Zinazobamba

SAMATTA jinsi alivyokuwa nembo ya mpira wa Tanzania

 



Kahema J Fimbo

Ukizungumzia nembo ya mpira wa Tanzania kwa sasa kwa kiwango kikubwa utamzungumzia mtoto wa mbagala kimbangulile Mbwana Ally Samatta.

Samatta amejitahidi kuitangaza Tanzania katika soka la kimataifa na pia amejitahidi kujijengea jina na heshima katika maeneo yote hayo ambayo amepita.

 Alianzia soka lake katika viunga vya mbagala na kisha akahamia simba ambako hakukaa sana akahamia kwa matajiri wa soka la Congo yaani TP Mazembe.

Huko congo alijijengea heshima na ufalme wake ambako alikuwa hakauki kuzifumania nyavu na hali iliyompelekea mpaka kupewa tuzo ya mchezaji bora wa afrika katika wale wanaocheza ligi za ndani ya afrika.

Katika siku ya tuzo, alipewa tuzo hiyo sambamba na Pierre Emmerick Aubemayang ambaye naye alipewa tuzo jumla ya mchezaji bora wa afrika.

Katika kila eneo ambalo amepita Mbwana amekuwa ni mtu ambaye anaacha alama.

Jitihada zake katika mchezo wa soka zilimfanya aingie katika rada za wababe wa ubelgiji, timu ya KRC GENK ambao walimsajili na kumhamishia makazi yake huko kwa wabelgiji.

Ndani ya nchi ya ubelgiji nako aliendeleza ufalme wake na kufunga magoli mengi na kujiweka katika kitabu cha magwiji waliowahi kupita katika klabu hiyo.

Hapo Ubelgiji kulimfungulia njia ya kuweza kushiriki katika ligi ya Europa ambako alizifunga na kuingiza jina lake na kuwa ni mtanzania wa kwanza kufunga goli katika shindano hilo na hakukaa sana timu yake ikabeba ubingwa wa ligi ya Ubelgiji na kisha kumpatia nafasi ya yeye kushiriki katika ligi ya klabu bingwa ulaya.

Katika ligi ya klabu bingwa ulaya alipangwa kundi moja na timu kubwa za ulaya kama vile Liverpool na Napoli na kujikuta akicheza mechi moja na mastaa wakubwa barani ulaya na huku akikabwa na mabeki bora kwa sasa katika viwango vya dunia yaani nawazungumzia Virgil Van Dijk pamoja na Wengineo.

Katika klabu ya mabingwa alizidi kupandisha thamani yake kwa kumfunga kipa bora Alisson Becker wa Liverpool.

Ufundi wake wa kupachika mabao uliwafanya mabosi wa Aston Villa kumsajili katika timu yao na kisha kumhamishia nchi ya uingereza. Alipofika Uingereza amecheza kidogo na hakuweza kuwika sana na wakongwe hao wa uingereza wakamhamishia katika nchi ya uturuki katika klabu ya Fenerbache kwa mkopo ambapo anacheza huko.

Kuna faida nyingi sana kwa watanzania kwa Samatta kununuliwa nchini Uturuki. Mosi kwa kucheza huko kutamsaidia kutengeneza fursa kwa wachezaji wa kitanzania kusajiliwa huko.

 Kwa kitendo cha yeye kusajiliwa huko ametambulisha vilabu ya uturuki kwamba nchi ya Tanzania ina vipaji vya soka na kwa sasa maskauti wa vipaji wa timu za soka huko uturuki watakuwa wameweka rada zao kwa vijana wa kitanzania ambao watakuwa wanaibukia.

Pili amefungua fursa za utalii kwa nchi ya Tanzania kwani kuna waturuki ambao wataijua nchi ya Tanzania kupitia yeye na watakuwa wana shauku ya kuja kutembelea Tanzania kuja kujionea vivutio vya utalii.

Kwa fursa hizo nina rai kwa shirikisho la mpira lishirikiane vizuri na bodi ya utalii kualika vilabu vya nchi ya uturuki kuja kucheza mechi zao za kujiandaa na msimu(pre-season) huku Tanzania na kisha baada ya kucheza mechi hizo wapate fursa ya kwenda kuandalia vivutio vya utalii.


No comments