Darasa la giza linavyogawa mikate ya akina dada
ADELADIUS MAKWEGA-DODOMA.
Kila mara tulikuwa tunaitwa katika darasa hilo maalumu na kuingia wanafunzi wote wa kike. Chumba hicho kilichokuwa na ukubwa wa kututoshwa wanafunzi wote wa kike tulijaa huku walimu wa kike wakikaa mbele na kuzungumza mengi
Nakumbuka darasa hilo lilikuwa na giza kubwa huku madirisha
yalikuwa yamezibwa yaani hata kama mtu akiwa nje akitaka kuchungulia ilikuwa
vigumu kuweza kuona waliomo humu ndani wakifanyacho.
Tulipokuwa tunaingia ndani ya chumba hiki kwanza macho yetu
yalikuwa hayaoni kitu kwa giza lakini baada ya dakika kadhaa ndipo macho yetu yaliweza
kuona vizuri maana macho yana desturi ya kuzoea mazingira ya kiza na kuona
vizuri.
Tukiwa mle ndani mwalimu wetu mkuu alikuwa miongoni mwao kwa kuwa
yeye alikuwa mwanamke, sasa mwalimu wa kike mmoja ambaye alikuwa mpole sana
alifundisha namna ya kujitunza na kujiheshimu. Nilikuwa najiuliza kwanini somo
hilo kutolewa katika chumba hicho kilicho na kiza? Lakini pia nilikuwa
najiuliza mbona somo hilo linafundishwa kwa sisi wasichana tu?
Katika shule hii nilikuwa nasoma na pacha wangu wa kiume nikawa
najiuliza mbona yeye hashiriki katika kipindi hiki? Mbona walimu wa kiume
hawashiriki katika mafunzo haya? Nilikuwa na maswali mengi mno. Hata nyumbani
hatukuwa tukitengwa na wazazi wetu, kwanini
katika somo hili?
Wakati tukifundishwa hayo, baada ya maelezo kadhaa tulitajwa
majina yetu na kila aliyekuwa akitajwa akitoka nje na kurudi darasani, kwa muda
mrefu mimi na wezangu kadhaa tulikuwa tunatajwa na kuondoka kurudi darasani
kuendelea na masomo.
Tukio hilo lilikuwa linafanyika kila mwezi na siku zilipokuwa
zinasonga nilibaini kuwa wapo ambao walikuwa wanabaki humo chumbani. Kwa hakika
nilimaliza shule hii ya msingi bila ya kupata jibu. Huku nikimshirikisha kaka
yangu ambaye alikuwa pacha nayeye alikuwa hafahamu kitu.
Mara zote nilipokuwa nikiingia katika darasa la giza tulikuwa
tunakutana mandhari ya meza moja kubwa iliyokuwa na boksi moja kubwa la rangi
ya udongo ambalo lilikuwa jirani na meza waliyokaa walimu wa kike. Boksi hili
lilikuwa si la chumba hiki kwani mara
nyingi mimi nilikuwa ndiye mfagizi wa chumba hiki kabla ya kikao. Nikienda kufagia
silioni lakini kikao kikianza lilikuwa linaletwa.
Jambo hili lilikuwa kitendawili kikubwa kwangu, nilikwenda mbali
nikiwa sasa ni darasa la saba ndipo nilipomuuliza mama yangu ambaye alikuwa
mwalimu na huku darasani tukisoma somo la uzazi niliambia kuwa wale wezangu
waliokuwa wanabaki walikuwa wanapewa mikate
ya akinadada.
Nilipoenda kidato cha kwanza, huku masomo haya yakifanyika vizuri
kabisa kwa shule ya wasichana hii ilikuwa miongoni mwa shule za umma ambapo
zilikuwa zinasimamiwa na serikali enzi za ujamaa.
Nikiwa kidato cha kwanza masomo yaliendelea vizuri. Huku kukiwa
hakuna tena darasa la chumba cha giza. Nilipokuwa kidato cha pili utu uzima
uliniingia na nilibaini kuwa katika kila mwezi matroni wa shule hii tukiwa
tunasoma alikuwa akipita bwenini
kwetu na kutuwekea sodo juu ya vitanda
vyetu kuzivicha kwa kila mmoja wetu bila ya kuomba.
