na kimfumo ili
kusimamia
kesi za ukatili kwa
haraka na
uhakika.
4. Kuongezeka kwa
watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi
Ni jambo
linalosikitisha kuona kasi kubwa ya kuongezeka kwa idadi ya watoto wanaoshi
katika mazingitra hatarishi kila mwaka.Serikali haionekani kustushwa na
ongezeko hili lisilo la kawaida na kuchukua hatua stahiki kuondokana na tatizo
lenyewe.
Tanzania
imeridhia kutekeleza Azimio la Umoja wa Mataifa juu ya Haki za Mtoto (UNCRC). UNCRC
ni chombo cha kisheria ambacho kinaelekeza na kinasisitiza haki za msingi za
watoto duniani pote na hii inahusisha, haki ya kuishi, kujiendeleza/kuendelezwa
kwa kadiri ya uwezo wa mtoto, kulindwa dhidi ya madhara na mazingira yanayoweza
kumdhuru, kumnyanyasa na kutumiwa kwa njia ya kudhulumiwa; kushiriki kikamilifu
katika maisha ya kifamilia, kitamaduni na kijamii.
Takwimu
zinaonyesha kuwa idadi ya watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi imefikia jumla ya watoto 218,369 (Me 85,699
na Ke 132,670) hawa ni wale tu waliotambuliwa na
wizara kati ya 2,398,354 wanaoishi katika mazingira magumu
nchini. Katika mwaka huu bajeti iliyotengwa na wizara kiasi cha Bilioni 2.6 kwa
ajili ya kukabiliana na watoto wanaoishi katika mazingira magumu na ukarabati
wa mahabusu za magereza ya watoto. Utengwaji wa bajeti hauzingatii kiini
kinachosababisha kuwepo kwa watoto wa mitaani na watoto wanaoishi katika
mazingira magumu.
Tunaishauri
serikali kuja na mpango wa kumaliza migogoro ya wanandoa, kukabiriana na
umaskini na kusimamia huduma bure za afya, lishe na makazi bora.
5.
Kasi
ndogo ya Uwezeshaji wa wanawake kiuchumi
Waziri imetoa Takwimu kuwa jitihada za serikali za kuwezesha
wanawake kiuchumi kwa katika kipindi cha mwezi Julai 2021 hadi mwezi Aprili 2022, jumla ya wanawake wajasiriamali 1,167 wamejengewa uwezo kupitia mafunzo yaliyotolewa katika Mikoa ya Shinyanga, Geita, Katavi na Tanga na takribani kiasi cha shilingi Bilioni 16.1
zilitumika kuwawesha wanawake hao.
Inasikitisha sana kwa serikali kutangaza kuwezesha
wanawake 1,167 nchi nzima. Kwa Mwenendo huu serikali inaweza kuchukua zaidi ya
miaka mia moja kukamilisha malengo ya kuwainua wanawake wote wapatao milioni
29.8.
Ni
muhimu suala la uratibu wa uwezeshwaji wa wanawake nchini utengenezewe mwongozo
na utaratibu utakaotumika ili kila mwanamke anapohitaji msaada ajue utaratibu
utakaomwezesha kupata msaada kwa haraka na uhakika.
6.
Huduma bora za afya na uzazi salama kwa wajawazito na
mama na watoto.
Mazingira rafiki ya huduma za uzazi ni haki ya kila
mwanamke
na mtoto.
Sera ya kutoa huduma za afya bure kwa
wajawazito, watoto chini ya miaka mitano (5) na wazee, ni kiini macho tu yaani
haitekelezwi kwa ufanisi. Kutotekelezwa kwa ufanisi unachangia pia kutokana na
uhaba wa Miundombinu ya msingi katika vituo vya afya (zahanati, vituo vya afya,
hospitali za wilaya na hospitali za rufaa za Mikoa). Aidha ukosefu wa vituo vya
afya kwenye baadhi ya vijiji vinafanya umbali mrefu kufikia huduma za afya jambo linalosababisha wajawazito kujifungulia
njiani, kukosa huduma bora na salama za uzazi na vifo vya mama wajawazito. Takwimu
za wiza zilizo kusanywa kutoka vituo vya kutolea huduma za afya nchini zinaonesha vifo vitokanavyo na uzazi kuwa 1,580 mwaka 2021. Na hii, haijumuishi vifo zinavyotokea kwa ngazi ya
jamii.
Pamoja na hali hiyo,
watoto wenye umri chini ya miaka mitano, wajawazito na wazee wenye miaka zaidi
ya 60 wana haki ya kupata matibabu bure kwa mujibu wa sera ya matibabu bure
kutoka katika vituo vya afya vya serikali.
Hata
hivyo, utekelezaji wake umekuwa na changamoto kubwa, tathmini yetu inaonyesha
kuwa wastani wa asilimia 40 ya watoto wenye umri chini ya miaka mitano
wanalazimika kulipia matibabu. Vilevile, kwa wajawazito wanalipishwa matibabu
na inatokea hivyo kwa watu wenye miaka zaidi ya 60 hulazimika kulipia huduma
hizo tofauti na utaratibu uliopo.
