siku zako zinahesabika!
Adeladius
Makwega-Dodoma.
Waswahili
huwa wana maneno ambayo yanatamkwa kwa hasira na mara nyingi hasira hizo ni
miongoni mwa vijana kwa vijana na mara chache mno kuona mzee kushindana na
vijana labda iwe kwa utani. Kauli ambazo zinatolewa katika hali ya hasira ni
nyingi mathalani utakiona cha mtema kuni! Utanitambua! Siku zako zinahesabika! Siku
zako zimekwisha! Tuone sasa kati ya mimi na wewe nani zaidi! na kauli nyingine
nyingi.
Kwa
siku ya leo ninatilia maanani kauli mbili tu nazo ni siku zako zinahesabika na
siku zako zimekwisha.
Unapoambiwa,
siku zako zinahesabika! Kwanza,
fasili yake ni moja bado unazo siku za kufunga safari mpaka kwa huyo aliyetamka
maneno hayo. Mnaweza kukaa mkayazungumza ili kuyamaliza. Pili, nafasi ya kumtuma
mtu ipo, maana utamuagiza ndugu/jamaa/rafiki ili akalifafanue jambo
hilo/kukuombea msamaha.
Tatu,
kama utakwenda mwenyewe au utamtuma mtu maana yake nafasi ya kusamehewa ipo,
japokuwa hata kukutaliwa kusamehewa kupo (50/50). Litazungumzwa jambo hilo na pengine
kitakuwa kikao cha watu kadhaa, mtajadili na kufikia tamati na yule mkosaji
kuomba msamaha na maisha kuendelea.
Ukija
kwa msemo siku zako zimekwisha!
Kwanza, fasili yake ni kuwa hakuna nafasi ya kumfuata mhusika na kumuomba
msamaha, hakuna nafasi ya kumtuma mtu na pia hakuna nafasi ya msamaha kabisa. Maana
yake ulipewa nafasi ukaitumia vibaya au ukarudia kosa kule katika siku zako
zinahesabika.
Kwa
makabila ya kibantu hii ni kaulu nzito na yakitamkwa mbele ya watu zaidi mmoja
na yule aliyetamkiwa akipata shida yoyote ile adui nambari moja huwa ni yule
aliyetamka hayo. Anayetamka maneno haya kama ni kijana kwa kijana (watu wa rika
moja) hapo matokeo yake ni kufishana (kuuwana) hapo ni ugomvi wa vijana(watu wa
rika moja) ambapo madhara yake yanakuwa kwa wawili hao na pengine
kuambukiza hata jamii zao haziwezi
kuombana chochote, kuoleana na hata kuzikana.
“Sisi
na wale, huwa hatuoleani ni mwiko, marehemu baba aliniambia hata iweje hakuna
ndoa na ukoo huo.”
Ukifuatilia
utakutana na viapo hivyo ambavyo mwisho wake unakuwa uadui wa kudumu. Kumfisha
mtu unaweza kufanya kwa kumtoa roho na kwa sasa unaweza kumfisha mtu hata
kitaaluma akashindwa kusonga mbele kwa maneno yaliyotamkwa dhidi yake.
Yanapotamkwa
maneno kama haya na mtu mzima hilo huwa ni jambo la hatari mno, tena kumtamkia
kijana. Maana yake huyo aliyetamkiwa atapatwa na madhara na yakitokea yule
aliyetamka anapaswa kuhamishwa katika eneo hilo na pengine kupelekwa ugenini ili
kuepusha visasi kwa jamii hiyo. Kama aliyetamka ni sehemu ya watumishi wa chifu
hapo lazima kunakuwa na mjadala mkubwa wa ndani kwani yapo mambo ya mwiko
kuyafanya hadharani, mhusika lazima aondolewe maana visasi huwa havipaswi
kuwepo nyumbani kwa chifu.
Unaweza
ukasikia katika ukoo fulani fulani kuwa sisi tuna babu yetu alikimbilia upande
fulani kisa alituhumiwa kwa hili na lile. Maana kukiuka mwiko huwa ni ulozi (uchawi).
“Utasikia
tema mate chini, mambo hayo yapitilie mbali na ukoo wetu.” Hii inakuwa laana
kubwa kwa mtu mwenye mvi kutamka maneno ya madhara kwa kumlaani kijana.
“Huko
kuinama kunaisha, mkiingia katika mitandao ya kijamii, mnashambulia kama nyuki
na kwa bahati nzuri wengi wenu majina yenu ya kibandia ninayajua, huwa najua
huyu ni wakili fulani, huyu ni fulani, anamshambulia jaji kwa jina. Wakati mwingine
yuko mahakamani, kesi inaendelea.Yuko mahakamani, anamshambulia wakili wa
upande wa pili, anamshambulia hakimu, anamshambulia jaji. Lakini tunawafahamu.
