Waraibu wapewe kipaumbele katika mikopo ya Halmashauri-Dkt Mollel
NAIBU Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel amezishauri halmashauri zote hapa nchini katika mikopo yao ya asilimia 10% wahakikishe watoa kipaumbele kwa waraibu ili na wao waze kujikita katika shughuli za uzalishaji.
Pia ametoa wito kwa Taasisi za Serikali na wadau wa maendeleo kuwasaidia waraibu waliotoka kwenye matumizi ya dawa za kulevya kwa hali na mali ili waweze kuanzisha shughuli za kiuchumi na kuepuka kurudi katika matumizi ya dawa za kulevya.
Dkt. Mollel ametoa rai hiyo akiwa Jijini Tanga wakati akihikitimisha shughuli za Kampeni Maalum ya Kujenga uelewa kwenye Jamii kuhusu udhibiti wa matumizi ya dawa za kulevya katika Jiji hilo pamoja na Wilaya ya Muheza.
Amesema katika mikopo ya halmashauri inayotolewa kwa vijana, wanawake na watu wenye ulemavu ni vizuri watu wenye uraibu wakapewa kipaumbele
Dkt. Mollel amesema Mkoa wa Tanga unashika nafasi ya Pili kwa kuwa na idadi kubwa ya waraibu wa madawa ya kulevya ukitanguliwa na Jiji la Dar es salaam.
“Takwimu za mwaka 2016 zinaonyesha Mkoa Tanga una zaidi ya waathirika 5190 huku Mkoa wa Dar Es Salaam ukiongoza kuwa na warahibu wengi wa dawa za kulevya.
Kampeni hiyo iliyoanza Mei, 2021 na kuhitimishwa Oktoba 2021 imeweza kuwafikia waraibu 879 ambao katik yao 63 wameweza kuanzishiwa dozi ya Methadone katika Kliniki iliyopo katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Bombo huku waraibu wengine wakiendelea kuongezeka kutaka kuanza kupata huduma ya methadone.
Aidha Dkt. Mollel amewashukuru waratibu wa kampeni hiyo pamoja na Walimu wa Shule za Msingi na Sekondari walioshiriki katika kutoa elimu ya athari za dawa za kulevya kwa zaidi ya wanafunzi 7000 katika Wilaya ya Muheza pamoja na wanafunzi zaidi 20,000 katika Jiji la Tanga.
Kampeni hiyo ilidhaminiwa na Shirika la Cassa Familia Rosetta pamoja na Shirika la Umoja wa Kimataifa la Kuzuia Dawa za Kulevya na Uhalifu (UNODC).
Hakuna maoni
Chapisha Maoni