Bodi TEA yaridhishwa na utekelezaji wa miradi Lindi
Muonekano wa mradi wa ujenzi wa nyumba nne za waalimu
zilizofadhiliwa na Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) katika shule ya Sekondari
Kassim Majaliwa iliyopo Wilayani Ruangwa, Mkoani Lindi. |
Muonekano wa madarasa yaliyokuwa yanatumiwa na wanafunzi katika shule ya msingi Mnimbila kabla ya ujenzi wa vyumba vitatu vipya vilivyofadhiliwa na TEA |
01. Madarasa yaliyokuwa yanatumika kwa ajili ya elimu ya awali kwenye shule ya msingi Ngwenya kabla ya mradi wa ujenzi wa vyumba vitatu vipya kupitia ufadhili wa miradi ya elimu chini ya TEA |
Muonekano wa madarasa yaliyokuwa yanatumiwa na wanafunzi katika shule ya msingi Mnimbila kabla ya ujenzi wa vyumba vitatu vipya vilivyofadhiliwa na TEA |
Ukaguzi wa mradi wa ujenzi wa vyumba vitatu vya madarasa ukiendelea katika shule ya msingi Ngwenya, mradi ambao uliipandisha hadhi shule hiyo kutoka shule ya awali na kuwa shule ya awali na msingi |
Na Eliafile Solla – TEA
Miundombinu bora ya elimu katika Halmashauri nyingi hapa nchini ni
changamoto kubwa ambayo haiwezi kuachiwa Serikali peke yake, bali kuna haja ya
kuongeza ushirikiano wa jamii katika kutatua changamoto hizo kupitia uchangiaji
wa rasilimali fedha au vifaa katika Mfuko wa Elimu wa Taifa.
Mfuko wa Elimu wa Taifa ulianzishwa kwa Sheria Namba 8 ya mwaka
2001, ili kusaidia juhudi za Serikali katika kuwezesha maendeleo ya Elimu
katika ngazi zote kwa Tanzania Bara na Elimu ya Juu kwa Tanzania Zanzibar.
Lengo la kuanzishwa Mfuko wa Elimu wa Taifa ni kuongeza nguvu za Serikali
katika kugharamia miradi ya elimu, ili kuinua ubora wa elimu na upatikanaji
wake kwa usawa katika mazingira ambayo hayafikiki kiurahisi.
Mkoa wa Lindi ni moja kati ya wanufaika wa miradi ya elimu ambayo
inafadhiliwa na Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) ambapo baadhi ya shule
zilizopata ufadhili ni shule ya Sekondari Kassim Majaliwa Wilayani Ruangwa
iliyopewa ufadhili wa ujenzi wa nyumba nne za waalimu, shule ya Msingi Ngwenya
na Mnimbila Manispaa ya Lindi, ambazo zote zilipata ufadhili wa ujenzi wa
vyumba vitatu vya madarasa.
Katika ziara ya viongozi wa Bodi ya Mamlaka ya Elimu Tanzania
(TEA) iliyofanyika wiki hii kwenye miradi hiyo, uongozi wa bodi ulionesha
kuridhishwa na hatua ya utekelezaji katika miradi yote baada ya kukuta mingi
ikiwa imekamilika kwa wakati na mmoja ukiwa katika hatua za mwisho za
utekelezaji.
Kiongozi wa msafara katika ziara hiyo Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya
TEA Prof. Bernadeta Killian aliwapongeza waalimu wa shule na viongozi wa
Halmashauri zote baada ya kupokea taarifa kuhusu miradi kwenye maeneo yao na
kulinganisha taarifa alizopokea na alichokiona uwandani.
‘‘Kwa kweli kazi mnayoifanya inaonekana ukilinganisha na thamani
ya kiasi cha fedha mlichopewa na TEA kutoka kwenye Mfuko wa Elimu wa Taifa japo
bado kuna uhitaji. Niseme tuu kwamba, Tanzania ni kubwa sana na miundombinu ya
kujifunzia na kufundishia ni changamoto hivyo tuendelee kutumia hizi zilizopo
kuongeza ubora wa elimu, alisema Prof. Killian’’.
Nae mwalimu mkuu wa shule ya msingi Ngwenya Bw. Masaninga Hussein
Twende alibainisha kwamba, mradi wa ujenzi wa vyumba vitatu vya madarasa katika
shule ya Ngwenya umeipandisha hadhi shule hiyo kutoka shule ya awali hadi
kusajiliwa na kuwa shule ya awali na msingi ingawa bado kuna uhitaji wa darasa
moja na nyumba za waalimu.
Aliongeza kuwa, kabla ya ujenzi wa vyumba hivyo wanafunzi walikuwa
wanaletwa kusoma hapo madarasa ya awali kama njia ya kuwaandaa kutembea
kilomita zaidi ya mbili kuendelea na shule ya msingi hivyo kusababisha wengi
kushindwa kutembea umbali huo na matokeo yake kuacha shule.
Aidha, Masaninga alisisitiza kwamba, kupatikana kwa vyumba hivyo
vya madarasa kumeipa sifa shule hiyo kuwa shule ya msingi na sasa hivi
wanafunzi kutoka katika vijiji vya karibu wanapata fursa ya kusoma na kujifunza
ambapo kwa mwaka huu wa masomo jumla ya wanafunzi 12 walifanya mtihani wa
darasa la saba na wanafunzi 9 kati yao walifaulu na wanatarajia kujiunga na
kidato cha kwanza mwakani.
Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) inatekeleza kazi zake chini ya
usimamizi wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia huku ikisimamia dhamira ya
kutafuta rasilimali fedha na vifaa kwa ajili ya Mfuko wa Elimu wa Taifa na
kuzigawa rasilimali hizo kwa ufanisi katika maeneo mbalimbali ili kufadhili
miradi ya elimu kwa lengo la kuboresha upatikanaji wa elimu bora kwa usawa.
Hakuna maoni
Chapisha Maoni