Siku zao zimekwisha na nyinyi msikubali kuingia katika huo mtego…”
Hayo
maneno niliyonukuu ni sehemu ya hotuba ya Jaji Mkuu ambayo aliyatoa katika
shughuli mojawapo ya mawakili/wanasheria wapya hivi karibuni ndani yake
alilitamka neon siku zao zimekwisha.
Binafsi
nilimfuatilia Mheshimwa Jaji Mkuu wakati akiyasema maneno haya kwani hakuyasoma
katika hotuba yake, bali alikuwa akiyasema bila ya kupitia sehemu ya hotuba
hiyo. Ndiyo kusema alikuwa akilisema jambo ambalo kwanza alikuwa analifahamu
kwa kina. Pili inaonekana jambo ambalo lilikuwa linamkwaza mno.
Nakubaliana
sana na Jaji Mkuu kuwa pengine hao anaowatuhumu inawezekana wamefanya kosa
hilo. Kwa mamlaka ya Jaji Mkuu kimahakama yeye ni mtu wa mwisho ambapo sisi
sote tunamtegemea yeye kusaidia kunyoosha pale haki inapopindishwa. Kitendo cha
Jaji Mkuu kumlalamikia mtu yoyote ambaye yupo katika uwanja wake hadharani ni
kosa kubwa sana katika kulinda heshima ya muhimili huu. Jambo hilo
linakaribisha wachokozi kuendelea kufanya hivyo na tena kwa nguvu zaidi.
Jaji
Mkuu, kwa maelezo yake mwenyewwe anasema kuwa anawafahamu baadhi ya hao
wakosaji wa heshima, alipaswa kuwaita mmoja baada ya mwingine na kuwaeleza kuwa
hapandezwi na mwenendo wao katika mambo kadhaa wa kadhaa huku akiwatajia.
Pia,
Jaji Mkuu kitendo cha kutamka hadharani kuwa siku zao zimekwisha ni kitendo
kibaya ambacho sawa na laana kama ile ya mila ya waswahili, ambapo watu wabaya
wanaweza kutumia kosa hilo na kuichafua taswira ya mahakama na hata kwake Jaji
Mkuu mwenyewe binafsi. Baya likitokea katika hili, Jaji Mkuu anaweza kuanza
Kusontwa Kidole ambalo si jambo jema, bali Mzee huyu natamani awe bize na kutoa
hukumu za haki huku akisimamia mahakama zetu kutoa hukumu za haki.
Ushauri
wangu kwa Jaji Mkuu, Mzee wetu Ibarahimu Juma ni kuwa kwa kumbukumbu zilizopo inaonesha
amezaliwa Juni 15, 1958, leo hii tunaweza kusema ana miaka 63 ambayo ni utu
mzima. Nina imani tangu Jaji Mkuu alipoanza kazi na mahakama amekutana mambo
mengi makubwa na mazito zaidi ya hili analolalilalamikia.
Lakini
Jaji Mkuu atambue kuwa hawahawa anaowalalamikia, kesho ndiyo wanakuja kuwa
viongozi wa mahakama zetu, maana mbaya wa leo ndiye mzuri wa kesho. Hawa hawa
ndiyo majaji wetu wa kesho. Wanapokosea waitwe, wakanywe lakini hilo litatoa
nafasi kuishi kwa amani kwa pande zote mbili wale wanaotazamwa kama wakosaji wa
leo na wale viongozi wa mahakama wa leo. Leo hii ukiwaita, ukiwakanya, na
kuwafinya kidogo kidogo na kesho ndiye majaji wetu ndipo alipo Jaji Mkuu wetu
wa kesho. Wale mawakili wanaotazamwa kuwa wakorofi wakiitwa watajua makosa yao
na nadhani wataelewa tu.
Binafsi
nina imani kuwa Jaji Mkuu mwenyewe amepitia vipindi mbalimbali katika kazi hiyo
hadi kuwa na cheo hicho. Kama ni hivyo basi kauli hizo nzito nzito zinapaswa
kuepukwa na kuwalea vizuri mawakili wa serikali, mawakili binafsi, mahakimu
wetu wote kwa ngazi zote na zinapopatikana fursa kama za kuwa majaji zitolewe
kwa haki bila ya kupendelewa kundi lolote. Kwa leo niishie hapo, nakutakia siku
njema.
0717649257
Hakuna maoni
Chapisha Maoni