WOSIA WA ABOUD JUMBE WATELEKEZWA,CCM WAAMUA KUFANYA HIVI,SOMA HAPO KUJUA
![]() |
| Safari ya mwisho ya Alhaj Aboud Jumbe, aliyekuwa Rais wa awamu ya pili ZanzibaR |
KAULI ya Alhaj Aboud Jumbe, aliyekuwa Rais wa
Zanzibar ya kugoma kuzikwa ‘kifalme’ kama ilivyo kwa viongozi wengine wa
kitaifa, imetekelezwa na Serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM),anaandika Hamis Mguta.
Taarifa ya Rais Jumbe kutotaka
kuzikwa kifalme ilisambazwa kwa haraka jana baada ya kufariki kwake jambo
ambalo lilizua mjadala hasa kutokana na wadhifa wa urais aliowahi kuwa nao
ndani ya nchi.
Rais Jumbe ambaye alikuwa rais wa awamu ya pili Zanzibar,
alifariki jana mchana nyumbani kwake Mji Mwema, Kigamboni jijini Dar es Salaam
na kuzikwa leo Migombani, Unguja.
Miongoni mwa wosia wake ni kutotaka kuzikwa kwa
taratibu za kiseriali ikiwa ni pamoja na jeneza lake kufunikwa kwa Bendera ya
Tanzania, Bendera ya CCM, kupigiwa mizinga pia kubebwa na watu maalum.
“Sitaki bendi, sitaki mizinga, sitaki maombolezo
wala lolote lingine lenye hata chembe ya kufuru,” ni sehemu ya wosia wake
uliosambazwa kwenye mitandao ya kijamii jana.
Ni kawaida kwa viongozi wa juu taratibu za mazishi
yao kuambatana na jeneza kufunikwa kwa bendera ya taifa, kupigiwa mizinga jambo
ambalo kwa Rais Jumbe hakulitaka.
Maisha ya Rais Jumbe baada ya kung’olewa urais
yamesikitisha wengi, Serikali ya CCM imemdhalilisha vya kutosha, imemtenga na
kumpuuza mpaka uhai wake unafika tamati. Ameondoka akijua kwamba, hana thamani.
Hana thamani kwa Wazanzibari wahafidhina, hana
thamani kwa wenye maslahi binafsi bara na visiwani pia hana thamani kwa
wasiojua thamani yao ndani ya Zanzibar.
Rais Jumbe amezikwa huku akiwa na fundo kwenye moyo
wake, ameondoka akiwa anasononeka. Ni kwa kuwa thamani yake kwa Watanzania
hususani Wazanzibari imepigwa teke na CCM.
Amewaacha wenye tamaa ya dunia, wanaojali mkono
kwenda kinywaji pasi na uhai wa vizazi vyao, amewaacha ‘wababe’ wanaobebwa na
vikosi vya kijeshi. Kwao haki si chochote isipokuwa madaraka.
Serikali ya CCM haina cha kujitetea, ndiyo
iliyomdhalilisha Rais Jumbe na ndivyo inadhalilisha wale walio na mtazamo
chanya na Zanzibar. Manyanyaso ya walio na mtazamo wa Rais Jumbe hayajakoma na
hayatokoma.
Kiongozi huyo ndiye aliyekuwa mwasisi wa Serikali ya
Mapinduzi Zanzibar muda mfupi baada ya Mapinduzi ya Januari 1964, pia alikuwa
mwasisi wa Muungano uliozaa Tanzania na amaefanya kazi kubwa ya kuwafungua macho
Wazanzibari.
Historia ya Rais Jumbe visiwani Zanzibar inaumiza
kwa wapenda haki. Inatekenya fikra za mabadiliko hususani wakati huu ambao
taifa linaelekea kuzama katika sauti ya mtu mmoja.
Udhalili wa CCM kwa Rais Jumbe ulishika hatamu
Januari 1984 baada ya Halmashauri Kuu (NEC-CCM), iliyokutana Dodoma kwa dharura
na kuafikia kumvua madaraka.
Alivuliwa madaraka ya urais wa Zanzibar, Uenyekiti
wa Baraza la Mapinduzi, Umakamu wa Rais wa Tanzania na Umakamu Mwenyekiti wa
CCM Taifa. Akabaki mtupu.
Rais Jumbe alivuliwa madaaka yote kwa sababu tu
alihoji Muungano. Ni jambo ambalo Mwalim Julius Nyerere hakuwa akitaka kuona
mjadala wake ukishika hatamu.
Rais Jumbe alikuwa rais wa awamu ya pili Zanzibar.
Dhambi kubwa kwake ilikuwa kunyimwa uhuru- kuwekwa chini ya kizuizi cha
nyumbani kwake.
Habari hii kwahisani ya Mwanahalisi Oline
