Zinazobamba

TAMASHA LA TWENDE ZETU KWA YESU KUFANYIKA JUNI 13 MWAKA HUU, WANANCHI WAOMBWA KUJITOKEZA KWA WINGI

Na Mwandishi Wetu 

Tamasha la Twende Zetu kwa Yesu 2026 linatarajiwa kufanyika Juni 13 katika viwanja vya Tanganyika Packers jijini Dar es Salaam, likiwakusanya vijana elfu 45 kutoka ndani na nje ya nchi.

Akizungumza na waandishi wa habari leo, Juni 11, 2026, jijini Dar es Salaam, Naibu Katibu Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Mashariki na Pwani (DMP), Dk. Wilbroad Mastai, amesema tamasha hilo halijalenga Wakristo pekee bali jamii yote kwa ujumla.

Hivyo, amewataka vijana kushiriki kwa wingi kwani vijana ni nguvu muhimu kwa maendeleo ya Kanisa na Taifa kwa ujumla.Aidha, amewahimiza vijana kutumia fursa ya tamasha hilo kuinua vipaji ili kukuza vipaji vyao, kujenga maadili mema na kubadili mitazamo yao ili iendane na matarajio mema ya jamii na mafundisho ya Mungu bila kujali tofauti za itikadi za kidini.

"Tamasha hili limetimiza miaka 13 na lilianza na washiriki elfu tano, lakini kwa sasa limekuwa na mafanikio makubwa kwani linawajengea vijana uwezo wa kimwili na kiroho na kumcha Mungu," amesema Dk. Mastai.

Aidha, ameongeza kuwa waimbaji maarufu wa nyimbo za injili watakuwepo, akiwemo Rose Muhando na wengine wengi.Kwa upande wake, Mkuu wa Idara ya Mission na Uinjilisti wa Dayosisi hiyo, Henry Mwinuka, amesema hali ya usalama katika tamasha hilo inatosha, hivyo watu mbalimbali, hususan vijana, wajitokeze kwa wingi.

No comments