Uwekezaji wapaa Tanzania
Na
Beatrice Sanga-MAELEZO
Baada ya Tanzania kupata Uhuru Mwaka 1961, Sera za Uwekezaji za
Tanzania Bara zilihamasisha uwekezaji wa sekta binafsi, ikiwa ni ni pamoja na
kutunga Sheria ya Kuhamasisha Uwekezaji wa Kutoka Nje ya nchi (Foreign
Investment Protection Act), ya Mwaka 1963 hadi ilipofika mwaka 1967
ilipotangaza Azimio la Arusha ambapo Serikali ilisimamia na kuendesha shughuli
kuu za uzalishaji, na kusababisha mvuto mdogo wa uwekezaji binafsi ikiwemo ule
wa kutoka nje
“Tunataka tuendelee kushughulika na umaskini wa watu wetu, tushughulike kwa dhati na matatizo ya wananchi ya uchumi wao, hali yao ya uchumi, hali yao ya viwandani, hali yao ya mashambani, hali yao ya shuleni, hali yao ya hospitalini.”
Ni moja ya kauli ya baba wa taifa Hayati Mwalimu Julius Kambarage
Nyerere, juu ya serikali kuwekeza nguvu katika kutatua changamoto za wananchi
ili kuondoa umaskini na kujenga taifa la watu huru kifikra na kiuchumi.
Hayati Mwalimu Nyerere aliamini kwamba ili uwe na taifa huru ni
lazima watu wake wawe huru kiuchumi, kijamii, na kisiasa kuliko kutegemea misaada
kutoka nchi zilizoendelea, na ndio maana alijikita katika kujenga jamii huru
kwa kuanzisha ujenzi wa vijiji vya ujamaa, ili kuwaleta watanzania pamoja na
kuweka msingi wa kushirikiana katika uzalishaji na uwekezaji.
Uwekezaji huu ulienda sambamba na ujenzi wa miundombinu, ili
kurahisisha usafirishaji na usafiri wa bidhaa na watu kutoka sehemu moja hadi
nyingine.
Baada ya kumaliza muda wake mwaka 1985 alipotangaza kung’atuka
mwenyewe kutoka madarakani, Rais mwinyi alikamata usukani na kuanzisha sera za
ushirikiano na mataifa ya nje katika uwekezaji ambapo ni wakati wa Mwinyi
aliporuhusu biashara huria (Mzee wa
Ruksa) ubinafsishaji na ushindani katika huduma za kijamii (Cost Sharing) ikiwa ni wakati ambao
huduma zote ambazo zilikuwa zinatolewa bure wakati wa Hayati Nyerere zilianza
kulipiwa na uwekezaji katika sekta mbalimbali uliongezeka.
Mwaka 1995 serikali ya Mkapa iliingia madarakani ambapo iliongozwa
na sera ya ukweli na uwazi
Wakati alipohojiwa na Mwandishi wa kituo cha radio cha Deutsche
Welle Petra Stein hayati Benjamin Mkapa wakati wa utawala wake kuhusu uwekezaji
alisema, “Hatuna mpango maalum kwa
wawekezaji kutoka Ujerumani, lakini kwa jumla kwa wawekezaji wote kutoka nje
tumeandaa mazingira ambayo wenye nia wanaweza kuwekeza kwa faida yao lakini
vile vile kwa maendeleo kwa nchi yetu.”
Aidha hayati Benjamini mkapa alianzisha Sheria ya Uwekezaji, kwa
ajili ya Wawekezaji wa Ndani na wa Nje pamoja na kuanzisha Kituo cha Uwekezaji Tanzania
(TIC) ambacho kinafanya kazi mpaka sasa.
Matokeo ya uwekezaji wa hayati Mkapa ni kwamba mapato yaliongezeka
karibu mara tatu kutoka dola 612,587 mwaka 1995 na kufikia dola 1,796,862 miaka
kumi baadae ya utawala wake.
Mwaka 2005 hayati Mkapa alikabidhi kijiti kwa Rais wa Awamu ya nne
Dr. Jakaya Mrisho Kikwete, ambaye alikuja na sera ya kilimo kwanza akiwa na
lengo la kuhimiza uwekezaji katika Sekta ya Kilimo ikiwa kwa wakati huo
watanzania asilimia 80 walikuwa wanategemea kilimo kwa uti wa mgongo wa taifa.
Sera hiyo ilihimiza Serikali kuwekeza katika kilimo cha kisasa ili
kukuza soko la bidhaa za ndani kutokana na uzalishaji viwandani,
Sera hii ilienda sambamba na uimarishwaji kwa sekta zingine
ikiwemo miundombinu, ambapo kulishuhudiwa kuongezeka kwa mtandao wa barabara
nchi nzima, kuongeza upatikanaji wa umeme kwa kujengwa kwa mitambo ya Songas
unaozalisha umeme wa gesi kutoka Mtwara hadi Dar es salaam
Dr. Kikwete alijenga maeneo mengi na kukaribisha wawekezaji wa
kigeni na wa ndani kwa wingi na kusababisha kukua kwa sekta mbalimbali.
