Mataruma Karani Wa Mahakama
ADELADIUS MAKWEGA-DODOMA.
Kikao cha bodi ya Shule ya Sekondari
Lugoba kilikaliwa kwa nia ya kutambua hali ya maisha ya wanafunzi wa kike
ikoje, kwa wakati huo Mbunge wa Jimbo la Chalinze alikuwa Ndugu Jakaya Kikwete.
Kikao cha siku hiyo kilijumuisha wazazi kadhaa wenye watoto katika shule hiyo
ya sekondarii.
Kwa hakika kikao kilikuwa
cha wazi na ukweli huku wazazi na bodi ya shule wakikubaliana kwanza kuwatambua
watu ambao walisababisha watoto wa kike kutokuwa na tabia nzuri shuleni na
jambo hilo kusababisha wanafunzi wasichana wengi kuharibikiwa na kutomaliza
shule iwe kwa tabia mbaya na kupata ujauzito.
Mwenyekiti wa bodi hiyo ya
shule ambaye jina lake silikumbuki kwa sasa, alimua kuwa wazazi wawataje watu
wote walionekana kuwa ni viranja wa kuwaharibu mabinti katika shule hiyo.
Majina kadhaa yalitajwa huku
mkuu wa shule hiyo ambaye nayeye silikumbuki jina lake kwa sasa, ambaye alikuwa
katibu wa bodi ya shule hii na katibu wa kikao hiki. Kikao hicho kilikuwa cha
jazba na hasira kutoka kwa kila mzazi kwani takwimu zilizosomwa na mkuu wa
shule juu ya mabinti waliopata ujauzito zilikuwa sawa na moto uliokuwa ukiwaka
katika ukoka wa majani makavu.
Mkuu wa shule aliendelea
kunakili kila jina lililotajwa. Yapo majina yaliyotajwa mara moja lakini yapo
yaliyotajwa mara nyingi. Kwa desturi vijijini huwa hakuna siri hata kama kuna
siri mambo yanapowafika shingoni wenye kijiji chao lazima wataibuka na kusema
juu ya jambo hilo ambalo linawakera, ndivyo ilivyokuwa siku hiyo.
Katika kikao hiki mimi
nilishiriki tu kama raia mwema lakini nilikuwa mwanahabari pekee ambaye
nilishiriki kikao hicho kwa bahati mbaya tu bila ya kupata mwaliko huo. Lakini
kwa kuwa nilikuwepo eneo hilo kama Afisa wa Serikali niliamua kusikiliza hadi
mwisho.
Ni kweli kwa takwimu ilionekana
kuwa hali ya shule hii itakuwa mbaya hivyo Mbunge wa jimbo hili alielezwa ambaye
siku hiyo hakuwepo. Pia ilibainika kuwa Subash Patel alikubaliana na Mbunge
kupeleka msaada wa magodoro kadhaa ili kuboresha mabweni ya shule hii ambayo yangesaidia
wanafunzi kuweza kukaa bwenini na kuwaepusha majanga haya.
Katika utarabu wa kikao
hicho ilishauriwa kuwa majina ya watu waliokuwa wanawarubuni watajwe kwa
kusemwa kikaoni na wengine waandike majina haya katika karatasi.
Harakati zilianza wenye
kunyoosha mkono walifanya hivyo na wale wa kuandika walifanya hivyo. Mwenyekiti
wa Bodi ya shule hii alipokea vijikaratasi hivyo na kumpatia katibu wake baada
ya kuyasoma majina yote yaliyoandikwa.
Basi majina yalitajwa bila
woga na huku wengine wakitolea mifano ya tabia ya hao waliokuwa wakitajwa.
Kikao hicho kilichukua karibu nusu ya muda wake katika zoezi la kutaja majina
haya. Kubwa nililolibainia lilikuwa ni kutajwa mara nyingi kwa jina la Mataruma
Karani wa Mahakama. Huyu bwana ndiye alikuwa kinara wa uhalibifu wa mabinti za
watu kwa mujibu wa kikao hicho ambacho bwana huyu aliangushiwa zigo la tuhuma.
