Zinazobamba

KITUO CHA SHERIA NA HAKI ZA BINADAMU CHAFANYA KIKAO KAZI NA WATU WENYE ULEMAVU, KUJADILI MAPUNGUFU YA SHERIA YA USALAMA WA BARABARANI,



Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kimewakutanisha wadau mbalimbali ikiwemo wanasheria, mawakili wa kujitegemea pamoja na viongozi wa vyama vya watu wenye ulemavu kujadili mapungufu ya sheria ya usalama barabarani.

Akizungumza leo Jijini Dar es Salaam katika kikao kazi hicho cha siku mbili kilichoratibiwa na LHRC Mratibu wa kikao hicho ambae ni Afisa program wa kituo hicho Joram Bwire amesema lengo la majadiliano hayo ni kuchambua mapungufu ya sheria ya usalama barabarani hususani kwa watu wenye ulemavu.

Aidha amesema majadiliano hayo yatahusisha uchambuzi wa sheria ya usalama barabarani ya mwaka 1973 sura ya 168 pamoja na Muswada namba 7 wa mwaka 2021 wa mabadiliko ya sheria ya usalama barabarani ambapo kumekuwepo na mapungufu ya kukosekana kwa alama za barabarani kwa watu wenye ulemavu.

Hata hivyo amesema mapungufu hayo ya sheria yamechangia ongezeko la idadi ya watu wenye ulemavu na tegemezi kutokana na ajali huku adhabu zinazotolewa kwa madereva wanaosababisha ajali hizo kuwa ndogo kuliko ukubwa wa madhara ya ajali husika.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Shirikisho la vyama vya watu wenye ulemavu Tanzania (SHIVYAWATA) Jonas Lubago amesema sheria hiyo imewaacha mbali wao kama watumiaji wa barabara wenye mahitaji maalum kwa kutokuwekwa kwa miundombinu rafiki ya kuwawezesha kutumia barabara na vyombo vya usafiri kwa usalama.

Aidha ameyataja mapungufu hayo kuwa ni pamoja na kukosekana kwa alama za barabarani kwa watu wenye ulemavu ambazo zinamuongoza dereva, sheria kutobainisha maegesho ya vyombo vya usafiri kwa watu wenye ulemavu, mabasi kutokuwa na miondombinu rafiki kwa watu wenye ulemavu na sheria hiyo pia haisemi ni nani muhusika wa kuwaelimisha watu wenye ulemavu pindi wawapo barabarani.

Hata hivyo ametaka sheria iwalazimishe wamiliki wa vyuo vya udereva kuweka mtaala ambao unatoa elimu na haki kwa watumiaji barabara wenye ulemavu pamoja na watu wenye ulemavu kujumuishwa kwenye baraza la ushauri la usalama barabarani ili haki zao zitamkwe huko kwani wengi wao wanagongwa barabarani na hakuna hatua zinazochukuliwa.

-Aidha amesema wao kama watu wenye ulemavu ambao wanakadiriwa kufikia asilimia 9 kwa Tanzania nzima bado hakujawa na bidii za makusudi kwa serikali kilizungumzia kitaifa ili kutatua kabisa changamoto hizo kwa mda mrefu na kuzifanya barabara na vyombo vya usafiri kuwa rafiki kwa watu wenye ulemavu.

Kikao kazi hicho cha siku mbili kilichoratibiwa na LHRC kimejumuisha wanasheria na mawakili wa kujitegemea pamoja na vyama vitatu vya watu wenye ulemavu ambavyo ni Shirikisho la vyama vya watu wenye ulemavu Tanzania (SHIVYAWATA) Chama cha watu wenye ualibino Tanzania (TAS) pamoja na Chama cha wasioona Tanzania (TLB).

Hakuna maoni