Kwa wale ambao tulikuwa tumeingia utu uzima tu na kwa wale ambao
walikuwa bado vitandani mwao hawakuwekewa chochote. Hapo ndipo nilipobaini juu
ya ile mikate ya akinadada(sodo) na vikao vya darasa lile la giza la shule ya
msingi.
Haya yote ni ya wakati wa ujamaa na enzi ya elimu bure ya Julius
Nyerere kwa watoto wa kike. Kama nilivyosimulia mama mmoja. Swali ni je leo hii
haya yote yanafanyika? Je kila binti mwanfunzi wa shule ya msingi/sekondari
anayehitaji sodo anapatiwa?
Katika utafiti wangu mdogo nimebaini kuwa shule moja ya sekondari
yenye wanafunzi zaidi ya 300 ina wanafunzi 140 ambao wanapaswa kupatiwa sodo
kila mwezi huko Mkoani Tanga Tanzania. Bei ya bunda la sodo moja ni kati ya
2500-4000. Gharama ya sodo kwa mwezi kwa mabinti hao shilingi 420,000/-. Katika
sodo hizi wapo mabinti wachache wanahitaji sodo maalumu ambazo zinafahamika
kama maternity ped.
Hizi zilitengenezwa kwa akina mama wanaojifungulia. Lakini huwa
inawasaidia mabinti wenye huhitaji maalumu kulingana na hali zao za kimwili na
gharama yake huwa kati ya 15,000-20,000/-. Kwa shule yenye mabinti 140 wenye
huhitaji panaweza pakawepo hata maternity pedi 10 kila mwezi ambayo itakuwa sawa
na shlingi 200,000/- kwa wahitaji kati ya 10-14 ambayo ni asilimia 10 ya
wahitaji wote 140.
Katika suala na maternity ped ni jambo la msingi sana shule kuwa
nazo kwani wapo baadhi ya mabinti/wanawake hali hii inapowakuta wanaweza
kupungukiwa damu hadi wakabakiwa na HB 4 ambapo kwa utaratibu wa kitabibu chini
ya HB 5 anapaswa kuongezewa damu. Je mtu kama huyu ataongezewa damu kila mwezi?
Nadhani hilo ni somo lingine nitamtafuta tabibu kulijibu.
Swali ni je shule hii inapata kiasi gani kutoka serikalini kila
mwezi kama fedha ya kuendesha shule? Utafiti wangu unabaini kuwa kwa mwezi
shule hii inapata kati ya shilingi 300,000-400,000 ya fedha zote za uendeshaji
wa shule. Fedha hiyo ni kwa mahitaji yote ya shule ikiwamo chaki na vifaa
vingine. Kwa mujibu wa miongozi ya fedha hizo zinazotajwa kuwa za elimu bure
asilimia 10 yake ni shilingi kati 30,000-40,000 ndiyo inapaswa kutumika kwa
Huduma za Afya Shuleni. Huduma za Afya ikiwamo dawa za chooni, Sanduku la
Huduma ya Kwanza na Sodo(ped). Nimebaini kuwa mwalimu mkuu anachokifanya ni
kununua sodo(ped) chache za dharura na kuwepo katika sanduku la huduma ya
kwanza tu. Hoja si ya kuwagawia wahitaji
kila mwezi ambayo ni sawa sawa na hakuna.
Hoja ni kwamba pesa inayopelekwa shuleni ni ndogo kwa kuwa sasa
Waziri wa elimu ni mwanamke, waziri wa TAMISEMI ni mwanamke na Rais pia ndivyo
hivyo. Haya ndiyo mambo yanayopaswa kufanyiwa kazi kwa haraka. Upelekaji wa pesa
za elimu bure ufanyike kwa wakati na pesa ziwe za kutosha maana ndani ya hawa mabinti wa leo wamebeba vizazi
vyetu vya kesho. Nakutakia siku njema.
0717649257
Hakuna maoni
Chapisha Maoni