Waziri Makamba asifu kazi inayofanywa na Africab
Waziri wa Nishati January Makamba akiwa katika ukaguzi. |
Mwandishi wetu
Waziri wa Nishati January Makamba amesifu kazi inayofanywa na
kiwanda cha Africab kinachojishughulisha na uzailishaji wa vifaa vya umeme kilichopo
kurasini, jijini Dar es salaam
Aidha, ameelezea kuridhika kwake na ubora wa bidhaa
zinazotengenezwa na kiwandani hapo huku akiwasihi kuendelea kuzingatia ubora huo
ili bidhaa zao ziweze kukidhi mahitaji kwenye soko.
Makamba amezungumza hayo jana Jijini Dar es Salaam alipofanya
Ziara ya Ukaguzi katika kiwanda cha Africab ili kuangalia hali ya Utendaji kazi
katika uzalishaji wa vifaa vya umeme hapa nchini.
Pia ametoa ushauri kwa viwanda vya ndani kuzingatia ubora katika
bidhaa.
Amesema hali ya Ufanisi wa viwanda vya ndani utaisaidia Serikali
kuondokana na utegemezi wa bidhaa za nje ya nchi ikiwemo kuepuka gharama za
uagizaji wa vifaa vya umeme nje ya nchi na kuharakisha utekelezaji wa miradi
mbalimbali ya umeme nchini.
Kwa upande wake David Tarimo ambae ni Mwakilishi kutoka Africab,
akizungumza mbele ya Waziri wa Nishati January Makamba ameihakikishia Serikali
kuendelea kuzalisha Vifaa vya umeme kwa viwango vya kimataifa
Aidha, Tarimo aliiomba Serikali kutoa ushirikiano kwa viwanda vya
ndani kwani vina uwezo mzuri wa kuzalisha bidhaa zinazokidhi vigezo.
“Tumefarijika kutembelewa na viongozi wa serikali, sisi Africab tunao uwezo mkubwa wa kuzalisha vifaa vyote vya umeme vikiwemo transfoma, na nyaya za umeme, kwa sasa tunajenga kiwanda kikubwa kule Kimbiji ambacho tunaimani kitasaidia kukidhi mahitaji ya nyaya za umeme hapa nchini,” alisema Tarimo
Mbali na kuongeza uzalishaji, pia Tarimo amesema Kampuni yao
inajivunia kuongeza ajira kwa watanzania na kutoa ombi kwa serikali kuendelea
kuwaunga mkono.
Katika hatua nyingine, Tarimo ameipongeza serikali kwa kitendo
chake cha kutoa maamuzi ya kutumia bidhaa zinazozalishwa nchini.
“Watanzania tunao uwezo wa kufanya vitu vyetu wenyewe bila
kutegemea bidhaa kutoka nje ya nchi,” alisema
Aidha akizungumzia uwezo wa kiwanda kuzalisha, Tarimo amesema
kiwanda kinauwezo mkubwa wa kuzalisha vifaa vya umeme
“Tunaiomba serikali iendelee kutuunga mkono, Kiwanda cha Kimbiji
kitatoa bidhaa nyingi za umeme, vifaa kama nyaya za umeme, swichi, transfoma na
vifaa vingine vyote vitazalishwa hapo,” aliongeza
Hakuna maoni
Chapisha Maoni