NINAYOYAKUMBUKA SAKATA LA VYETI FEKI
Adeladius Makwega-Dodoma.
Tulimaliza zoezi hilo mapema
na kwa kuwa nilikuwa mgeni nilikuta kazi hiyo imeshamalizika na wale walioshiriki
waliniambia kuwa zoezi limekamilika vizuri na majina kadhaa yamebainika kuwa
wana vyeti feki. Miongoni mwa majina hao walikuwepo watumishi wawili. Nao ni
mke wa mheshimiwa mmoja na ndugu mmoja ambaye alikuwa Bwana Shamba.
Kati ya watumishi hao wawili
mmoja alikuwa mke wa mheshimiwa kwa kuwa alikuwa mke wa mkubwa nilitaka kubaini
je cheti hicho kilikuwa feki au halali? Niliomba nakala ya vyeti hivyo lakini
wahusika waliniambia kuwa mkuu, kwa suala la nakala unapoteza muda kuangalia
kwa kuwa hawa wenye vyeti feki wote vyeti vyao vya original/halisi vyote tuliwaagiza
wavilete na vipo hapa njiani kwenda Baraza la Mitihani.
Mhusika aliyekuwa navyo
aliniletea na kunieleza shida la cheti hicho. Kwa kukitazama kwa macho ya
kawaida tu kilibainika kuwa kuna sehemu imeandikwa This certify that ………alafu
linakuja jina lake aliyechapa hakuweza kulenga vizuri. Kwa desturi ya kompyuta
lazima maandishi hayo yangekuwa yanafutana vizuri lakini haya hayakufuatana
vizuri kwa hiyo cheti hicho kilikuwa ni manila tu. Pia aliyekuwa ananiongoza kufanya
uhakiki huo aliniambia kuwa hata kwenye kumbukumbuku ya shule hiyo anayodaiwa
kusoma mke huyu wa mheshimiwa jina hilo halikuwepo.
Aliniambia kuwa hata Baraza la
Mitihani la Taifa nao walithibitisha hilo. Sasa swali lililopo huyu ni mke wa
mheshimiwa inakuwaje? Kwa hakika zoezi hilo la vyeti feki lilikuwa la haki na
hakuna aliyeweza kupindisha labda kwa bahati ya Mungu tu. Binafsi niliamua
kumtuma bwana mmoja nikimuagiza amjulishe mheshimiwa juu ya cheti hicho feki
cha mkewe. Japokuwa mheshimiwa aliambiwa lakini hakuamini nilichomueleza.Kwa
hekima zangu niliona si vizuri kumvua nguo mheshimiwa hadharani.
Katika mashauriano na
wezangu tulikubaliana kuwa ili kuficha siri ya mheshimiwa huyu basi ufanyike
utaratibu wa kumpeleka eneo lingine kwa kuwa alikuwa na cheti feki. Basi umma
unaweza kuona kuwa mke wa mheshimiwa alihamishiwa mbali na kwa kuwa uhamisho
huo ni mbali ameamua kuacha kazi mwenyewe na hilo litaweza kuficha ile hoja ya
mke wa mkubwa kuwa na cheti feki. Mheshimiwa huyu kwa upande ni nimeposa dada
yake lakini kwangu mimi yeye ni mheshimiwa sana.
Hilo lilifanyika vizuri na
uhamisho ukatolewa lakini mheshimiwa huyu hakuelewa kabisa alisema kuwa
kunafanyika uonevu dhidi ya mkewe na kibaya zaidi alisema kuwa suala la vyeti
feki kwa mkewe ni kisingizio tu. Malalamiko yalikuwa makubwa sana. Huku mheshimiwa
huyu alifanya kila linalowezekana kupambana na hoja ya uhamisho wa mkewe.
Hali ilipokuwa mbaya zaidi,
wakubwa juu yangu waliniuliza hapo limekaaje? Nilieleza hoja hiyo vizuri basi walisema
kama bado anang’ang’ania hilo basi mrudishe mkewe alipokuwa, kweli sikuwa na
pingamizi kwa hilo mke wa mheshimiwa alirudishwa katika kituo cha kazi cha
awali.
Mheshimiwa Magufuli mara
baada ya kamati yake kumaliza kazi ambayo ilikuwa inasimamiwa na Waziri wa
Utumishi wakati huo Bi Angela Kairuki alitoa majina ya wenye vyeti feki likiwamo
jina la mama huyu na kuondolewa katika utumishi wa umma pamoja na ndugu Bwana
Shamba. Mheshimiwa hakuwa na hoja nyingine lakini kisiasa alisimamia hoja kuwa
mkewe ameonewa katika sakata hilo la vyeti feki.
Je ni kweli mimi kama msimamizi
wa taasisi niliweza kufanya uonevu huo ambao ilikuwa kazi iliyokuwa
ikisimamaiwa na Magufuli mwenyewe?
Katika sakata hilo pia
alikuwepo mtumishi mmoja ambaye alikuwa Bwana Shamba kama nilivyokwambia hapo
awali, mtumishi huyu alikuwa na uwezo mkubwa wa kufanya kazi lakini aliingia
katika sakata la vyeti feki kwa bahati mbaya kwani uwezo wake wa kiakili
ulikuwa mkubwa sana na hata nilipobaini kuwa nayeye yumo katika shida hilo
moyoni mwangu nilihuzunika sana. Kwani uwezo wake wa kufanya kazi ulionekana
kwa vitendo katika kazi zake alizokuwa akifanya, alikuwa anajiamni. Taasisi
yoyote lazima kumpenda mtumishi kama huyu.Kama malengo ni kufika mbali.
