Zinazobamba

WAJASIRIAMALI WA SOKO LA STOP OVER KIMARA WAPEWA ELIMU YA UTENGENEZAJI WA MBOLEA YA MBOJI NA KC SARANGA.

Wajasiriamali wa soko la Kimara Stop Over wametakiwa kuizingatia elimu waliyopewa na kituo cha Taarifa na Maarifa kata ya Saranga, ya kufainya changamoto ya takataka zinazozalishwa sokoni hapo kuwa fursa kwa kutengeneza mbolea aina ya Mboji.

Mtendaji wa Serikali ya mtaa wa Kimara Stop over Bi. Hidaya J. Mbaga akitoa ufafanuzi wa jambo katika mafunzo ya ujasiriamali mkoani Dar es salaam.

Hayo yamesemwa na Mtendaji wa mtaa wa Kimara stop over Bi. Hidaya J. Mbaga wakati akifungua mafunzo ya siku moja kwa wafanyabishara wa soko la stop over, jinsi ya kujipatia kipato cha ziada kwa kutumia rasilimali zinazowazunguka.

Aidha amewataka kuzingatia mafunzo kwa faida yao wenyewe.

“Kwa mafunzo kama haya ya ujasiriamali kuyapata kwake ni nadra sana hata ukiyapata ni lazima utalipia, lakini kwa hapa sokoni kwetu tumepata bahati ya kuletewa mafunzo haya bure hivyo tuwe makini na tusikubali kupoteza muda wetu bure bali tukae kwa faida.” amesema Mtendaji

Ameongeza kuwa fursa ya mbolea ipo kwani hata wakiweza kuzalisha watapata wateje tu kwani wataweza kuwauzia wenye bustani za mboga mboga wanaozalisha miche pamoja na maua hao wote watakuwa wateja wao na pia ni vema wakaunda vikundi ili wafanye kitu kikubwa na kizuri Zaidi.

Na mwisho amewasihi kuhakikisha wanachofundishwa ni vema wakakitekeleza kwa vitendo ili waone matunda yake, Na endapo watahitaji msaada wowote kutoka serikalini basi wamuone Mtendaji au Mwenyekiti wa mtaa na kama jambo lao litahitaji viongozi wajuu Zaidi yeye atawasaidia kwa namna yoyote ile ili waweze kufanikisha jambo hilo.

Mwanachama wa Kituo cha Taarifa na Maarifa kata ya Saranga Catherine Mwanyilu Akiongea na waandishi wa habari.

Kwa upande wake mwanachama wa Kituo cha Taarifa na Maarifa kata ya Saranga Catherine Mwanyilu amesema kuwa sababu za wao kuwepo katika soko hilo ni kuwapa elimu wajasiriamali namna ya kujipatia kipato cha ziada kupitia rasilimali zilizopo sokoni hapo.

Ameongeza kuwa hiyo ni sehemu ya mrejesho wao kwa TGNP, baada ya kupewa mafunzo julai 15 mwaka huu, ambapo walifundishwa kupitia muduli inayoitwa ABCD kutoka chou cha COADY Institute, inayowataka wao kama walaghibishi kuweza kuelimisha jamii juu ya umuhimu wa kutumia rasilimali walizonazo katika maeneo yao.

Ameendelea kusema kuwa mchakato huo wa kutoa elimu ulianza katika soko la kimara Temboni wakaenda na soko la suka na mpaka leo wapo katika soko la stop over, ambapo wamefundisha namna ya kutengeneza bidhaa mbalimbali za urembo, kusindika mboga na matunda pamoja na kuzifanya takataka kuwa fursa kwa kutengeneza mbolea ya mboji.

Mjasiriamali wa soko la Kimara Stop over Habiba Magero akitoa ufafanuzi wa jambo fulani katika semina ya wajasiriamali wa soko hilo. 

Naye mjasiriamali wa soko hilo Habiba Magero amesema mafurahishwa sana na elimu hiyo na kuliomba shirika la TGNP kwa kushirikiana na KC kata ya Saranga kuweza kupeleka elimu hiyo katika maeneo yote ya mkoa wa Dar es salaam kwa kuwa kila sehemu watu wanazalisha takataka.

Na mwisho ameitaka serikali ikiwezekana kuichukua elimu hii ili kuweza kuwakomboa vijana kupata ajira,

“Lakini pia serikali yetu ingejaribu kuichukua fursa hii kwani itasaidia halmashauri nyingi kuondokana na gharama kubwa za kusafirisha taka kupeleka kwenye madampo, na badala yake kuzihifadhi vizuri kwa ajili ya kutengenezea mbolea, Na hii itaisaidia sana serikali lakini pia vijana wataweza kupata kipato kupita hizi takataka.” amesema Habiba

Muwezeshaji wa mafunzo kutoka TGNP, Bw. Hans Obote akifundisha madhara ya ukatili wa kijinsia kwa jamii na taifa kwa ujumla.
Washiriki wakifuatilia mafunzo kwa umakini.
Mafunzo yakiendelea.
Makamu Mwenyekiti wa Kituo cha Taarifa na Maarifa kata ya Saranga Bi. Maria Mwigune akitoa ufafanuzi wa jambo fulani katika semina ya kuwajengea uwezo wajasiriamali wa soko la Kimara stop over.

Washiriki wa mafunzo wakiwa katika picha ya pamoja na mgeni rasmi ambae ni Mtendaji wa kata ya Stop over Bi. Hidaya J. Mbaga. 

Hakuna maoni