Tanzania yapokea dozi 499590 ya Pfizer
Serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya
Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imepokea Dozi 499,590 za Pfizer ikiwa ni
mwendelezo wa mkakati wa Serikali wa kuwakinga Wananchi dhidi ya ugonjwa wa
UVIKO-19.
Hafla fupi ya mapokezi imefanyika Novemba 23, 2021 na kuongozwa na
Waziri wa Afya Dkt. Dorothy Gwajima katika uwanja wa ndege wa Kimataifa wa
Julius Nyerere, Jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na baadhi ya viongozi
wa Serikali, Ubalozi na Taasisi zisizo Zakiserikali.
Akizungumza katika hafla hiyo, Dkt. Gwajima amesema, Serikali
kupitia Wizara ya Afya imelenga kuwakinga jumla ya Watanzania 249,795 kutokana
na kupokea Chanjo dozi 499,590 za Pfizer zilizoingia kutoka Marekani kupitia
mpango wa COVAX Facility.
“Leo Novemba 23, 2021 tumepokea dose 499,590 za Pfizer ambazo zitakinga
watanzania 249,795 (dose mbili).” Amesema Dkt. Gwajima.
Chanjo hizi kama zilivyokuwa za Janssen na Sinopharm zimethibitishwa na
WHO kuwa ni bora na salama, huku akisisitiza Wizara ya Afya itafanya
wajibu wake wa kujiridhisha na uhakiki wa ubora wa Chanjo hii kwa kupitia
wataalamu wa ndani na Mamlaka husika kabla ya kuanza kutolewa kwa Watanzania.
Aliendelea kusema kuwa, Hadi kufika kufikia tarehe 19.11.2021, takwimu
zinaonesha kuwa jumla ya wananchi ,359,624 tayari wamepata chanjo ya
kuwakinga dhidi ya UVIKO-19.
Aidha, Dkt. Gwajima amewaagiza Viongozi na Watendaji wa ngazi zote
kutoa ushirikiano wa hali ya juu ili kuhakikisha kuwa wananchi wanaelimishwa
kwenda kupata chanjo ili kujikinga dhidi ya UVIKO-19.
“Ninawaagiza Viongozi na Watendaji wa ngazi za Mikoa na Halmashauri
kutoa ushirikiano wa hali ya juu ili kuhakikisha kuwa wananchi wanaelimishwa
kwenda kupata chanjo ili kujikinga dhidi ya UVIKO-19. ” Amesema. Gwajima.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa huduma za Afya na Ustawi wa
Jamii na Lishe OR TAMISEMI Dkt. Paul Chawote amewashukuru Wadau kwa kuendelea kushirikiana
na Serikali katika kuboresha afya ya wananchi, huku akisisitiza kuwa Serikali
itaendelea kushirikiana nao katika kuketa Maendeleo hususan katika sekta ya
afya.
Nae, Balozi wa Marekani nchini Tanzania Dkt. Donald J. Wright amesema,
nchi ya Marekani ndani ya kipindi cha miongo miwili imeendelea kuwa kinara
katika kusaidia nchi za Afrika ikiwepo Tanzania katika kuboresha Sekta ya Afya
hususan katika kipindi hiki cha mapambano dhidi ya UVIKO-19.
Pia, amesisitiza kuwa, hakuna muda wa kulala katika kipindi hiki cha
mapambano dhidi ya UVIKO-19, ili kuwalinda wananchi dhidi ya mlipuko wa ugonjwa
wa UVIKO-19 ni lazima Elimu ya umuhimu wa chanjo iendelee kutolewa kisha watu
wachanje. Amesema.
Hakuna maoni
Chapisha Maoni