Zinazobamba

Diwani kata ya Saranga aeleza umuhimu wa kupinga ukatili wa kijinsia

 JAMII imetakiwa kuunga mkono jitihada zinazofanywa na Serikali, wadau na asasi za kiraia katika kupinga vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia kwa wanawake na mabinti ili kujenga jamii yenye usawa ifikapo mwaka 2022. 





Mgeni Rasmi katika maadhimisho ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia ambaye pia ni Diwani wa kata ya Saranga Mh. Edward Laizer akiongea na wanaharakati wa kata mbalimbali za jiji la Dar es slaam.

Hayo yameelezwa leo na Diwani wa kata ya Saranga Edward Laizer wakati wa mwendelezo wa siku 16 za Uanaharakati wa kupinga ukatili wa kijinsia uliokutanisha Mtandao wa Vituo vya Taarifa na Maarifa vya Kata za Wilaya ya Ubungo hafla iliyofanyika katika viwanja vya TGNP jijini Dar es Salaam.

"Ili kufanikisha zoezi hili lazima mapambano yaanzie katika ngazi ya familia kwa kuhakikisha hakuna mwanajamii anayethubutu kuonesha vitendo hivyo kwa wanawake na mabinti....Lazima tujenge jamii yenye usawa kuanzia ngazi ya familia." Amesema.

Laizer amesema kuwa Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP,) umeleta mabadiliko makubwa tangu kuanzishwa kwake hasa katika ngazi ya familia, jamii na katika ngazi ya kutoa maamuzi.

"TGNP imeleta mabadiliko  mengi kubwa zaidi ni katika kutoa elimu kwa makundi mbalimbali wakiwemo wanafunzi juu ya njia ya kuripoti matukio yoyote ya unyanyasaji wa kijinsia hasa unyanyasaji wa kingono, Serikali kupitia Halmashauri, Wilaya, Kata na Mitaa tupo nao pamoja katika hili na kila mmoja kwa nafasi yake ashiriki vita hii." Ameeleza.

Aidha Laizer ameshauri mabadiliko ya sheria ya ndoa ya mwaka 1971 ipewe nguvu zaidi ya kuangazia masuala ya usawa katika umiliki wa mali pamoja na kutambulika na kuipa heshima jinsia ya kike.

Kwa upande wake Diwani wa viti maalum  Wilaya ya Ubungo Liberata Samson ameipongeza TGNP kwa kushirikiana na Mtandao wa Vituo vya Taarifa na Maarifa katika kutoa elimu ya kupinga vitendo vya ukatili wa kijinsia.

"Vituo hivi ndiyo jamii na vinashuhudia vitendo hivyo, hatua ya TGNP kushirikiana na vituo hivi wanajamiii na waathirika wa matukio haya wanapata ahueni na pahala pa kusemea,....jamii ishiriki katika vita hii na kwa siku hizi 16 za kupinga vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia ulete mabadiliko chanya kuanzia ngazi ya familia zetu." Amesema.

Awali akitoa taarifa vituo hivyo Mwenyekiti wa  Mtandao wa Vituo vya Taarifa na Maarifa Wilaya ya Ubungo Neema Mwinyi amesema ndani ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia vituo vyote vilivyopo katika mikoa 15 nchini vitajadili mafanikio, changamoto na mwendelezo wa mpango mkakati wa kukomesha vitendo hivyo.

Amesema, Serikali imeweka sera na mikakati ya kupinga vitendo vyote vya ukatili na nguvu zaidi ni kwa jamii kushiriki kwa ukaribu katika kukemea na kuripoti vitendo hivyo.

"Tumefanikiwa kwa kiasi kikubwa kutoa elimu katika makundi mbalimbali, kutambulika katika Serikali za Mitaa, Polisi na katika madawati wa jinsia ambapo tumekuwa tukitoa elimu juu ya kupinga vitendo hivyo na jamii imekuwa na mwamko jambo ambalo linaleta matumaini ya kukomesha vitendo vya ukatili wa kijinsia ikiwemo ubakaji, ulawiti na vitendo vingine vya udhalilishaji." Amesema.

Amesema licha ya kuwa na changamoto mbalimbali ikiwemo kutoripotiwa kwa vitendo vya rushwa ya ngono vituo hivyo vimedhamiria kuendelea kutoa elimu, kuwa na mshauri katika kila Kata na Mtaa pamoja na kushirikiana kwa ukaribu na Serikali na wadau katika kukomesha vitendo vya ukatili wa kijinsia.

Hafla hiyo iliyowakutanisha wadau wa Mtandao wa Vituo vya Taarifa na Maarifa Wilaya ya Ubungo, Madiwani, wenyeviti wa Mitaa na wanafunzi ni mwendelezo wa siku 16 za uanaharakati wa kupinga vitendo vyote vya ukatili wa kijinsia kwa kauli mbiu ya 'Ewe Mwananchi Umejipangaje Kupinga Ukatili wa Kijinsia, Komesha Sasa.'

Hakuna maoni