Ajinyonga mpaka kufa huku akiacha ujumbe kuwa mkewe ni mshirikina na si mwaminifu katika ndoa yake
Samweli Mbingilwa (54)
almaarufu kama Kamanda amejinyonga hadi kufa akiacha ujumbe kuwa ‘mke wangu si
mwaminifu katika ndoa na ananifanyia mambo ya kishirikina.’
Mwili wa Mbingilwa
aliyekuwa mkazi wa Tambukareli mjini Mpanda ulikutwa kwenye kiti huku kamba ya
chandarua aliyojifunga juu na kujining’iniza ikiwa kimekatika.
Mke wa marehemu, Maria
Nswima alisema siku kadhaa kabla ya kujiua, mumewe alichoma moto nguo zake huku
mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Tambukareli, Selestino Shauritanga akisema
Mbingilwa aliwahi kunywa dawa akitaka kujiua.
Akieleza zaidi,
Shauritanga alisema taarifa za tukio hilo alipata kwa watoto wa marehemu
waliomweleza kuwa baba yao amefariki lakini hawakumjuza chanzo cha uamuzi huo.
Hata hivyo, mwenyekiti huyo alikiri kuwa wanandoa hao walikuwa na ugomvi
uliotokana na wivu wa mapenzi.
“Siyo mara ya kwanza
kusuluhisha ugomvi kati yao, walikuwa wafanyabiashara wa pombe za kienyeji na
kilabu kipo nyumbani kwao, kwa hiyo wateja wakinunua na kuongea na mkewe
(Mbingilwa) alikuwa anachukia,” alisema Shauritanga.
Mwenyekiti huyo alifafanua kuwa marehemu, enzi za uhai wake, aliwahi kunywa dawa ili ajiue lakini akaokolewa mapema.
Kamanda wa polisi Mkoa wa
Katavi, Abdi Issangu alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema “ni tukio
la kweli na mwanaume huyo ameacha ujumbe unaosema, ‘mke wangu siyo mwaminifu
katika ndoa na ananifanyia mambo ya kishirikina.”
Akieleza ilivyokuwa,
Maria alisema Novemba 25 mwaka huu mumewe alikwenda kilabuni lakini kesho yake
kuliibuka ugomvi kati yao na akamtishia maisha.
“Nilimpisha nyumbani ila
saa mbili usiku nikarudi akaniambia leo ni siku yako ya mwisho, nikamuuliza
kivipi akajibu ya mwisho kuishi. Kuona hivyo niliamua kwenda kwa mwenyekiti
lakini sikumkuta...baada ya kurudi nyumbani nikakuta amechoma nguo zangu zote
moto na kukatakata masufuria pamoja na kupasua mabakuli yote.”
Kutokana na hali hiyo,
alisema “nilienda kituo cha polisi nikaeleza na kupewa wito niliompelekea
balozi akampa lakini watoto wakaniambia ameichana, hii hapa. Nikavichukua hivyo
vipande na kuvipeleka kwa mwenyekiti akaniambia rudi tena polisi,
nikarudi...tangu siku hiyo niliamua kuishi kwa shangazi yangu,” alisema Maria.
Alisema Desemba 5 saa 11
jioni mtoto wake alikwenda kumpa taarifa kuwa baba yao amejinyonga chumbani
kwake.
“Baada ya kufika nilikuta
ametumia chandarua ambacho kilikuwa imekatika na yeye alikuwa amekaa kwenye
kiti akiwa amefariki tayari. Ilikuwa kawaida yake kwenda kunywa pombe akirudi
lazima kelele ziwepo lakini baadaye zinaisha,” alisema Maria.
licha ya uvumilivu
aliounyesha kwa miak amingi waliyoishi pamoja, Maria alisema “awamu hii
alizidisha, nikaamua kuondoka. Nimezaa naye watoto saba, naumia kwakuwa
nilimzoea. Sikuwahi kufikiria kama anaweza kujinyonga,” alisema.
Kaka wa marehemu, Daniel
Peter (75) anayeishi Kilimahewa mjini hapa alisema amemshangaa ndugu yao
kuchukua uamuzi huo ambao hakuwahi kuutamka au kuonyesha dalili za kuutekeleza.
“Ni mdogo wangu wa
mwisho, alikuwa dereva wa magari madogo ya abiria kwa muda mrefu lakini
alipumzika, nilishangaa nilipopigiwa simu kuwa amefariki. Eti amejinyonga kwa
kutumia kamba ya neti. Nilikuwa nakutana naye, kuna wakati alikua na furaha
mwingine hana, baada ya kumpekua wakaona karatasi ya ujumbe wakadai
nitafuatilia kwa hiyo sijui kilichokuwa kimeandikwa,” alisema Peter.

No comments
Post a Comment