Zinazobamba

KITUO CHA TAARIFA NA MAARIFA MAJOHE CHAWAFUNDA WAJASIRIAMALI WA KATA YA KIVULE JINSI YA KUTENGENEZA MKAA MBADALA NA BIDHAA ZA UREMBO.

Na Vicent Macha 

Wajasiriamali wa kata ya Kivule wametakiwa kuzichangamkia fursa za mafunzo mbalimbali ya ujasiriamali, ili waweze kujikomboa katika maisha yao na waondokane na dhana ya kusema maisha ni magumu.

Mwenyekiti wa kituo cha Taarifa na Maarifa Majohe Bi. Amina Nasoro akitoa ufafanuzi wa jambo fulani katika mafunzo ya ujasiriamali yaliyofanyika kata ya kivule mkoani Dar es salaam hapo jana.

Hayo yamesemwa Mapema jana na Mwenyekiti wa Kituo cha Taarifa na Maarifa kata Majohe Bi. Amina Nasoro wakati kituo hicho kikitoa mafunzo ya ujasiriamali kwa wakazi wa kata Kivule iliyopo mkoani Dar es salaam.

Mwenyekiti huyo amesema kuwa sababu ya wao kuweza kutoa elimu hii ni kuweza kubadilishana uzoefu kwa kile ambacho wao wanakijua wakaona wawashirikishe na wenzao wa Kivule, ili ikitokea na Kivule wakipata elimu nyingine waweze kuwashirikisha na wao lengo likiwa ni kukuza vipato na kuendelea kudumisha ujenzi wa nguvu za pamoja.

Ameendelea kusisitiza njia rahisi ya utengenezaji wa bidhaa hizi kwa kusema haya.

“leo tupo kata ya kivule tumekuja kuwapa elimu wakazi wa hapa jinsi ya kujiongezea kipato kwa kazi mbalimbali za mikono ambazo ni rahisi sana kama kutengeneza mkaa wa maboksi, mkaa wa chenga za mkaa, udi, mafuta ya kujipaka, kutengeneza virago pamoja na mapambo ya aina mbalimbali” Amesma Amina.

Ameongeza kuwa mafunzo hayo ni sehemu ya mrejesho wa mafunzo ya ABCD waliyopewa na TGNP ambayo yanataka wajasiriamali au watanzania kuweza kuongeza kipato kupitia rasilimali zinazowazunguka katika mazingira yao ya kawaida.

Naye mfanyabishara wa chakula katika shule ya Sekondari Kerezange iliyopo kata ya Kivule Bi. Happiness Masesa amesema kuwa mafunzo hayo ya mkaa yatawasaidia sana hususani wao wanaofanya kazi za kupika shuleni, Kwani kwa sasa kuni upatikanaji wake umekuwa na changamoto kubwa hivyo waoa wataitumia vizuri fursa ya mkaa mbadala.

Na mwisho amemaliza kwa kusema kuwa yeye pia ni mjasiriamali wa pilipili na alikuwa akitamani kupata elimu ya kufanya  pilipili zake ziweze kukaa muda mrefu bila kuharibika, lakini leo ameweza kupata elimu hiyo kutoka kwa wajasiriamali hao kutoka Majohe.

Kwa upande wake mwalimu wa shule ya Kerezange sekondari Veronika Julius amesema amefurahishwa na mafunzo hayo kwani vitu walivyofundishwa vitawasaidia kupata kipato cha ziada nje ya kazi zao wanazozifanya.

Ameongeza kuwa pia mafunzo haya yatasaidia kuokoa fedha ambazo zilikuwa zikipote bila sababu kwani badala ya kununua mkaa sasa hivi wakazi kivule watatafuta maboksi ambayo yanatupwa ovyo pamoja na chenga za mkaa ili kuweza kutngeneza mkaa huu mbadala.

Mwalimu wa ujasiriamali Salma Msabaha akitoa ufafanuzi wa jambo kwa wajasiriamali kata Kivule katika mafunzo yaliyofanyika jana mkoani Dar es salaam.  
Mwenyekiti wa kituo cha Taarifa na Maarifa Majohe Bi. Amina Nasoro akifundisha namna ya kutengeneza mkaa kupitia chenga za mkaa na uji wa Ngano.
Mwalimu wa ujasiriamali Zakayo Kahamba akifundisha jinsia ya kutengeneza Kirago cha kufutia miguu kwa kutumia uzi wa vitambaa na na kiroba.

Mafunzo yakiendelea kwa wajasiriamali wa kata ya Kivule hapa wakifundishwa namna ya kutengeneza mafuta ya mgando.





Hakuna maoni