Mwaka 2015 Hayati Dr. John Magufuli aliingia madarakani ambapo
alijikita katika kukuza uchumi wa nchi kwa kuwekeza zaidi katika miundombinu
wezeshi ya ukuaji uchumi na uwekezaji hapa nchini.
Siku zote hayati Dr. Magufuli aliamini kuwa Tanzania ni nchi
tajiri, “Nchi hii ni tajiri, Tanzania ni tajiri ndugu zangu kwahiyo wala tusiogope
kuyasema haya na kusimama imara katika kulinda rasilimali zetu.”
“Nchi yetu ni
tajiri nataka niwaeleze ukweli, kilichokuwa kinatusumbua ni ufisadi na wizi
kikipatikana hiki hakiendi kwa watu walengwa, lakini tulichofanya kulingana na
mazingira yaliyotengenezwa mazuri na waliotutangulia awamu ya kwanza, awamu ya
pili, awamu ya tatu, awamu ya nne sisi awamu ya tano tumetumia hayo mazingira
kuyaboresha zaidi na ndiyo maana mnaona kila kitu kiinawezekana mpaka wale
waliozoea kutunyonya wanashangaa” Alisema
Rais Magufuli
Kauli ya nchi yetu tajiri alisema mara kwa mara kuonesha ni jinsi
gani rasimali za nchi zinaweza kutumiwa katika uwekezaji na uzalishaji mali na
ukaleta tija kwa taifa.
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tangu ipate Uhuru
mwaka 1961 kupitia Awamu ya Kwanza hadi ya Sita chini ya uongozi wa Rais Samia
Hassan Suluhu imefanya juhudi mbalimbali ili kukuza uwekezaji, maendeleo ya
sekta binafsi, ushiriki wa wananchi kwenye shughuli za kiuchumi pamoja na
miradi ya kimkakati na uwekezaji Shabaha kubwa ya uwekezaji imejikita katika
kupiga vita umasikini, ujinga na maradhi.
Kupitia uwekezaji nchi yetu
imeweza kukuza ajira zenye kipato kupanua wigo wa kodi, kukuza teknolojia na
kuhamasisha matumizi ya rasilimali watu.
Tangu Tanzania ipate uhuru, Serikali imefanikiwa chukua hatua ya
makusudi za kukuza uchumi wa Taifa na kuboresha hali ya maisha ya wananchi wake
kwa kuhamasisha uwekezaji na ushiriki wa wananchi katika uchumi. Kutokana na
juhudi hizo, Serikali imepata mafanikio ikiwa ni pamoja na kuongezeka kwa
uwekezaji katika sekta mbalimbali nchini, kuboresha mazingira ya biashara na
uwekezaji, utoaji wa mikopo kwa wajasiliamali, ujenzi wa miundombinu (umeme,
reli, barabara, madaraja, n.k), utaoaji wa elimu kwa wajasiriamali, utoaji wa
huduma za kijamii (afya, elimu, n.k) na ujenzi wa vituo vya uwezeshaji.
Katika taarifa ya mafanikio katika kipindi cha miaka 60 ya Uhuru
wa Tanzania Bara iliyotolewa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu
(UWEKEZAJI), Mhe. Geoffrey Mwambe hivi karibuni jijini Dododma alisema Serikali
inaendelea kuchukua hatua nyingine za kuandaa, kusimamia na kuweka mazingira
mazuri ya uwekezaji ikiwemo Sheria, Kanuni na Maelekezo yote yanayohusu
uwekezaji ili kuhakikisha kuwa vikwazo vyote katika uwekezaji vinatambulika na
kuondolewa pamoja na kuwa na mazingira rafiki na sawa katika uwekezaji.
“Serikali itaendelea kujenga mazingira wezeshi ambayo yatasaidia
wananchi na sekta binafsi kuchangia kikamilifu katika ujenzi wa Taifa pamoja na
kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji nchini, kuimarisha miundombinu
(barabara, reli, madaraja, umeme, viwanja vya ndege) ili kupunguza gharama za
uzalishaji, kutengwa kwa maeneo ya biashara, kuongeza ushiriki wa watanzania
katika miradi ya kimkakati na miradi mikubwa ya uwekezaji, kuboresha utoaji wa
mikopo kwa kupunguza riba na masharti mengine, kutoa elimu kwa wajasiriamali na
kudhamini mikopo kwa wajasiriamali.” Alisema Mhe. Mwambe
Hakuna maoni
Chapisha Maoni