Waziri Bashungwa apongeza ubunifu wa Dkt. Abbasi
Bashungwa |
Adeladius Makwega -Dodoma-WUSM.
Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo (WUSM) Mhe. Innocent
Bashungwa amewataka watumishi wa umma kufanya kazi kwa bidii ili kuhakikisha
wanatimiza malengo ya Serikali inayosimamiwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Samia Suluhu Hassan katika kuijenga Tanzania Mpya.
Mhe. Bashungwa ametoa kauli hiyo leo, Novemba 19, 2021 kwenye
kikao kazi na watumishi kikiwa ni kikao
cha kwanza tangu Wizara mpya ya Utamaduni, Sanaa na Michezo kuundwa rasmi hivi
karibuni na Mhe. Rais ambapo kimejadili utekelezaji wa majukumu ya Wizara akiwa
na Naibu wake, Mhe. Pauline Gekul, Katibu Mkuu, Dkt. Hassan Abbasi jijini
Dodoma
Amempongeza Katibu Mkuu wa Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa kuwa mbunifu
ambapo amesema tayari uongozi wa Wizara umekaa pamoja na kujipanga ili kufanya
kazi vizuri.
Waziri Bashungwa ametumia fursa hiyo kumshukuru Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhui Hassan kwa kutoa fedha takriban bilioni
22 kwa ajili ya ujenzi wa jengo la Wizara katika Mji wa Serikali Mtumba na
kumuagiza Katibu Mkuu Dkt. Hassan Abbasi kuhakikisha jengo hilo limajengwa kwa
ubora ambao utasaidia watumishi kuleta tija katika utendaji wao wa kila siku wa
kuwahudumia watanzania kupitia sekta za Utamaduni, Sanaa na Michezo.
“Tuendelee kubuni vitu mbalimbali na tujiratibu vizuri ili tuweze
kuwaratibu vizuri wadau wetu, tushirikiane kwa pamoja watumishi na viongozi
hatua inayosaidia kufikia malengo ya Serikali” amesema Mhe. Bashungwa.
Mhe. Bashungwa ameongeza kuwa Wizara yake ipo mstari wa mbele na
imefanikiwa kupiga hatua kwa kuzingatia msukumo wa kiasia ambao Serikali ya
Awamu ya Sita inatoa kwa Wizara hiyo kwa kuzingatia umoja na mshikamano wa
watumishi ambao unaifanya Wizara hiyo kusonga mbele.
Baadhi ya mafanikio hayo ni kuanzishwa kwa Mfuko wa Utamaduni na
Sanaa, Mfuko wa Maendeleo ya Michezo, kupunguzwa kodi ya VAT kwa nyasi bandia
kwenye viwanja vya Michezo, kurejeshwa kwa Taifa Cup pamoja na kurejeshwa kwa
michezo ya Shule za Msingi (UMITASHUMTA) na Sekondari (UMISETA).
Aidha, amesema Wizara yake itaendelea kushirikiana na wizara nyingine
kama TAMISEMI, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ili kuhakikisha kuwa sekta
za Utamaduni, Sanaa na Michezo zinafanikiwa.
Akizungumza katika kikao hicho, Naibu Waziri. Mhe, Pauline Gekul
amesema kwa sasa nguvu ya Wizara zinaelekezwa katika sekta tatu zilizosalia
baada ya kuondolewa kwa Sekta ya Habari ili ziweze kufanya vizuri zaidi.
“Mimi kama Naibu Waziri nitaendelea kushirikiana na Waziri wangu
Mhe. Bashungwa, Katibu Mkuu na Watumishi wote ili kutekeleza Ilani ya CCM, kwa
kuwa Wizara hii inagusa vipaji vingi vya Watanzania kazi yetu ni kuviunganishwa
ili kupata fursa mbalimbali ndani na nje ya Tanzania yetu.” Amefafanua Mhe.
Gekul
Awali Katibu wa Wizara hiyo, Dkt. Hassan Abbasi ametoa taarifa ya
utekelezaji wa shughuli zote hususani kupandishwa madaraja, kulipa malimbizo ya
madai, ununuzi wa vifaa mbalimbali ikiwamo magari ambayo yatawawezesha
watumishi zaidi 182 kufanya kazi vizuri.
“Tumefanikisha watumishi 66 kulipwa malimbikizo ya sehemu ya madai
yao na watumishi waliosalia wanaodai zaidi ya milioni 90 watalipwa stahiki zao,
pia watumishi watapandishwa madaraja ambapo mpaka sasa watumishi 74 tayari
wameshapandishwa madaraja na kulipwa nyongeza za mishahara yao.”
Katika kikao hicho watumishi kadhaa walipata nafasi ya kutoa ushauri,
maoni na kuuliza maswali mbalimbali ambayo yalipokelewa na kupatiwa majibu
ambayo yanafanya utekelezaji wa majukumu ya Wizara ipasavyolijibiwa.
Hakuna maoni
Chapisha Maoni