Serikali yawaagiza Mameneja wa Posta kuwa wabunifu
Hussein Ndubikile, Dar es Salaam
Waziri wa mawasiliano Dkt Faustne Ndungulile ametoa maelekezo kwa Mameneja wote wa Mikoa wa Shirika la Posta Nchini kuhakikisha wanakuwa wabunifu katika utendaji wao wa kazi ili kuzalisha fedha za kuendesha huduma pamoja kulipa mishahara.
Maagizo hayo yametolewa jana jijini Dar es Salaam katika Kikao Maalum cha Viongozi wa Posta cha Kutathimini mwaka uliopita na kupanga mikakati ijayo.
Amesema mameneja hao wanatakiwa
kuwa wabunifu katika utendaji kazi wa kila siku lengo likiwa kutimiza malengo
waliyowekewewa kusaidia uendeshaji wa shirika na ulipaji wa mtendaji mkuu wa
Posta,
" Nendeni mkawe wabunifu
matafute masoko ya bidhaa zenu timizeni malengo mliyojiwekea mkifaulu mtaweza
kuendesha shirika na kulipa mshahara wa mkuu wenu mkishindwa hamtoshi
kuwa hapo," amesema Dkt. Ndungulile.
Amebainisha kuwa mameneja
wanatakiwa kusimamia utoaji huduma kwa wateja bila urasimu hasahasa wanapofanya
kazi na taasisi binafsi pamoja na kuwapa mafunzo watoa huduma wa shirika hilo
ili kuendana na kasi ya mifumo ya uendeshaji ya kidijitali.
Amewasisitiza mameneja na
watendaji wa shirika hilo kubuni vyanzo vipya mapato vitakavyosaidia kuendesha
shirika pamoja na kujenga utamaduni wa kujadiliana na vyama vya wafanyakazi ili
kuondoa migogoro ndani ya Posta.
Ameongeza kuwa ifikapo mwezi
Septemba mwaka Posta na Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) wawe
wamefikia muafaka katika mgawanyo wa mali na kutangaza katika gazeti la
Serikali.
Kwa upande wake Kaimu Mkuu
PostaMasta wa shirika hilo, Macrice Mbodo amesema kikao hicho siku tano
kitahusisha utoaji wa mafunzo kwa viongozi, kupata uzoefu wa pamoja kutoka
taasisi iliyofanikiwa, kufundishwa itifaki na ustaarabu wa viongozi kutoka Chuo
cha Diplomasia, kujadili tathimini ya mwaka uliopita na changamoto, kupata
mafunzo ya kupanga malengo kutoka ofisi ya utumishi pamoja na kupata nasaha za
wakongwe wenye uzoefu wa kiposta na nje ya posta.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa TTCL,
Waziri Kindamba amewaomba mameneja kusimamia vyema mikoa yao kutoa
ushirkiano kwa Kaimu huyo ili kuhakikisha Posta inafikia malengo iliyojiwekea
kufikia hatua ya utoaji huduma kimataifa kwa mifumo ya kidijitali.
Mwakilishi wa Mkurugenzi wa
Mamlaka ya Mawasiliano Nchini (TCRA) Haroun Lemanya ameishauri menejimenti ya
Posta kujifunza kwa njia ya mafunzo wafikie kutambulika viwango vya ubora wa
kimataifa.
Mkurugenzi wa Mfuko wa
Mawasiliano kwa Wote Jastina Mashimba amesema mameneja hao wampe ushirkiano
Mbodo ili wafikie viwango vya utendaji kazi wa mashirika ya kimataifa ya huduma
za posta likiwemo la DHL kutoka Ujerumani.
Mkurugenzi wa Idara ya Mawasiliano wa wizara hiyo Mhandisi Clarence Chikweleza amewahimiza watendaji wa shirika hilo kuendelea kufanya kiufanisi kufikia malengo waliyojiwekea na kuwasisitiza kutoa ushirikiano kwa Waziri Dkt. Ndungulile
Hakuna maoni
Chapisha Maoni