Tunaitaka
Serikali ifuatilie kwa makini utekelezwaji wa sera hii ili kuhakikisha kuwa
walengwa – ambao ni watoto, wajawazito na wazee wanapata haki zao za msingi.
7.
Kuongezeka
kwa matukio ya mauaji na vifo vya wanandoa na wanajamii.
Hali ya
usalama ya wananchi hususani wanandoa na watu wenye mahusiano ya kimapenzi
imezidi kuwa katika hali mbaya kwa takribani mwaka. Ndani ya mwezi Mei, 2022
kumeripotia zaidi ya matukio makubwa 8 ya mauaji ya wapenzi au wanandoa ama
wanafamilia kwa sababu za wivu wa kimapenzi au kukosa maelewano katika
ndoa/familia.
Takwimu za hivi karibuni
zilizotolewa na Jeshi la Polisi zinaonyesha kuwa kuanzia Januari hadi Juni 2021
watu 15,131 walifanyiwa
ukatili wa kijinsia huku ripoti hiyo ikionyesha ongezeko la mauaji kwa wanawake
walio katika ndoa.
Vilevile, ripoti iliyotolewa Septemba
2021 na jarida la Afrika
kuhusu hali ya ukatili wa kijinsia Tanzania miongoni mwa wanandoa, imeonyesha kuwa,
asilimia 46 ya wanandoa hufanyiwa ukatili wa kijinsia, ambapo asilimia 36 walifanyiwa ukatili wa kimwili na
asilimia 32 walifanyiwa ukatili wa kisaikolojia na asilimia 13 walifanyiwa ukatili wa kingono.
ACT
Wazalendo tunaishauri serikali kupitia jeshi la polisi kuimarisha uwezo wa
kubaini matukio ya uhalifu na kuweka mazingira rafiki ya wahanga kutoa taarifa
na taarifa kufanyiwa kazi.
8. Mazingira magumu
ya wafanyabiashara wadogo na
ushirikishwaji katika utungaji wa sheria ya Wamachinga.
Tumesikiliza hotuba ya waziri, tumeona mikakati
iliyowekwa kuhusu wamachinga ni kwa ajili ya kuimarisha ofisi za viongozi wa
wamachinga na sio katika kuboresha mazingira ya Wafanyabiashara madogo
(wamachinga, mamalishe, na wajasiriamali wengine) bado hayajawekewa mkakati wa
kuondoa changamoto zao. Sekta ya biashara ndogo ina mchango mkubwa sana nchini
kwenye pato la taifa wastani wa asilimia 22 na mchango wake kwenye sekta ya
ajira ni wastani wa asilimia 14 ya nguvu kazi nchini zinapatikana kwenye
biashara ndogo.
Hali
ya sasa wafanyabiashara
hawaonekani wakilindwa kisheria au shughuli zao kutambulika kama halali kwenye
mchango wa uchumi wetu. Kwa, kifupi Wafanyabiashara wadogo hawachukuliwi kama
injini ya maendeleo ya miji na majiji. Uamuzi wa kuwapanga Wafanyabiashara wadogo umetikisa
uaminifu wao kwa taasisi za kifedha. Matukio ya kuungua moto kwa masoko ya
Wafanyabiashara wadogo yamesababisha hasara kubwa sana kwa Wafanyabiashara.
Tafiti nyingi, zinaonyesha uhusiano uliopo katika
shughuli za Wafanyabiashara wadogo na ukuaji na uendelezaji wa viwanda vidogo
nchini. Asilimia 47 ya biashara ndogo zinahusisha bidhaa za kilimo ambazo
zinaongezwa thamani.
ACT
Wazalendo tunapendekeza kuwa Serikali kwa kuziweka pamoja na wizara ya
Maendeleo ya jamii, Viwanda na uwekezaji na TAMISEMI kusikiliza na kuondoa
vikwazo kwa wafanyabioashara wadogo. Pia, katika mchakato wa kutunga kwa sheria
ya wamachinga nchini, ushirikishwaji wa wamachinga uwe wa hali ya juu.
Hitimisho.
Bajeti
ni chombo muhimu sana katika kupima vipaumbele vya matumizi ya fedha za umma katika
kukabiliana na changamoto za wananchi. Katika kutazama bajeti ya mwaka huu
haiakisi uhalisia wa mahitaji ya wizara.Wizara imetenga bajeti kama vile ni
idara kuu ya wizara ya afaya kama ilivyokuwa mwaka jana. Ni muhimu kwa serikali
kuona mikakati yake inatafsiriwa kwenye ugharamiaji wa mikakati hiyo kupitia
bajeti. Aidha, changamoto za mauaji, ukatili dhidi ya wanawake, wazee na watoto
ni muhimu zinapewa kipaumbele kama tulivyoshauri.
Ndg. Janeth Joel Rithe
Msemaji wa Sekta ya Ustawi na Maendeleo ya jamii,
wanawake na waototoi,
ACT Wazalendo
31 Mei, 2022.
.jpg)
No comments
Post a Comment