Jamii yatakiwa kuacha kuwafungia ndani watoto wenye Ulemavu
Na Mussa Augustine.
Afisa Elimu Jiji la Dar es salaam Bi.Sipora Tenga ametoa wito Kwa jamii kuacha kuwafungia ndani watoto wenye Ulemavu na badala yake waache wajiunge na masomo ili wapate haki yao ya Elimu.
Katibu wa Jumuiya ya Walemavu wa ccm wilaya ya ilala Charles Temba katikati akitoa zawadi kwa wanafunzi wa makundi maalum waliofanya vizuri katika masomo yao. |
Bi. Tenga ametoa wito huo mwishoni mwa wiki wakati wa hafla ya kuwaaga wahitimu watano wa Elimu maalumu katika shule ya Msingi Viwege jijini hapa,ambapo amewataka wananchi kuachana na Mila potofu kwamba mzazi akizaa mtoto mwenye Ulemavu ni laana kwenye jamii nakuamua kuwaficha ndani.
Aidha ameipongeza Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassani kuendelea kuwajali watoto wenye Ulemavu Kwa kuwapatia chakula wanafunzi wenye Ulemavu ambao wanasoma kwenye shule zenye kitengo maalumu cha Walemavu ikiwemo shule ya Msingi Viwege na Uhuru Mchanganyiko.
"Naomba niwapongeze Sana walimu wa shule ya Msingi Viwege kwa sadaka yenu ya kujitoa kuwasaidia watoto hawa,Mungu atawalipa,Sisi walimu wa shule za Msingi Mungu pekee ndio atatulipa (Only God will pay us) amesema Bi Sipora.
Kupitia risala iliyoandaliwa na walimu wakitengo maalumu cha Wanafunzi wenye Ulemavu katika shule ya Msingi Viwege imebainisha kwamba kitengo hicho kinakumbwa na changamoto mbalimbali ikiwemo upungufu wa vyumba vya Madarasa,Shule kukosa Uzio nakusababisha Wanafunzi kuzurura hovyo nakuhatarisha usalama wao,pamoja na upungufu wa Mwalimu wa kiume kwani wapo Wanafunzi wakiume ambao wanahitaji kuhudumiwa na Mwalimu wakiume Kwa mahitaji maalumu.
"Tunaomba kujengewa vyumba vitatu vya Madarasa Kwa maana ya hatua ya Kwanza ya pili na yatatu,pia tujengewe jiko na stoo,pamoja na kuzungushiwa Ukuta kulinda usalama wa Wanafunzi ,kuongezewa Mwalimu wakiume ili kukidhi mahitaji ya Wanafunzi wa kiume imesema taarifa hiyo".
Kwa upande wake Katibu wa Jumuiya ya Chama cha Mapinduzi(CCM) ya Walemavu Bw. Charles Temba amesema kwamba Wanafunzi hao wanahitaji kusaidiwa Kwa haraka iwezekanavyo huku akidai kwamba Kwa sasa Serikali imekuwa ikiwajali watu wenye Ulemavu nakutoa haki Sawa na wengine wasio na Ulemavu.
"Tumezisikia changamoto zao sasa ni wakati wa kuiomba Serikali iwangalie Kwa jicho la huruma ,hiki ni kitengo muhimu Sana kinawasaidia vijana wetu wenye Ulemavu wa akili na viungo kujifunza stadi mbalimbali za kazi ambazo zitawasaidia kujiendesha kwenye maisha yao,sasa hatuna budi kuwapongeza walimu hawa Kwa kuwalea nakuwasaidia kupata maarifa" amesema Temba.
Nae Mwenyekiti wa Jumuiya ya CCM ya Walemavu Wilaya ya Ilala Makamba Bilali amemuomba Rais Samia Suluhu Hassani akiwa ndio mlezi wa Taifa kuendelea na Moyo wake wa upendo kuwajali watu wenye mahitaji maalumu ili waendelee kupata haki zao za msingi.
Mkuu wa Shule ya Msingi Viwege Bi Bupe Moga amesema kwamba shule hiyo inatoa huduma ya Elimu Kwa Wanafunzi wa kawaida na wenye Ulemavu wa aina tofauti kama vile akili na viungo ambapo kwasasa kitengo hicho maalumu kimesajili Wanafunzi wapatao 51 tangu kuanzishwa kwake Mwaka 2017.
"Leo Wanafunzi watano wenye Ulemavu wa akili wanahitimu mafunzo yao Kwa mara ya Kwanza tangu kuanzishwa Kwa kitengo hiki shuleni hapa,ni jambo la faraja kwetu ,tunaomba Serikali kuzitatua changamoto zinazowakumba kama mlivyosikia kwenye risala yao walivyoeleza" amesema Bi Sipora.
Hakuna maoni
Chapisha Maoni