Rais Samia- Miaka 60 ya uhuru, Kiswahili kimekua kimataifa
Na. John Mapepele
Rais wa Jamhuri ya Tanzania. Mhe, Samia Suluhu Hassan kuelekea
kilele cha maadhimisho ya miaka 60 ya Uhuru leo Disemba 9, 2021 amesema Tanzania
imepiga hatua kubwa kwenye lugha ya Kiswahili.
Rais Samia ameyasema haya jana usiku Disemba 8, 2021 jijini Dar es
Salaam wakati akiwahutubia wananchi ambapo alieleza pamoja na mambo mengine
mafanikio yaliyopatikana katika kipindi cha miaka 60 ya uhuru wa Tanzania.
“Nchi nyingi zinatumia lugha za kigeni kama lugha za mataifa yao
zinazowaunganisha, inapendeza kuona kuwa tunatimiza miaka 60 tukiwa wamoja
wenye utambulisho mmoja na lugha moja ya Kiswahili inayoendelea kupata umaarufu
kimataifa siku hadi siku”. Amefafanua
Rais Samia.
Amesema wakati Tanzania ilipopata uhuru Kiswahili haikuwa lugha
inayozungumzwa na watu wote ndani ya Tanganyika bali kizazi kilichofuata baada
ya uhuru walijifunza kiswahili shuleni. Hii inafanya nchi kuwa kati ya nchi
chache zenye lugha ya taifa yenye asili ya nchi husika.
Ameongeza kuwa katika miaka 60 Tanzania imefanikiwa kushawishi Kiswahili
kuwa moja ya lugha rasmi zinazotumika
katika Jumuiya ya Maendeleo Kusini
mwa Afrika na Umoja wa Afrika.
Amesema, Shirika la Umoja wa Mataifa Sayansi na Elimu (UNESCO)
limepitisha azimio la kutenga siku ya tarehe 7 Julai ya kila mwaka kuwa siku ya
Kiswahili duniani ambapo amesema azimio hilo linaifanya lugha ya Kiswahili kuwa
kuwa ya kwanza katika bara la Afrika kutambuliwa na kutengewa siku yake rasmi.
Akiongea na Waandishi wa Habari hivi karibuni, mara baada ya
UNESCO kupitisha rasmi azimio hilo Waziri mwenye dhamana ya Utamaduni nchini,
Mhe. Innocent Bashungwa aliwataka wadau mbalimbali wa Kiswahili nchini
kuendelea kutumia lugha hiyo ili iendelee kukua duniani.
Hakuna maoni
Chapisha Maoni