Jambo hilo kikaoni ilielezwa
kuwa wazazi wengi walishalalamika muda mrefu kwa mkuu wa shule juu ya ndugu
Mataruma na tabia yake mbaya. Kikao kilielezwa kuwa mwalimu wa nidhamu shuleni hapo
anao ushahidi wa kutosha kwa wanafunzi waliopata ujauzito wa bwana huyu na
kuacha masomo ambapo wanafunzi hao waliopata ujauzitio waliungama kwa mwalimu
huyo kwa maandishi.
Kama hilo halitoshi kikaoni Mwalimu
wa Nidhamu alieleza kuwa kuna siku akiwa nyumbani kwake alibishiwa hodi na
mgeni. Alimkaribisha mgeni huyu na kumbe alikuwa ndiye Mataruma Karani wa
Mahakama, ndugu huyu alipofika nyumbani kwa mwalimu wa nidhamu alilalamika kuwa
mwalimu wa nidhamu anamfuatamfuata sana.
Mwalimu huyu alimwambia Ndugu
Mataruma kuwa tabia anayoifanya ya uharibifu wa mabinti za watu ilikuwa kero
kwa jamii wala siyo yeye anayelalamika bali watoto wenyewe walimtaja na pamoja wazazi
wa watoto hao pia.
Matarumu alimwambia mwalimu
huyu kuwa aache tabia ya kumfuatafuata. Kwa bahati nzuri mwalimu huyu wa
nidhamu alikuwa ni mtu mzima mwenye watoto wa kike na wakiume wa kuzaa mwenyewe
waliokuwa wanasoma shuleni hapo. Kwa mwalimu huyu ukiachia nafasi yake kama mwalimu
lakini pia alikuwa mazazi.
Mwalimu huyu alisema kuwa
japokuwa Ndugu Matarumu alifika nyumbani kwake kulalamikia juu ya yeye kutajwa
nilimjibu kuwa tuhuma hizo zipo. Mwalimu huyu alienda mbali zaidi anasema kuwa
baada ya Mataruma kutoka nyumbani kwake alihamishia nguvu za kuwasaka mabinti
kwa familia ya mwalimu huyu.
Ushuhuda wa binti wa mwalimu
huyu ulithibitisha kuwa karani huyu wa mahakama alijaribu kutumia fedha nyingi
angalau atimize haja zake kwa binti wa mwalimu wa nidhamu ambapo suala hilo lilielezwa
kikaoni na alieleza alikuwa mke wa mwalimu wa nidhamu ambaye nayeye alifika
kama mzazi kikaoni hapo. Mataruma Karani wa Mahakama alionywa na kuchukuliwa
hatua kali.
Kwa bahari nzuri pia Ndugu Subash
Patel aliwezesha kupatikana kwa magodoro ya wanafunzi hao na kuweza kuishi
bwenini na kuepukana na adha ya kuishi mitaani.
Hoja yangu ya leo ni moja tu
angalia namna Mataruma Karani wa Mahakama anavyohangaika kulipiza kisasi kwa
binti wa Mwalimu wa Nidhamu kwa tabia yake mbaya ambayo kwa hakika kwa hoja ya
Mwalimu wa Nidhamu inaonesha kuwa tabia ya karani huyu ilikuwa mbaya.
Lakini pia angalia shule hii
wazazi, mbunge na wadau walivyoshirikiana kuwawanusuru wanafunzi wa kike na
matatizo ya kujiingiza katika tabia hizo mbaya. Kwa hakika jamii
inaposhirikiana wanaweza kushinda changamoto zozote zile. Ebu kwa leo niishie
hapo tu, nakutakia siku njema.
0717649257
Hakuna maoni
Chapisha Maoni