Wale waliokuwa
wakishughulikia hilo waliniambia kuwa ndugu huyu alipata ajira baada ya
kuhudhuria mafunzo ya masuala ya kilimo. Lakini cheti chake cha kidato cha nne
tangu alipoombwa kukileta hakikupatikana na nakala hiyo taasisi niliyokuwapo hawakuipata.
Agizo la vyeti feki
lilipotolewa ndugu huyu aliondolewa kazini, nilijaribu kumuita ndugu huyu
alifika katika ofisi niliyokuwepo na kunieleza mengi.
“Kuwa ni kweli nilisoma hadi
kidato cha nne miaka ya 1980 katikati, Shule ya Sekondari ya Mzumbe Mkoani
Morogoro na nilifanya mtihani huo vizuri na kuhitimu.”
Wakati akiwa shuleni ndugu
huyu alikuwa akifanya kazi kama mtunzaji wa stoo ya shule yaani (Store Keeper)
kwa wale waliosoma shule za bweni wanafunzi wanakabidhiwa majukumu kama hilo kwa
kuaminiwa, huku wengine mnapoenda kulima hawa huwa na kazi hiyo ya utunzaji wa stoo.
Utakuta wengine walipokuwa shuleni walikuwa wauza duka la shule, watunzaji wa
mabanda ya ng’ombe na kadhalika kwa hiyo ni sehemu tu ya maisha ya shuleni na
walimu wanafanya hivyo kuwafundisha kazi wanafunzi.
Wakiwa katika harakati za
mitihani ulitokea upotevu wa vifaa katika stoo hiyo kwa hiyo ilileta usumbusu mkubwa.
Ikiaminika kuwa aliyekuwa Mkuu wa Shule ya Mzumbe wakati huo aliandika barua
Baraza la Mitihani juu ya kuzuiliwa kwa matokeo ya mwanafunzi huyo hadi shauri
lake litakapo kamilika.
“Kweli matokeo ya kidato cha
nne wezangu wote niliofanya nae mtihani huo yalitoka isipokuwa mimi na ndiyo
maana hadi wakati wa vyeti feki vya Magufuli zoezi likiendelea sikuwa na cheti
mkononi au katika faili langu.Tangu wakati huo nilipomalzia shule kila nilipojaribu
kutafuta nafasi ya kukipata cheti change nilishindwa na ndiyo maana nilishindwa
hata kujiendeleza zaidi.”
Baraza la Mitihani la Taifa
lilitoa nafasi kwa kila anayelalamika kuwa na utata wa cheti chake, kweli ndugu
huyu alifanya hivyo na mimi nilifanya mawasiliano na taasisi hiyo. Baada ya
muda wa miezi kama 15 hivi baraza walijibu kuwa ndugu huyu alifanya mtihani wa
kidato cha nne na kufaulu vizuri masomo yote na daraja la mwisho katika matokeo
hayo ambalo hufaulu wake ulikuwa mdogo ni C huu kukiwa na A na B kadhaa kwa
hakika alifanya vizuri sana.
Lakini kwa kuwa kulikuwa na
hoja ya shule juu ya matokeo yake hayakuwekuwa Division/ Daraja. Kama yangekuwa
na daraja namna nilivyoyaona anagekuwa na daraja la kwanza kwa pointi za 13/14.
Swali ni je ndugu huyu ni miongoni mwa wenye vyeti feki au kukosa feki?Ndugu
huyu alishakaa nyumbani zaidi ya miaka mwili bila kazi na bila mshahara.
Pia tambua nafasi ya Mkuu wa
Shule na maoni yake juu ya tabia ya mwanafunzi kwa Baraza la Mitihani
yalivyokuwa na athari kubwa kwa mwanafunzi huyu/Bwana Shamba.
Je suala lake lilimalizwaje?
Je kutokea kwa matatizo ya upotevu wa stoo kule shuleni sasa kumesababisha shida
zote hizo. Pengine hata huyo Mkuu wa Shule wakati jambo hili linaibuka juu ya
vyeti feki pengine ameshafariki dunia lakini kile alichoandika bado kimesimama./bado
kipo hai/bado kinaishi.Mwanakwetu kumbuka na wewe kile unachoandika juu ya
yoyote yule jitihadi kukimaliza ili ukifa kisiache majeraha kwa wengine. Natambua
Mkuu wa Shule yeye alitimiza wajibu wake tu lakini alipaswa kutambua huyu
aliyemfanyia hivyo alikuwa mwanafunzi mwenye safari ndefu ya maisha..
Kwa mwaka 2018 ilikuwa miaka
kama 34 tangu kutokea kwa shauri hilo katika Shule ya Sekondari Mzumbe. Kwa
hiyo kosa la upotevu liwe kweli kwa ndugu huyu kama alishiriki au alisingiziwa
ndani ya miaka 34 lilipaswa kuwa limemalizika kwa kila upande kutimiza wajibu
wake ipasavyo.
Mungu Bahati, mjadala
ulifanyika na Baraza la Mitihani na mtumishi huyu aliendelea na kazi na mara ya
mwisho nazungumza naye aliniambia anamshukuru Mungu alirudishwa kazini na alikuwa
anafanya mipango ili aweze kustaafu kwa miaka 55.
Hoja yangu ya leo ni kuwa
hiyo ndiyo hali ya vyeti feki wakati huo na mimi haya ninayokusimulia na baadhi
ya mengi niliyoyaona katika sakata hilo. Kwa leo ninaishia hapo nakutakia siku
njema.
0717649257
Hakuna maoni
Chapisha Maoni