Zinazobamba

Waislamu tulizembea mikopo ya halmashauri za Wilaya- Msomi




Mtaalamu na mbobezi katika masuala ya fedha ya Kiislamu, Sheikh Khalfani Abdallah amewashauri Waislamu kushughulikia kero zote zilizowafanya kushindwa kuchangamkia fursa ya kuchukua mikopo ya Halmashauri ambayo hutolewa bila riba kwa wanawake, vijana na walemavu hapa nchini.

Akizungumza hivi karibuni, mtaalamu huyo wa fedha alisema waislamu hatukufanya vizuri sana katika kuchangamkia fursa ya mikopo ya halmashauri na kwamba bado sababu hazijajulikana kwa nini kumekuwa na kusuasua kwa watu wetu.

“Nataka niseme hapa kwenu nyie viongozi wa taasisi zetu, mpo hapa viongozi wa misikiti, mashule na taasisi, hapa nchini kwetu kuna fursa ya mikopo ya serikali, zile ni kodi zetu tunapaswa kuzichangamkia na kama tunaona zinashubuhati basi tutoke tuseme ili wanaohusika wajue kwa nini waislamu hawashiriki kwenye kuchukua fedha hizo za mikopo,” alisema Sheikh Khalfani.

Alisema kuendelea kukaa kimya ni sawa na kubariki jambo liendelee, maana hakuna atakayejua kwa nini jamii ya kiislamuwengine haijitokezi kuchukua mikopo hiyo kwa lengo la kujiletea maendeleo.

Aidha pia amewashauri kuchunguza katika taasisi za umma namna wanavyotoa mikopo yao ikiwezekana kama haiendani na matakwa ya dini yao basi watoe njia mbada ili nao waislamu wanufaike na mikopo ya serikali.

Kuna Taasisi nyingi za umma zinakopesha lakini ushiriki wa waislamu umekuwa mdogo sana, tufahamu kuwa zile ni pesa za serikali na zinapaswa zinufaishe jamii yote bila kubagua dini, sasa sisi kama tunachangamoto tunaziona ni vizuri tukakaa nao kitako kuwaeleza njia wanazoweza kufanya ili na sisi waislamu tuweze kufaidika.

“Tunajua kuwa watoaji wa mikopo wanahitaji kupata faida, maana wanagharama mbalimbali wanazotakiwa kuzishughulikia ikiwamo kulipa mishahara, kuendesha ofisi, kulipa tozo mbalimbali, kwa hiyo lazima wawe na utaratibu wa kupata faida na katika uislamu biashara haijakatazwa, tuwaambie wale wanaotoa mikopo njia nzuri ya kiislamu itakayowavutia waislamu wengi kuchukua mikopo,” alisema

Vile vile amewataka wasomi wa dini ya kiislamu kuacha kukashifiana kwa sababu ya hitilafu chache za kimtizamo, suala likionekana limepiganiwa na kiongozi wa kiislamu hadi serikali wakaamua kuliwekea mfumo ili waislamu wanufaike tuwe na utaratibu wa kulipokea na kulifanyia kazi

“Kuna vitu vingine huwa vinatuzibia tusisonge mbele kimaendeleo kama waislamu, unaweza kukuta kuna jambo zuri limefanywa na viongozi wa kiislamu lakini anakuja anatokea mtu anapuuza jitihada zilizofanyika, tena anakwenda mbele anawaambia waislamu wasitumie pengine huduma yenyewe, we unadhani serikali inawachukuliaje?, kama nyie wenyewe mnagombana nani atawasaidia

Ndio mwanzo wa kufuta hata huduma yenyewe na wakabaki na mfumo wanaoutaka wao, jambo ambalo ni hsara katika jamii ya kiislamu,” alisema Khalfani.

Kuhusu zile taaisi za serikali ambzo zinatoa mikopo lakini wanatoa kwa riba, na tunajua wazi wanatumia kodi zetu katika kufikisha huduma hizo basi sisi kama viongozi wa kidini tunatakiwa kulisema bila woga, tuwaandikie hata barua kuwajulisha changamoto zetu ili nasi tupate fursa ya kuchukua mikopo yao

“Msiogope ndugu zangu waislamu mkitaka usaidizi wa namna ya kuandika barua hizo, chombo chenu cha ushauri wa masuala ya fedha, CIFCA, kipo kitawasaidia katika kuweka sawa barua zenu,” aliongeza.

Hatutaki kuwa walalamikaji, ni suala la kusema tu jamani sisi hatuji kwa sababu ya riba lakini mkifanya hivi sisi tutakuja, lakini mkikaa kimya nani atasema kuwa pale kuna tatizo.

Tusiseme tu kuna riba, tuwaambie njia za kufanya ili nao waislamu waweze kushiriki ipasavyo, tusiwe waangaliaji tu, tujitahidi kuwaonyesha tatizo na njia mbadala ya kufanya, ili waislamu wengi waweze kushiriki vizuri na wakiwa huru katika imaani zao.

Miaka ya hivi karibuni, serikali ilikuja na mbinu ya kuwapa mikopo wananchi wake hasa vijana, wanawake na watu wenye ulemavu, mikopo hiyo ilielekezwa kabisa inatolewa bila riba, vile unavyochukua ndivyo utakavyoirudisha

Kila Halmashauri ilielekezwa kutenga asilimia kumi ya mapato yake ya ndani kwa ajili ya kutoa mikopo hiyo kwa makundi yaliyosajiliwa, watu wengi walikimbilia fursa hiyo lakini waislamu wanaona kama hawajaitumia fursa hiyo vya kutosha

Kufuatia hali hiyo viongozi wameshauriwa kuangalia uwezekano wa kuzitumia kila fursa ya kifedha inayojitokeza ili kuleta maendeleo kwa taasisi au muislamu mmojammoja.

Tayri Halmashauri nyingi zimeshatoa fedha nyingi kwa ajili ya zoezi hilo, wananchi wengi waliokuwa na mipango walinufaika na mradi huo.


 

 

Hakuna maoni